30
1 Raheli alipoona kwamba hamzalii Yakobo watoto, Raheli akamwonea wivu dada yake. Akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, sivyo nitakufa.”
2 Hasira ya Yakobo ikawaka juu ya Raheli. Akasema, “Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia usipate watoto?
3 Akasema, “Tazama, kuna mjakazi wangu Bilha. Lala naye, hivyo aweze kuzaa watoto magotini pangu, nami nitapata watoto kwake.
4 Hivyo akampa Bilha mjakazi kama mke wake, na Yakobo akalala naye.
5 Bilha akashika mimba na kumzalia Yakobo mwana.
6 Kisha Raheli akasema, “Mungu ameamua kwa faida yangu. Ameyasikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa sababu hiyo akamwita jina lake Dani
7 Bilha, mjakazi wa Raheli, akashika mimba tena na kumzalia Yakobo mwana wa pili.
8 Raheli akasema, “Kwa mashindano yenye nguvu nimeshindana na dada yangu na kushinda.” Akamwita jina lake Naftali.
9 Lea alipoona kwamba ameacha kuzaa, akamchukua Zilpa, mjakazi wake, na kumpa Yakobo kama mke wake.
10 Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana.
11 Lea akasema, “Hii ni bahati njema!” Hivyo akamwita jina lake Gadi.
12 Kisha Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili.
13 Lea akasema, “Nina furaha! Kwa maana mabinti wataniita furaha.” Hivyo akamwita jina lake Asheri.
14 Siku za mavuno ya ngano Rubeni akaenda shambani na kuona tunguja. Akazileta kwa mama yake. Kisha Raheli akamwambia Lea, “Nipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
15 Lea akamwambia, “Je ni jambo dogo kwako, kumchukua mme wangu? Je na sasa unataka kuchukua tunguja za mwanangu pia? Raheli akasema, “Kisha atalala nawe leo usiku, kwa kubadilishana na tunguja za mwanao.
16 Jioni Yakobo akaja kutoka uwandani. Lea akaenda kumlaki na kusema, “Leo usiku utalala nami, kwani nimekuajiri kwa tunguja za mwanangu.” Hivyo Yakobo akalala na Lea usiku huo.
17 Mungu akamsikia Lea, na akashika mimba na kumzalia Yakobo mwana wa tano.
18 Lea akasema, “Mungu amenipa ujira wangu, kwa sababu nilimpa mme wangu mjakazi wangu.” Akamwita jina lake Isakari.
19 Lea akashika mimba tena na kuzaa mwana wa tano kwa Yakobo.
20 Lea akasema, “Mungu amenipa zawadi njema. Sasa mme wangu ataniheshimu, kwa sababu nimemzalia wana sita.” Akamwita jina lake Zabuloni.
21 Baadaye akazaa binti na kumwita jina lake Dina.
22 Mungu akamkumbuka Raheli na kumsikiliza. Akampa kushika mimba.
23 Akashika mimba na kuzaa mwana. Akasema, “Mungu ameiondoa aibu yangu.”
24 Akamwita jina lake Yusufu, akisema, Yahwe ameniongeza mwana mwingine.”
25 Baada ya Raheli kumzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, “Niache niande, ili kwamba niende nyumbani kwetu na katika nchi yangu.
26 Nipe wake zangu na watoto wangu niliokutumikia kwa ajili yao, na uniache niondoke, kwani unafahamu nilivyokutumikia.
27 Labani akamwambia, “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, subiri, kwa sababu nimejifunza kwa kutumia uaguzi kwamba Yahwe amenibariki kwa ajili yako.”
28 Kisha akasema, “Taja ujira wako, nami nitalipa.”
29 Yakobo akamwambia, “Unajua nilivyokutumikia, na jinsi ambavyo mifugo wako wamekuwa nami.
30 Kwani walikuwa wachache kabla sijaja, na wameongezeka kwa wingi. Popote nilipokutumikia Mungu amekubariki. Je ni lini mimi nitaandaa kwa ajili ya nyumba yangu pia?”
31 Hivyo Labani akasema, “Je nikulipe nini? Yakobo akasema, 'Usinipe chochote. Ikiwa utafanya jambo hili kwa ajili yangu, nitawalisha tena kondoo wako na kuwatunza.
32 Niache nipite kati ya kundi lako lote leo, kwa kuondoa kila kondoo mwenye milia na mabaka, na kila kondoo mweusi kati yao, na kati ya wenye mabaka na milia katika mbuzi. Hawa watakuwa ujira wangu.
33 Uadilifu wangu utashuhudia kwa ajili yangu hapo baadaye, utakapokuja kuangalia ujira wangu. Kila ambaye hana milia na hana madoa miongoni mwa mbuzi, na mweusi kati ya kondoo, ikiwa wataonekana kwangu, watahesabiwa kuwa wameibwa.”
34 Labani akasema, “Nakubali. Na iwe kama yalivyo maneno yako.”
35 Siku hiyo Labani akaondoa mabeberu yaliyokuwa na milia na madoa, na majike ya mbuzi yaliyokuwa na milia na madoa, kila aliyekuwa mweupe, na weusi wote katika mbuzi, akawakabidhi katika mikono ya wanaye.
36 Pia Labani akaweka safari ya siku tatu kati yake na Yakobo. Hivyo Yakobo akabaki kuchunga wale kondoo wa Labani waliosalia.
37 Yakobo akachukua matawi mabichi yaliyokatwa ya mipopla, mlozi na mwaramoni mbichi akatoa maganda ili michilizi myeupe ionekane, na akaifanya sehemu nyeupe ya ndani ya mti iliyokuwa ndani ya fito ionekane.
38 Kisha akaziweka fito alizokuwa amezibambua mbele ya makundi ya kondoo, mbele ya mabirika yakunyweshea walipokuja kunywa maji. Wakashika mimba walipokuja kunywa maji.
39 Wanyama wakapandana mbele ya fito; nao wakazaa watoto wenye milia, mabaka na wenye madoa.
40 Yakobo akawatenga hawa wanakondoo, lakini akawafanya waliosalia kuelekea wanyama wenye milia na kondoo weusi wote katika kundi la Labani. Kisha akayatenga makundi yake mwenyewe pekee na hakuwaweka pamoja na wale wa Labani.
41 Pindi kondoo wenye nguvu katika kundi walipopandana, Yakobo alilaza fito katika mabirika ya maji mbele ya macho ya kundi, ili kwamba washike mimba kati ya fito.
42 Lakini wakati waliodhaifu walipokuja, hakuweka fito mbele yao. Hivyo wanyama dhaifu wakawa wa Labani, na wenye nguvu wakawa wa Yakobo.
43 Mtu huyo akastawi sana. Akawa na kundi kubwa la kondoo, wajakazi na wajoli, ngamia na punda.