4
1 Hatimaye, ndugu, twawatia moyo na kuwasihi kwa Yesu Kristo. Kama mlivyopokea maelekezo toka kwetu namna iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kwa njia hiyo pia muenende na kutenda zaidi.
2 Kwa kuwa mwajua ni maelekezo gani tuliyowapa kupitia Bwana Yesu.
3 Kwa kuwa haya ndiyo mapenzi ya Mungu: utakaso wenu - kwamba muepuke zinaa,
4 Kwamba kila mmoja wenu anajua namna ya kumiliki mke wake mwenyewe katika utakatifu na heshima.
5 Usiwe na mke kwa ajili ya tamaa za mwili (kama Mataifa wasiomjua Mungu).
6 Asiwepo mtu yeyote atakaye vuka mipaka na kumkosea nduguye kwa ajili ya jambo hili. Kwa kuwa Bwana ndiye mwenye kulipa kisasi kwa mambo yote haya, kama tulivyo tangulia kuwaonya na kushuhudia.
7 Kwa kuwa Bwana hakutuita kwa uchafu, bali kwa utakatifu.
8 Kwa hiyo anayelikataa hili hawakatai watu, bali anamkataa Mungu, anayewapa Roho Mtakatifu wake.
9 Kuhusu upendo wa ndugu, hakuna haja ya mtu yeyote kukuandikia, kwa kuwa mmefundishwa na Mungu kupendana ninyi kwa ninyi.
10 Hakika, mlifanya haya yote kwa ndugu walioko Makedonia yote, lakini twawasihi, ndugu, mfanye hata na zaidi.
11 Twawasihi mtamani kuishi maisha ya utulivu, kujali shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu, kama tulivyowaamuru.
12 Fanya haya ili uweze kuenenda vizuri na kwa heshima kwa hao walio nje ya imani, ili usipungukiwe na hitaji lolote.
13 Hatutaki ninyi muelewe isivyo sahihi, enyi ndugu, juu ya hao waliolala, ili msije mkahuzunika kama wengine wasio na uhakika kuhusu wakati ujao.
14 Iwapo tunaamini kuwa Yesu alikufa na akafufuka tena, vivyo hivyo Mungu atawaleta pamoja na Yesu hao waliolala mauti katika yeye.
15 Kwa ajili ya hayo twawaambia ninyi kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaokuwepo wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wale waliolala mauti.
16 Kwa kuwa Bwana mwenyewe atashuka toka mawinguni. Atakuja na sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, pamoja na parapanda ya Mungu, nao waliokufa katika Kristo watafufuka kwanza.
17 Kisha sisi tulio hai, tuliobaki, tutaungana katika mawingu pamoja nao kumlaki Bwana hewani. Kwa njia hii tutakuwa na Bwana siku zote.
18 Kwa hiyo, mfarijiane ninyi kwa ninyi kwa maneno haya.