43
1 Njaa ilikuwa kali katika nchi.
2 Ikawa walipokuwa wametumia chakula chote walichokitoa Misri, baba yao akawambia, “Nendeni tena; mtununulie chakula.”
3 Yuda akamwambia, “Yule mtu alituonya kwa ukali, 'Hamtauona uso wangu ndugu yenu asipokuwa nanyi.'
4 Ikiwa utamtuma ndugu yetu pamoja nasi, tutashuka na kuwanunulia chakula.
5 Lakini usipompeleka, hatutashuka. Kwa maana yule mtu alitwambia, 'Hamtauona uso wangu ndugu yenu asipokuwa nanyi.”
6 Israeli akawambia, “Kwa nini mlinitendea mimi vibaya hivyo kwa kumwambia mtu huyo kwamba mnaye ndugu mwingine?”
7 Wakasema, “Yule mtu alituuliza habari zetu na familia yetu kwa kina. Akasema, 'Je baba yenu bado yuko hai? Je mnaye ndugu mwingine?'Tukamjibu kulingana na maswali haya. Tungejuaje kwamba angetwambia, 'Mleteni ndugu yenu?”
8 Yuda akamwambia Israeli baba yake, “Mtume kijana pamoja nami. Tutainuka na kwenda ili kwamba tuishi tusife, wote sisi, wewe, na hata watoto wetu.
9 Mimi nitakuwa mdhamini wake. Utaniwajibisha mimi. Kama nisipomleta na kumweka mbele yako, basi nibebe lawama daima.
10 Kwani kama tusingekawia, bila shaka hata sasa tungekuwa tumekwisha rudi mara ya pili.”
11 Israeli baba yao akawambia, “Kama ni hivyo, basi fanyeni hivi. Chukueni baadhi ya mazao mazuri ya nchi katika mifuko yenu. Mchukulieni yule mtu zawadi: baadhi ya malhamu, asali, viungo na manemane, jozi na lozi.
12 Chukueni pesa mara mbili mikononi mwenu. Pesa iliyorudishwa katika magunia yenu, muichukue tena katika mikono yenu. Pengine walikosea.
13 Mchukueni ndugu yenu pia. Inukeni na mwende tena kwa mtu yule.
14 Mungu Mwenyezi na awape kuona rehema mbele ya huyo mtu, hivyo kwamba awafungulie ndugu yenu mwingine na Benjamini. Kama nikipotelewa na watoto, nimepotelewa.”
15 Watu wale wakachukua zawadi hii, na katika mikono yao wakachukua mara mbili ya kiasi cha pesa, pamoja na Benjamini. Wakaamka na kushuka Misri na kusimama mbele ya Yusufu.
16 Yusufu alipomwona Benjamini akiwa nao, akamwambia mtunzaji wa nyumba yake, “Walete watu hao ndani ya nyumba, chinja mnyama na umwandae, kwani watu hawa watakula chakula cha mchana pamoja nami.”
17 Mtunzaji wa nyumba akafanya kama Yusufu alivyosema. Akawaleta wale watu nyumbani kwa Yusufu.
18 Wale ndugu wakaogopa kwa vile walivyoletwa katika nyumba ya Yusufu. Wakasema, “Ni kwa sababu ya pesa iliyorudishwa katika magunia yetu mara ya kwanza tulipoletwa ndani, kwamba atafute nafasi kinyume chetu. Kwamba aweze kutukamata na kutuchukua kama watumwa, na kuchukua punda wetu.” Wakamsogelea mtunzaji wa nyumba ya Yusufu,
19 nao wakaongea naye mlangoni mwa nyumba,
20 wakisema, “Bwana wangu, tulikuja mara ya kwanza kununua chakula.
21 Ikawa, tulipofika katika eneo la kupumzikia, tukafungua magunia yetu, na, tazama, pesa ya kila mtu ilikuwa katika gunia lake, pesa yetu kwa kiasi kamili. Tumeileta katika mikono yetu.
22 Tumekuja na pesa nyingine pia mikonon mwetu ili kununua chakula. Hatujui aliyeziweka pesa katika magunia yetu.”
23 Mtunzaji wa nyumba akasema, “Amani iwe kwenu, msiogope. Mungu wenu na Mungu wa baba yenu ndiye aliyeweka pesa katika magunia yenu. Nilipokea pesa yenu.” Kisha mtunzaji wa nyumba akamleta Simoni kwao.
24 Msimamizi wa nyumba akawapeleka watu hao katika nyumba ya Yusufu. Akawapa maji, nao wakaosha miguu yao. Akawalisha punda wao.
25 Wakaandaa zawadi kwa ajili ya Yusufu aliyekuwa akija mchana, kwani walikuwa wamesikia kwamba watakula pale.
26 Yusufu alipokuja nyumbani, wakaleta nyumbani zawadi iliyokuwa mikononi mwao, nao wakainama mbele yake hata chini.
27 Akawauliza juu ya hali zao na kusema,”Je baba yenu hajambo, yule mzee mliyemnena? Je bado yu hai?”
28 Wakasema, “Mtumishi wako baba yetu hajambo. Na bado yu hai” Wakajinyenyekeza na kuinama chini.
29 Alipoinua macho yake akamwona Benjamini ndugu yake, mwana wa mamaye, naye akasema, “Je huyu ndiye mdogo wenu mliyemsema?” Na kisha akasema, “Mungu na awe mwenye neema kwako, mwanangu.”
30 Yusufu akaharakisha kutoka chumbani, kwani aliguswa sana kuhusu nduguye. Akatafuta mahali pa kulia. Akaingia chumbani mwake na kulia umo.
31 Akaosha uso wake na kutoka nje. Akajizuia mwenyewe, akasema, “karibuni chakula.”
32 Watumishi wakamhudumia Yusufu peke yake na wale ndugu peke yao. Wamisri pale wakala pamoja naye peke yao kwa sababu Wamisri hawakuweza kula mkate na Waebrania, kwani hilo ni chukizo kwa Wamisri.
33 Wale ndugu wakakaa mbele yake, mzaliwa wa kwanza kwa kulingana na haki yake ya uzaliwa, na mdogo kulingana na ujana wake. Wale watu wakashangaa wote.
34 Yusufu akapeleka sehemu kwao kutoka katika chakula kilichokuwa mbele yake. Lakini sehemu ya Benjamini ilikuwa mara tano zaidi ya kila ndugu zake. Wakanywa na wakamfurahia.