47
1 Kisha Yusufu akaingia kwa Farao na kumwambia, “Baba yangu na ndugu zangu, kondoo wao, mbuzi wao, na yote waliyonayo, wamefika kutoka katika nchi ya Kanaani. Tazama, wapo katika nchi ya Gosheni.”
2 Akawachukua watano katika ndugu zake na kuwatambulisha kwa Farao.
3 Farao akawambia ndugu zake, “Kazi yenu ni nini?” Wakamwambia Farao, “Watumishi wako ni wafugaji, kama mababu zetu.”
4 Kisha wakamwambia Farao, “Tumekuja kukaa kwa muda katika nchi. Hakuna malisho kwa ajili ya makundi ya watumishi wako, kwa maana njaa ni kali sana katika nchi ya Kanaani. Hivyo, tafadhari waache watumishi wako wakae katika nchi ya Gosheni.”
5 Kisha Farao akamwambia Yusufu, kusema, “Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako.
6 Nchi ya Misri iko mbele yako. Mkalishe baba yako na ndugu zako katika eneo zuri, nchi ya Gosheni. Ikiwa unafahamu watu wenye uwezo miongoni mwao, uwaweke kuwatunza wanyama wangu.”
7 Kisha Yusufu akamwingiza Yakobo baba yake na kumweka mbele ya Farao. Yakobo akambariki Farao.
8 Farao akamwambia Yakobo, “Umeishi kwa muda gani?”
9 Yakobo akamwambia Farao, “Miaka ya safari zangu ni mia moja na thelathini. Miaka ya maisha yangu imekuwa mifupi na ya maumivu. Siyo kama miaka ya baba zangu.”
10 Kisha Yakobo akambariki Farao na kuondoka mbele zake.
11 Kisha Yusufu akamweka baba yake na ndugu zake. Akawapa eneo katika nchi ya Misri, sehemu nzuri sana ya nchi, katika eneo la Ramesesi, kama Farao alivyokuwa ameagiza.
12 Yusufu akamhudumia baba yake kwa chakula, ndugu zake, na nyumba yote ya baba yake, kulingana na hesabu ya wahitaji wao.
13 Basi hakukuwa na chakula katika nchi yote; kwani njaa ilikuwa kali sana. Nchi ya Misri na nchi ya Kanaani ikaharibika kwa sababu ya njaa.
14 Yusufu akakusanya pesa yote iliyokuwa katika nchi ya Misri na nchi ya Kanaani, kwa kuwauzia wakaaji wake chakula. Kisha Yusufu akaleta ile pesa katika kasri la Farao.
15 Pesa yote ya nchi za Misri na Kanaani ilipokwisha, Wamisri wote wakaja kwa Yusufu wakisema, “Tupe chakula! Kwa nini tufe mbele zako kwa maana pesa yetu imekwisha?”
16 Yusufu akasema, “Ikiwa pesa yenu imekwisha, leteni wanyama wenu nami nitawapa chakula badala ya wanyama wenu.”
17 Hivyo wakaleta wanyama wao kwa Yusufu. Yusufu akawapa chakula kwa kubadilishana na farasi, kondoo, mbuzi na kwa punda. Akawalisha kwa mkate kwa kubadilisha na wanyama wao mwaka ule.
18 Mwaka ule ulipokwisha, wakaja kwake mwaka uliofuata na kumwambia, “Hatutaficha kwa bwana wangu kwamba pesa yetu yote imekwisha, na wanyama ni wa bwana wangu. Hakuna kilichobaki mbele za bwana wangu, isipokuwa miili yetu na nchi yetu.
19 Kwa nini tufe mbele za macho yake, sisi na nchi yetu? Utununue sisi na nchi yetu badala ya chakula, na sisi na nchi yetu tutakuwa watumishi wa Farao. Tupe mbegu ili kwamba tuishi na tusife, na kwamba nchi isiwe tupu bila watu.
20 Hivyo Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri. Kwani kila Mmisri akauza shamba lake, kwa sababu njaa ilikuwa kali sana. Kwa njia hii, nchi ikawa mali ya Farao.
21 Na watu, akawafanya kuwa watumwa kutoka mpaka mmoja wa Misri hata mkapa mwingine.
22 Ilikuwa ni nchi ya makuhani pekee ambayo Yusufu hakuinunua, kwa maana makuhani walikuwa wakipewa posho. Walikula katika sehemu aliyowapa Farao. Kwa hiyo hawakuuza nchi yao.
23 Kisha Yusufu akawambia watu, “Tazama, nimewanunua ninyi na nchi yenu leo kwa ajili ya Farao. Basi mbegu hii hapa kwa ajili yenu, nanyi mtapanda katika nchi.
24 Wakati wa mavuno, mtampa Farao sehemu ya tano, na sehemu nne zitakuwa zenu, kwa mbegu za shamba na kwa chakula cha nyumba zenu na watoto wenu.”
25 Wakasema, “Umeokoa maisha yetu. Na tupate kibali machoni pako. Tutakuwa watumishi wa Farao.”
26 Hivyo Yusufu akaifanya kuwa sheria inayofanya kazi hata leo katika nchi ya Misri, kwamba moja ya tano ni ya Farao. Eneo la makuhani peke yake ndo halikufanywa kuwa la Farao.
27 Hivyo Israeli akaishi katika nchi ya Misri, katika eneo la Gosheni. Watu wake wakapata umiliki pale. Walikuwa wenye kuzaa na kuongezeka sana.
28 Yakobo akaishi katika nchi ya Misri miaka kumi na saba, kwa hiyo miaka ya maisha ya Yakobo ilikuwa miaka mia moja arobaini na saba.
29 Wakati wa kufa kwake Yakobo ulipokaribia, alimwita Yusufu mwanaye na kumwambia, “Ikiwa nimepata kibali mbele zako, weka mkono wako chini ya paja langu, na unitendee kwa uaminifu na kweli. Tafadhari usinizike Misri.
30 Nitakapolala na baba zangu, utanitoa Misri na kunizika katika eneo la kuzikia la baba zangu.” Yusufu akasema, “Nitafanya kama ulivyosema.”
31 Israeli akasema, “Niapie,” na Yusufu akamwapia. Kisha Israeli akainama chini mbele ya kitanda chake.