39
1 Yusufu akaletwa Misri. Potifa, aliyekuwa afisa wa Farao mkuu wa walinzi na Mmisri, akamnunua kutoka kwa Waishmaeli, waliokuwa wamempeleka pale.
2 Yahwe alikuwa pamoja na Yusufu na akawa mtu aliyefanikiwa. Aliishi katika nyumba ya Mmisri bwana wake.
3 Bwana wake akaona kwamba Yahwe alikuwa pamoja naye na kwamba Yahwe alifanikisha kila kitu alichokifanya.
4 Yusufu akapata kibali mbele zake. Akamtumikia Potifa. Potifa akamfanya msimamizi juu ya nyumba yake, na kila alichokimiliki, akakiweka chini ya uangalizi wake.
5 Ikawa alipomfanya msimamizi juu ya nyumba yake na juu ya kila kitu alichomiliki, Yahwe akaibariki nyumba ya Mmisri kwa sababu ya Yusufu. Baraka za Yahwe zilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa nyumbani na shambani.
6 Potifa akaweka kila alichokuwa nacho chini ya uangalizi wa Yusufu. Hakuwa na haja ya kufikiri juu ya lolote isipokuwa chakula alichokula tu. Basi Yusufu alikuwa kijana mzuri na wa kuvutia.
7 Ikawa baada ya hayo mke wa bwana wake akamtamani Yusufu. Akamwambia, “Lala nami.”
8 Lakini yeye alikataa na kumwambia mke wa bwana wake, “Tazama, bwana wangu haangalii chochote nikifanyacho nyumbani, na ameweka kila kitu anachokimiliki chini ya uangalizi wangu.
9 Hakuna mtu aliye mkuu katika nyumba hii kuliko mimi. Hajanidhuiria chochote isipokuwa wewe, kwa sababu wewe ni mkewe. Ni kwa namna gani basi naweza kufanya uovu mkuu namna hii na kumtenda dhambi Mungu?
10 Akamwambia Yusufu siku baada ya siku, lakini yeye akakataa kulala naye wala kuwa naye.
11 Ikawa siku moja aliingia ndani kufanya kazi yake. Hakuna mtu yeyote wa nyumbani aliyekuwepo pale ndani.
12 Akashika nguo zake na kusema, “Lala nami.” Akaacha nguo zake mikononi mwake, akakimbia, na kutoka nje.
13 Ikawa, alipoona kwamba ameziacha nguo zake mikononi mwake na kwamba amekimbia nje,
14 akawaita watu wa nyumbani mwake na kuwambia, “Tazama, Potifa ameleta Mwebrania huyu kutudhihaki. Aliingia kulala nami, na nikapiga kelele.
15 Ikawa aliponisikia nikipiga kelele, akaniacha na nguo yake, akakimbia, na kutoka nje.”
16 Akaweka nguo zake karibu naye hata bwana yake alipokuja nyumbani.
17 Akamwambia maelelezo haya, “Yule mtumishi Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia kunidhihaki.
18 Ikawa nilipopiga kelele, akaacha nguo yake kwangu akakimbia nje.”
19 Ikawa, bwana wake aliposikia maelezo aliyoambiwa na mkewe, “Hivi ndivyo mtumishi wako alivyonitenda,” alikasirika sana.
20 Bwana wa Yusufu akamchukua na kumweka gerezani, mahali walipowekwa wafungwa wa mfalme. Akawa pale kifungoni.
21 Lakini Yahwe alikuwa pamoja na Yusufu na kumwonyesha uaminifu wa agano. Akampa kibali mbele ya mlinzi wa gereza.
22 Mlinzi wa gereza akawaweka mikononi mwa Yusufu wafungwa wote waliokuwa gerezani. Chochote walichokifanya, kilikuwa chini ya uangalizi wa Yusufu.
23 Mlinzi wa gereza hakuwa na wasiwasi juu ya chochote kilichokuwa mkononi mwake, kwa sababu Yahwe alikuwa pamoja naye. Yahwe akafanikisha kila alichokifanya.