45
1 Ndipo Yusufu hakuweza kujizuia mwenyewe mbele ya watumishi waliosimama kando yake. Akasema kwa sauti, “Kila mtu aondoke.” Hivyo hakuna mtumishi aliyesimama kando yake wakati Yusufu alipojitambulisha kwa ndugu zake.
2 Akalia kwa sauti, Wamisri wakasikia, na nyumba ya Farao wakasikia kuhusu hilo.
3 Yusufu akawambia ndugu zake, “Mimi ni Yusufu. Je baba yangu ni mzima bado? Ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwani walitishwa na uwepo wake.
4 Kisha Yusufu akawambia ndugu zake, “Nikaribieni, tafadhari.” Nao wakasogea. Akawambia, “Mimi ni Yusufu ndugu yenu, mliyemwuza Misri.
5 Lakini sasa msihuzunike au kukasirika miongoni mwenu kwamba mliniuza huku, kwani Mungu alinituma mbele yenu ili kutunza uhai.
6 Maana ni miaka miwili njaa imekuwa katika nchi, na bado kuna miaka mitano ambayo hakutakuwa na kulima wala kuvuna.
7 Mungu alinituma mbele yenu kuwahifadhi kama masalia duniani, na kuwaweka hai kwa ukombozi mkuu.
8 Hivyo si ninyi mlionipeleka huku bali ni Mungu, na amenifanya baba kwa Farao, bwana wa nyumba yake yote, na mtawala wa nchi yote ya Misri.
9 Fanyeni haraka mwende kwa baba yangu na mmwambie, 'Hivi ndivyo asemavyo Yusufu mwanao, “Mungu amenifanya bwana kwa Wamisri wote. Shuka kwangu, usikawie.
10 Utaishi katika nchi ya Gosheni, nawe utakuwa karibu nami, wewe na watoto wako na watoto wa watoto wako, na kondoo wako na mbuzi wako, na yote uliyonayo.
11 Nami nitakuhudumia pale, kwa maana bado kuna miaka mitano ya njaa, hivyo usije ukaingia katika uhitaji, wewe, nyumba yako, na yote uliyonayo.”
12 Tazama, macho yenu yanaona, na macho ya Benjamini ndugu yangu, kwamba ni kinywa changu kinachoongea nanyi.
13 Mtamwambia baba yangu juu ya heshima yangu yote huku Misri na yote mliyoyaona. Mtaharakisha na kumleta baba yangu huku.”
14 Akaikumbatia shingo ya Benjamini ndugu yake na kulia, na Benjamini akalia shongoni mwake.
15 Akawabusu ndugu zake wote na kulia kwa ajili yao. Baada ya hayo ndugu zake wakaongea naye.
16 Habari ya jambo hili ikasemwa katika nyumba ya Farao: “Ndugu zake Yusufu wamekuja.” Ikampendeza sana Farao na watumishi wake.
17 Farao akamwambia Yusufu, “Wambie ndugu zako, 'Fanyeni hivi: Wapakieni wanyama wenu na mwende katika nchi ya Kanaani.
18 Mchukueni baba yenu na nyumba zenu mnijie. Nami nitawapa mema ya nchi ya Misri, nanyi mtakula unono wa nchi.'
19 Basi mmeamriwa, 'Fanyeni hivi, chukueni mikokoteni kutoka Misri kwa ajili ya watoto wenu na kwa ajili ya wake zenu. Mchukueni baba yenu na kuja.
20 Msijari kuhusu mali zenu, kwani mema yote ya nchi ya Misri ni yenu.”
21 Wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yusufu akawapa mikokoteni, kwa kadili ya agizo la Farao, na akawapa mahitaji ya safari.
22 Akawapa wote mavazi ya kubadilisha, lakini akampa Benjamini vipande mia tatu vya fedha na mavazi matano ya kubadilisha.
23 Akampelekea baba yake: punda kumi waliobeba mema ya Misri, punda majike kumi wamebeba nafaka, mikate, na mahitaji mengine kwa baba yake kwa ajili ya safari.
24 Hivyo akawaruhusu ndugu zake nao wakaondoka. Akawambia, “Angalieni msijemkagombana njiani.”
25 Wakapanda kutoka Misri na kuja katika nchi ya Kanaani, kwa Yakobo baba yao.
26 Wakamwambia “Yusufu bado yu hai, na ndiye mtawala juu ya nchi yote ya Misri.” Na moyo wake ulishikwa na ushangao, kwani hakuwaamini.
27 Wakamwambia maneno yote ya Yusufu aliyokuwa amewambia. Yakobo alipoona mikokoteni Yusufu aliyokuwa amepeleka kuwabeba, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka.
28 Israeli akasema, “Inatosha. Yusufu mwanangu yu hai. Nitakwenda nikamwone kabla sijafa.”