26
1 Basi njaa ikatokea katika nchi, mbali na njaa ya kwanza iliyotokea siku za Ibrahimu. Isaka akaenda kwa Abimeleki, mfalme wa Wafilisiti huko Gerari.
2 Basi Yahwe akamtokea na kumwambia, “Usishuke kwenda Misri; kaa katika nchi niliyokuambia.
3 Kaa katika nchi hii hii niliyokuambia, nami nitakuwa pamoja nawe na kukubariki; kwani kwako wewe na uzao wako, nitawapa nchi hii yote, nami nitatimiza kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako.
4 Nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote. Kupitia uzao wako mataifa yote ya dunia yatabarikiwa.
5 Nitalifanya hili kwa sababu Ibrahimu aliitii sauti yangu na kutunza maelekezo yangu, amri zangu na sheria zangu.”
6 Hivyo Isaka akakaa Gerari.
7 Watu wa eneo hilo walipomwuliza juu ya mke wake, alisema, “Yeye ni dada yangu.” Aliogopa kusema, “Yeye ni mke wangu,” kwa kuwa alidhani, “Watu wa nchi hii wataniua ili wamchukue Rebeka, kwa kuwa ni mzuri wa uso.”
8 Baada ya Isaka kuwa amekaa pale kwa muda mrefu, Ikatukia kwamba Abimeleki mfalme wa Wafilisiti alichungulia katika dirisha. Tazama, akamwona Isaka akimpapasa Rebeka, mke wake.
9 Abimeleki akamwita Isaka kwake na kusema, “Tazama, kwa hakika yeye ni mke wako. Kwa nini ulisema, 'Yeye ni dada yangu?” Isaka akamwambia, “Kwa sababu nilidhani mtu mmoja aweza kuniua ili amchukue.”
10 Abimeleki akamwambia, “Ni jambo gani hili ulilotufanyia? Mmojawapo wa watu angeweza bila shaka kulala na mke wako, nawe ungeweza kuleta hatia juu yetu.”
11 Hivyo Abimeleki akawaonya watu wote na kusema, “Mtu yeyote atakayemgusa mtu huyu au mke wake atauwawa.”
12 Isaka akapanda mazao katika nchi hiyo na kuvuna mwaka huo vipimo mia, kwa kuwa Yahwe alimbariki.
13 Mtu huyo akawa tajiri, naye akaongezeka zaidi hata akawa mkuu sana.
14 Alikuwa na kondoo na ngombe na familia kubwa. Wafilisiti wakamwonea wivu.
15 Basi visima vyote watumishi wa baba yake walikuwawamevichimba katika siku za Ibrahimu baba yake, Wafilisiti wakavikatalia kwa kwa kuvijaza kifusi.
16 Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kati yetu, kwa kuwa wewe una nguvu kuliko sisi.”
17 Hivyo Isaka akaondoka pale na kukaa katika bonde la Gerari, na kuishi pale.
18 Kwa mara nyingine tena Isaka akachimba visima vya maji, vilivyokuwa vimechimbwa siku za Ibrahimu baba yake. Wafilisiti walikuwa wamevizuia baada ya kufa kwake Ibrahimu. Isaka akaviita visima kwa majina aliyokuwa ameviita baba yake.
19 Watumishi wa Isaka walipochimba katika bonde, wakaona kisima cha maji yaliyokuwakuwa yakibubujika.
20 Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka, na kusema, “Haya ni maji yetu.”Hivyo Isaka akakiita kisima hicho “Eseki,” kwa sababu waligombana naye.
21 Wakachimba kisima kingine, wakakigombania hicho nacho, hivyo akakiita “Sitina.”
22 Akatoka hapo na akachimba kisima kingine, lakini hicho hawakukigombania. Hivyo akakiita Rehobothi, na akasema, “Sasa Yahwe ametufanyia nafasi, na tutafanikiwa katika nchi.”
23 Kisha Isaka akaenda Beersheba.
24 Yahwe akamtokea usiku huohuo na akasema, “Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi nipo pamoja nawe na nitakubariki na kuvidisha vizazi vyako, kwa ajili ya mtumishi wangu Ibrahimu.”
25 Isaka akajenga madhabahu pale na akaliita jina la Yahwe. Akapiga hema yake pale, na watumishi wake wakachimba kisima.
26 Kisha Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi, rafiki yake, na Fikoli, jemedari wa jeshi.
27 Isaka akawambia, “Kwa nini mmekuja kwangu, kwani mlinichukia na kunifukuza kwenu.
28 Nao wakasema, “Tumeona yakini kwamba Yahwe amekuwa nawe. Hivyo tukaamua kwamba kuwe na kiapo kati yetu, ndiyo, kati yetu nawe. Hivyo na tufanye agano nawe,
29 kwamba hautatudhuru, kama ambavyo sisi hatukukudhuru, na kama sisi tulivyokutendea vema wewe na tumekuacha uondoke kwa amani. Kwa kweli, Yahwe amekubariki.”
30 Hivyo Isaka akawaandalia sherehe, na wakala na kunywa.
31 Wakaamuka mapema asubuhi na wakaapiana kiapo. Kisha Isaka akawaruhusu kuondoka, nao wakamwacha katika amani.
32 Siku hiyohiyo watumishi wake wakaja na kumwambia juu ya kisima walichokuwa wamekichimba. Wakasema, “Tumeona maji.”
33 Akakiita kile kisima Shiba, hivyo jina la mji ule ni Beersheba hata leo.
34 Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akajitwalia mke, Yudithi binti Beeri Mhiti, na Basemathi binti Eloni Mhiti.
35 Wakamhuzunisha Isaka na Rebeka.