5
Yeyote anayeamini kuwa Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu. Na yeyote ampendaye yeye ambaye ametoka kwa Baba pia huwapenda watoto wake. Kwa hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu — tunapompenda Mungu na kutekeleza amri zake. Hivi ndivyo tunavyompenda Mungu kwamba twazishika amri zake. Na amri zake ni nyepesi. Kwa kuwa kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Na huu ndio ushindi wa kuushinda ulimwengu, imani yetu. Ni nani aliyeushinda ulimwengu? Ni yule aaminiye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu- Yesu Kristo. Hakuja tu kwa maji bali kwa maji na damu. Kwa kuwa kuna watatu washuhudiao: Roho, maji na damu. Hawa watatu hukubaliana. (Zingatia: Maneno haya “Baba, Neno, na Roho Mtakatifu” hayaonekani katika nakala bora za kale). Kama tunaupokea ushuhuda wa wanadamu ushuhuda wa Mungu ni mkuu kuliko huo. Kwa kuwa ushuhuda wa Mungu ni huu- kwamba anao ushuhuda kuhusiana na Mwanawe. 10 Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu ana ushuhuda ndani yake mwenyewe. Na yeyote asiye mwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini ushuhuda ambao Mungu ameuleta kuhusu Mwanawe. 11 Na ushuhuda ndio huu — kwamba Mungu alitupa uzima wa milele, na uzima huu umo ndani ya Mwanawe. 12 Aliye naye Mwana ana uzima. Asiyekuwa naye Mwana wa Mungu hana uzima. 13 Nimewaandikia haya mweze kujua kwamba mnao uzima wa milele — ninyi mnaoamini katika jina la Mwana wa Mungu. 14 Na huu ndio ujasiri tulionao mbele zake, kwamba kama tukiomba kitu chochote sawa sawa na mapenzi yake, hutusikia. 15 Na kama tunajua kwamba hutusikia — chochote tumwombacho tunajua kwamba tunacho hicho tulichomwomba. 16 Kama mtu amwonaye ndugu yake anatenda dhambi isiyopelekea kifo, yampasa kuomba na Mungu atampa uzima. Ninasema kwa wale ambao dhambi yao ni ile isiyopelekea kifo — Kuna dhambi ipelekeayo kifo — sisemi kwamba anapaswa kuomba kwa ajilli ya dhambi hiyo. 17 Uasi wote ni dhambi — lakini kuna dhambi isiyopelekea kifo. 18 Tunajua ya kuwa aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi. Bali aliyezaliwa na Mungu hutunzwa naye salama daima, na yule mwovu hawezi kumdhuru. 19 Tunajua kuwa sisi ni wa Mungu na tunajua kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu. 20 Lakini twajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja na ametupatia ujuzi, kwamba tunamjua yeye aliye kweli na kwamba tumo ndani yake yeye aliye kweli, hata katika Mwanawe Yesu Kristo. Ni Mungu wa kweli na uzima wa milele. 21 Watoto wapenzi, jiepusheni na sanamu.