8
1 Sasa jambo ambalo tunasema ni hili: tunaye kuhani mkuu aliyekaa chini katika mkono wa kulia wa kiti cha enzi Mbinguni.
2 Yeye ni mtumishi katika mahali patakatifu, hema la kweli ambalo Bwana ameliweka, siyo mtu yeyote wa kufa.
3 Kwa maana kila kuhani mkuu huwekwa kutoa zawadi na dhabihu; kwa hiyo ni muhimu kuwa na kitu cha kutoa.
4 Sasa kama Kristo alikuwa juu ya nchi, yeye asingekuwa kuhani zaidi ya hapo. Kwa kuwa walikuwa tayari wale waliotoa vipawa kulingana na sheria.
5 Walihudumu kitu ambacho kilikuwa nakala na kivuli cha vitu vya mbinguni, sawa kama Musa alipoonywa na Mungu wakati alipotaka kujenga hema. “Ona,” Mungu akasema, “kwamba tengeneza kila kitu kulingana na muundo ulioonyeshwa juu ya mlima”.
6 Lakini sasa Kristo amepokea huduma bora zaidi kwa sababu yeye pia ni mpatanishi wa agano zuri, ambalo limekwisha kuimarishwa kwa ahadi nzuri.
7 Hivyo kama agano la kwanza lisingekuwa na makosa, ndipo hakungekuwa na haja kutafuta agano la pili.
8 Kwa kuwa wakati Mungu alipogundua makosa kwa watu alisema, “Tazama, siku zinakuja, 'asema Bwana, 'wakati nitakapotengeneza agano jipya pamoja na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
9 Halitakuwa kama agano nililofanya pamoja na baba zao siku ambayo niliwachukua kwa mkono kuwaongoza kutoka nchi ya Misri. Kwa kuwa hawakuendelea katika agano langu, nami sikuwajali tena,' asema Bwana.
10 Kwa kuwa hili ndilo agano nitafanya kwa nyumba ya Israeli baada ya siku hizo,' asema Bwana. 'nitaweka sheria zangu mawazoni mwao, na nitaziandika mioyoni mwao. Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
11 Hawatafundishana kila mmoja na jirani yake, na kila mmoja na ndugu, yake, akisema, “Mjue Bwana,” hivyo wote watanijua mimi, kutoka mdogo hadi mkubwa wao.
12 Hivyo nitaonyesha rehema kwa matendo yao yasiyo ya haki, na sizitazikumbuka dhambi zao tena.”
13 Kwa kusema “Mpya,” amelifanya agano la kwanza kuwa kuukuu. Na hilo ambalo amelitangaza kuwa kuukuu liko tayari kutoweka.