24
1 Basi Abraham alikuwa mzee sana na Yahwe akawa amembariki katika mambo yote.
2 Abraham akamwambia mtumwa wake, ambaye alikuwa mkubwa kuliko wote wa nyumbani mwake na mkuu wa vyote alivyo kuwa navyo.”Weka mkono wako chini ya paja langu
3 na nitakufanya uape kwa Yahwe, Mungu wa Mbingu na nchi, kwamba hutampatia mwanangu mke kutoka kwa mabinti wa Wakanaani, miongoni mwao wale nikaao kati yao.
4 Lakini utakwenda kwenye nchi yangu, na kwa ndugu zangu, na kumtafutia mwanangu Isaka mke.”
5 Yule mtumwa wake akamwambia, “Itakuwaje ikiwa mwanamke hatakuwa tayari kufuatana nami hadi katika nchi hii? Je nitamrudisha mwanao katika nchi ambayo ulitoka?”
6 Abraham akamwambia, “Hakikisha kwamba hutamrudisha mwanangu kule!
7 Yahwe, Mungu wa mbingu, ambaye alinitoa mimi kutoka katika nyumba ya baba yangu na kutoka katika nchi ya ndugu zangu, na ambaye aliniahidia kwa kiapo maalumu akisema, 'Nitawapa uzao wako nchi hii,' atatuma malaika wake mbele yako, na utapata mke kwa ajili ya mwanangu kutoka huko.
8 Lakini ikiwa mwanamke hatakuwa tayari, ndipo utakuwa huru katika hiki kiapo changu. Cha muhimu tu ni kwamba usije ukamrudisha mwanangu huko.”
9 Kwa hiyo mtumwa akaweka mkono wake jini ya paja la Abraham bwana wake, na akaapa kuhusiana na jambo hili.
10 Mtumwa akachukua ngamia kumi wa bwana wake na akaondoka. Akachukua pia aina zote za zawadi kutoka kwa bwana wake. Akaondoka na kwenda katika mkoa wa Aramu Naharaimu, mji wa Nahori.
11 Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji. Ilikuwa jioni wakati ambao wanawake huenda kuchota maji.
12 Kisha akasema, “Yahwe, Mungu wa bwana wangu Abraham, anijalie kufanikiwa leo na aoneshe agano la uaminifu kwa bwana wangu Abraham.
13 Tazama, nimesimama hapa karibu na chemchemi ya maji na binti za watu wa mji wanakuja kuteka maji.
14 Na itokee hivi kwamba. Nikimwambia msichana, tafadhari tua mtungi wako ili niweze kunywa maji,' na akiniambia, 'Kunywa, na kwamba nitawanywesha ngamia wako pia,' huyo ndiye awe ambaye umemchagulia mtumwa wako Isaka. Kwa njia hii nitajua kuwa umeonesha agano la uaminifu kwa bwana wangu.”
15 Ikawa kwamba hata kabla hajamaliza kuzungumza, tazama, Rebeka akaja akiwa na mtungi wake wa maji begani mwake. Rebeka alizaliwa na Bethueli mwana wa Milka, mke wa Nahori, ndugu yake na Abraham.
16 Msichana huyu alikuwa mzuri na alikuwa bikira. Hapana mwanaume aliye kuwa amekwisha lala naye. Akashuka kisimani na kuujaza mtungi wake, na kupanda juu.
17 Kisha mtumwa yule akakimbia kumlaki yule msichana, na kusema, “Tafadhari nipatie maji kidogo ya kunywa kutoka katika mtungi wako.”
18 Akasema, “kunywa tafadhari bwana wangu,” na kwa haraka akatua mtungi wake juu ya mkono wake, na akampatia maji ya kunywa.
19 Alipokuwa amemaliza kumpatia maji, akasema, “Nitachota maji kwa ajili ya ngamia wako pia, mpaka watakapomaliza kunywa.”
20 Hivyo akaharakisha akamwaga maji yaliyokuwa mtungini kwenye chombo cha kunywshea mifugo, kisha akakimbia tena kisimani kuchota maji, na kuwanywesha ngamia wake wote.
21 Yule mtu akamtazama msichana akiwa kimya kuona kama Yahwe amefanikisha njia yake au la.
22 Ngamia walipomaliza kunywa maji, yule mtu akaleta pete ya pua ya dhahabu yenye uzito wa nusu shekeli, na bangili mbili za dhahabu kwa ajili ya mikono yake zenye uzito wa shekeli kumi,
23 akamuuliza, “wewe ni binti wa nani? Niambie tafadhali, Je kuna nafasi nyumbani mwa baba yako kwa ajili yetu kupumzika usiku?”
24 Akamwambia, “Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, ambaye alimzaa kwa Nahori.”
25 Akasema pia, “Tunayo malisho tele na chakula, na iko nafasi kwa ajili yako kulala usiku.”
26 Kisha yume mtu akainama chini na kumwabudu Yahwe.
27 Akasema, “Abarikiwe Yahwe, Mungu wa bwana wangu Abraham, ambaye hakuacha agano lake la uaminifu na kweli yake mbele ya bwana wangu. Kwa vile Yahwe ameniongoza moja kwa moja kwenye nyumba ya ndugu zake bwana wangu.”
28 Kisha yule msichana akakimbia na kwenda kuwaeleza watu wa nyumba ya mama yake juu ya mambo yote haya.
29 Na sasa Rebeka alikuwa na kaka yake, jina lake aliitwa Labani. Labani akakimbia kwa yule mtu aliye kuwa nje barabarani karibu na kisima.
30 Akisha kuona hereni ya puani pamoja na zile bangili kwenye mikono ya dada yake, na kusikia maneno ya Rebeka dada yake, “Hivi ndivyo yule mtu alicho niambia,” alikwenda kwa yule mtu, na, Tazama, alikuwa amesimama karibu na ngamia pale kisimani.
31 Labani akasema, “Njoo, wewe uliye barikiwa na Yahwe. Kwa nini umesimama nje? nimekwisha andaa nyumba, pamoja na mahali kwa ajili ya ngamia.”
32 Kwa hiyo yule mtu akaingia ndani ya nyumba na akashusha mizigo kutoka kwa wale ngamia. Ngamia wakapatiwa malisho na chakula, na maji yakatolewa kuosha miguu yake pamoja na miguu ya wale watu aliokuwa pamoja nao.
33 Wakaandaa chakula mbele yake ale, lakini akasema, “Sitakula mpaka niseme kile ninacho paswa kusema.” Kwa hiyo Labani akmwambia, “Sema.”
34 Akasema, “Mimi ni mtumwa wa Abraham.
35 Yahwe amembariki sana bwana wangu na amekuwa mtu mkuu. Amempatia mifugo na makundi ya wanyama, fedha, dhahabu, watumwa wa kiume na watumwa wa kike, pamoja na ngamia na punda.
36 Sara, mke wa bwana wangu, alimzalia mwana bwana wangu alipokuwa mzee, na amempatia mwanawe kila kitu anachomiliki.
37 Bwana wangu aliniapisha, akisema, “Usije ukampatia mwanangu mke kutoka kwa mabinti wa Wakanaani, ambao kwao nimefanya makazi.
38 Badala yake, lazima uende kwa familia ya baba yangu, na kwa ndugu zangu, na kupata mke kwa ajili ya mwanangu.'
39 Nikamwambia bwana wangu, pengine mwanamke huyo asikubali kufuatana nami.'
40 Lakini akaniambia, Yahwe, ambaye ninakwenda mbele yake, atatuma malaika wake pamoja nawe na atakufanikisha njia yako, kwamba utapata mke kwa ajili ya mwangu kutoka miongoni mwa ndugu zangu na kutoka katika ukoo wa baba yangu.
41 Lakini utakuwa huru katika kiapo changu ikiwa utafika kwa ndugu zangu na wasikuruhusu kuja naye. Ndipo utakuwa huru katika kiapo changu.
42 Hivyo nimefika leo kisimani, na nikasema, 'O Yahwe, Mungu wa bwana wangu Abraham, tafadhari, ikiwa kweli umekusudia kuifanya safari yangu kuwa yenye kufanikiwa -
43 tazama niko hapa nimesimama karibu na kisima cha maji - na iwe kwamba binti ajaye kuchota maji, nitakaye mwambia, “Tafadhari unipatie maji kidoka kutoka kwenye mtungi wako ninywe,” mwanamke atakaye niabia,
44 “Kunywa, na nitakuchotea pia maji kwa ajili ya ngamia wako” - na awe ndiye ambaye wewe Yahwe, umemchagulia mtoto wa bwana wangu.”
45 Ikawa hata kabla sijamaliza kuzungumza moyoni mwangu, Tazama, Rebeka akaja na mtungi wake juu ya bega lake akashuka chini kisimani akachota maji. Hivyo nikamwambia, 'Tafadhari nipatie maji ninywe.'
46 Ndipo kwa haraka alipoushusha mtungi wake begani mwake na akasema, 'Kunywa, na pia nitawapatia maji ngamia wak.' Kwa hiyo nikanywa, na akawanywesha ngamia pia.
47 Nikamuuliza na kusema, 'Wewe ni binti wa nani?' Akasema, 'Binti wa Bethueli, Mwana wa Nahori, ambaye Milka alizaa kwake.' Kisha nikamwekea pete puani mwake pamoja na bangili mikononi mwake.
48 Kisha nikainama chini nikamwabudu Yahwe, na kumbariki Yahwe, Mungu wa bwana wangu Abraham, ambaye ameniongoza katika njia sahihi kumpata binti wa ndugu za bwana wangu kwa ajili ya mwanawe.
49 Kwa hiyo, ikiwa mko tayari kumfanyia rehema na kweli, niambieni. Lakini kama sivyo, niambieni, ili kwamba niweze kwenda upande wa kulia, au kushoto.”
50 Ndipo Labani na Bethueli wakajibu na kusema, “Jambo hili limetoka kwa Yahwe; hatuwezi kusema kwako aidha neno baya au zuri.
51 Tazama, Rebeka yu mbele yako. Mchukue na uende, ili awe mke wa mtoto wa bwana wako, kama Yahwe alivyosema.”
52 Mtumwa wa Abraham aliposikia maneno yao, akainama mwenyewe chini ardhini kwa Yahwe.
53 Mtumwa akaleta vipande vya fedha na vipande vya dhahabu, na nguo, akampatia Rebeka. Akampatia pia kaka yake na mama yake zawadi zenye thamani.
54 Kisha yeye na watu aliokuwa nao wakala na kunywa. wakakaa pale mpaka usiku, na walipoamka asubuhi, akasema, Niruhusuni niende kwa bwana wangu.”
55 Kaka yake na mama yake wakasema, mwache binti abaki nasi kwa siku chache zingine, angalau siku kumi. baada ya hapo anaweza kwenda.”
56 Lakini akawambia, msinizuie, kwa kuwa Yahwe amefanikisha njia yangu. Niruhusuni niende kwa bwana wangu.”
57 Wakasema, “Tutamwita binti na kumuuliza.”
58 Kwa hiyo wakamwita Rebeka na kumuuliza, “Je utakwenda na mtu huyu?” Akajibu, “Nitakwenda.”
59 Kwa hiyo wakampeleka dada yao Rebeka, pamoja na watumishi wake wa kike, kwenda njiani pamoja na mtumishi wa Abraham na watu wake.
60 Wakambarikia Rebeka, na wakamwambia, “Ndugu yetu, na uwe mama wa maelfu na wa makumi elfu, uzao wako upate kumiliki lango la wale wanao wachukia.”
61 Kisha Rebeka akasimama, yeye na watumishi wake kwa hesabu ya ngamia, na wakamfuata yule mtu. Hivyo watumishi wakamchukua Rebeka, na wakaenda zao.
62 Nyakati hizo Isaka alikuwa anakaa katika Negebu, na alikuwa tu amerejea kutoka Beerlahairoi.
63 Isaka akaenda kutafakari shambani jioni. Alipotazama akaona, natazama, kulikuwa na ngamia wakija!
64 Rebeka akatazama na alipomwona Isaka, akaruka kutoka kwenye ngamia.
65 Akamwambia mtumwa, “mtu huyo ni nani anaye tembea shambani akija kutupokea?” Mtumwa akasema, “Ni bwana wangu.” Hivyo Rebeka akachukua shela yake akajifunika.
66 Mtumwa akamwambia Isaka mambo yote ambayo amefanya.
67 Kisha Isaka akamleta katika hema ya Sara mama yake na akamchukua Rebeka, na akawa mke wake, na akampenda. Kwa hiyo Isaka akafarijika baada ya kifo cha mama yake.