22
1 Ikawa kwamba baada ya mambo hayo Mungu akampima Abraham. Akamwambia, “Abraham!” Abraham akasema, “Mimi hapa.”
2 Kisha Mungu akasema, “Mchukue mwanao, mwanao wa pekee, umpendaye, Isaka, na uende katika nchi ya Moria. Mtoe kama sadaka ya kuteketezwa mahali pale juu ya moja ya milima hiyo, ambayo nitakwambia.”
3 Kwa hiyo Abraham akaamka asubuhi na mapema, akatandika punda wake, akawachukuwa vijana wake wawili, pamoja na Isaka mwanawe. Akakata kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kisha akapanga safari kwenda mahali ambapo Mungu alimwambia.
4 Siku ya tatu Abraham akatazama juu na akaona mahali pakiwa mbali.
5 Abraham akawambia vijana wake, “kaeni hapa pamoja na punda, mimi pamoja na Isaka tutakwenda pale. Tutaabudu na kisha tutarudi hapa penu.”
6 Ndipo Abraham akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa akaziweka juu ya Isaka mwanawe. Mkononi mwake akachukua moto na kisu; na wote wawili wakaondoka pamoja.
7 Isaka akazungumza na Abraham baba yake akisema, “Baba yangu,” naye akasema, “ Ndiyo mwanangu.” Akasema, “Tazama huu ni moto na kuni, lakini yuko wapi mwanakondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?”
8 Abraham akasema, “Mungu mwenyewe atatupatia mwanakondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, mwanangu.” Kwa hiyo wakaendelea, wote wawili pamoja.
9 Walipofika mahali ambapo Mungu alikuwa amemwambia, Abraham akajenga madhabahu pale na akaweka kuni juu yake. Kisha akamfunga Isaka mwanawe, na akamlaza juu ya madhabahu, juu ya zile kuni.
10 Abraham akanyoosha mkono wake akachukua kisu ili kumuua mwanawe.
11 Ndipo malaika wa Yahwe akamwita kutoka mbinguni na kusema, “Abraham, Abraham!” naye akasema, “Mimi hapa.”
12 Akasema, “usinyooshe mkono wako juu ya kijana, wala usifanye jambo lolote kumdhuru, kwa kuwa sasa najua unamcha Mungu, kwa kuona kuwa hukumzuilia mwanao, mwanao wa pekee, kwa ajili yangu.”
13 Abraham akatazama juu na tazama, nyuma yake kulikuwa na kondoo mume amenaswa pembe zake kichakani. Abraham akaenda akamchukua kondoo na akamtoa kama sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.
14 Kwa hiyo Abraham akapaita mahali pale, Yahwe atatoa,” na panaitwa hivyo hata leo. “Juu ya mlima wa Yahwe itatolewa.”
15 Malaika wa Yahwe akamwita Abraham kwa mara ya pili kutoka mbinguni
16 na kusema - Hiki ni kiapo cha Yahwe, “Kwa ajili ya nafsi yangu nimeapa kwamba kwa kuwa umefanya jambo hili, na hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,
17 hakika nitakubariki na nitakuzidishia uzao wako kama nyota za angani, na kama mchanga ulioko kwenye ufukwe wa bahari; na uzao wakowatamiliki lango la adui zao.
18 Kupitia uzao wako mataifa yote ya dunia watabarikiwa, kwa sababu umetii sauti yangu.”
19 Kwa hiyo Abraham akarejea kwa vijana wake, na wakaondoka wakaenda pamoja Beerisheba, hivyo akakaa Beerisheba.
20 Ikawa kwamba baada ya mambo haya ambayo Abraham aliambiwa, “Milka amemzalia pia watoto, ndugu yako Nahori.”
21 Hawa walikuwa ni Usi mzaliwa wa kwanza, Busi ndugu yake, Kemueli aliye mzaa Aramu,
22 Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu, na Bethueli.
23 Bethuel akamzaa Rebeka. Hawa walikuwa ni wale watoto wanane ambao Milka alizaa kwa Nahori, ndugu yake na Abraham.
24 Suria wake, ambaye aliitwa Reuma, pia akamzaa Teba, Gahamu, Tahashi, na Maaka.