7
1 Yahwe akamwambia Nuhu, “Njoo, wewe na nyumba yako wote, katika safina, kwa kuwa nimeona kuwa wewe ni mwenye haki mbele yangu katika kizazi hiki.
2 Kwa kila mnyama aliye safi utakuja nao saba wa kiume na saba wa kike. Na kwa wanyama wasio safi, lete wawili wawili, wakiume na wakike.
3 Pia na kwa ndege wa angani, lete saba wa kiume na saba wa kike, ili kuhifadhi kizazi chao juu ya uso wa nchi yote.
4 Kwa kuwa ndani ya siku saba nitasababisha mvua kunyesha juu ya nchi muda wa siku arobaini mchana na usiku. Nitaharibu kila kiumbe hai nilichokiumba juu ya uso wa ardhi.”
5 Nuhu alifanya yote ambayo Yahwe alimuagiza.
6 Nuhu alikuwa na umri wa miaka mia sita wakati gharika ilipokuja juu ya nchi.
7 Nuhu, watoto wake wa kiume, mke wake, na wake za watoto wake waliingia katika safina pamoja kwa sababu ya maji ya gharika.
8 Wanyama ambao ni safi na wanyama ambao si safi, ndege, na kila kitambaacho juu ya ardhi,
9 wawili wawili mume na mke wakaja kwa Nuhu na wakaingia katika safina, kama vile Mungu alivyokuwa amemwagiza Nuhu.
10 Ikawa kwamba baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya nchi.
11 Katika mwaka wa mia sita wa maisha yake Nuhu, katika mwezi wa pili, katika siku ya kumi na saba ya mwezi, katika siku iyo hiyo, chemchemi zote za vilindi vikuu zilipasuka na kufunguka, na madirisha ya mbinguni yakafunguka.
12 Mvua ikaanza kunyesha juu ya nchi kwa siku arobaini mchana na usiku.
13 Katika siku iyo hiyo Nuhu pamoja na watoto wake, Shem, Ham, na Yafethi na mke wa Nuhu, na wale wake watatu wa wana wa Nuhu pamoja waliingia katika safina.
14 Waliingia pamoja na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho juu ya ardhi kwa jinsi yake, na kila aina ya ndege kwa jinsi yake, kila aina ya kiumbe chenye mabawa.
15 Viwili viwili katika kila chenye mwili ambacho kilikuwa na pumzi ya uhai kilikuja kwa Nuhu na kuingia katika safina.
16 Wanyama walioingia ndani walikuwa wakiume na kike katika wote wenye mwili; wakaingia kama vile Mungu alivyokuwa amemwagiza. Kisha Yahwe akawafungia mlango.
17 Kisha gharika ikaja juu ya nchi kwa siku arobaini, na maji yakaongezeka na kuinua safina juu ya nchi.
18 Maji yakafunika kabisa nchi, na safina ikaelea juu ya uso wa maji.
19 Maji yakaongezeka zaidi juu ya nchi kiasi kwamba milima yote mirefu ambayo ilikuwa chini ya anga ikafunikwa.
20 Maji yakaongezeka dhiraa kumi na tano juu ya vilele vya milima.
21 Vitu vyote vyenye uhai ambavyo vilitembea juu ya nchi vilikufa: ndege, mifugo, wanyama wa mwituni, viumbe hai vyote kwa wingi vilivyoishi juu ya nchi, pamoja na watu.
22 Viumbe hai vyote ambavyo vilikaa juu ya ardhi, vilivyo pumua pumzi ya uhai kwa njia ya pua, vilikufa.
23 Hivyo kila kilichokuwa hai ambacho kilikuwa juu ya uso wa mchi kilifutwa, kuanzia watu mpaka wanyama wakubwa, mpaka vitambaavyo, na mpaka ndege wa angani. Vyote viliangamizwa kutoka kwenye nchi. Nuhu tu pamoja na wale waliokuwa naye kwenye safina ndio walisalia.
24 Maji haya kuzama chini ya nchi kwa muda wa siku miamoja na hamsini.