11
1 Ndipo Sofari Mnaamathi alijibu na kusema,
2 “ Huo wingi wa maneno haupaswi kujibiwa? Mtu huyu, aliyejaa maneno mengi awe wa kuaminiwa?
3 Kujivuna kwako kunapaswa kuwafanya wengine wabaki wamenyamaza? Wakati unapoyadhihaki mafundisho yetu, hakuna awaye yote atakayekufanya wewe ujisikie mwenye aibu?
4 Kwa kuwa wewe unasema kwa Mungu, 'Imani yangu ni safi, Mimi sina waa lolote machoni pako.'
5 Lakini, laiti, Mungu huyo angesema na kufungua midomo yake dhidi yako;
6 hivyo angekuonyesha wewe siri za hekima! Kwa kuwa yeye ni mkuu katika ufahamu. Tena tambua huyo Mungu anataka kutoka kwako kidogo kuliko uovu wako unavyostahili.
7 Je, wewe unaweza kumfahamu Mungu kwa kumtafuta yeye? Unaweza kumtambua aliye mkuu kwa ukamilifu?
8 Upeo uko juu kama mbingu; unaweza kufanya nini wewe? Ni wenye kina kirefu kuliko kuzimu; waweza kufahamu nini wewe?
9 Vipimo vyake ni virefu kuliko nchi, na vipana kuliko bahari.
10 kama yeye akipita kati na kumyamazisha mtu yeyote, kama yeye akimwita mtu yeyote hukumuni, tena ni nani anayeweza kumzuia yeye?
11 Kwa maana anawajua watu waongo; wakati anapoona uovu, hawezi yeye kuukumbuka?
12 Lakini watu wapumbavu hawana ufahamu; wataupata wakati punda mwitu atakapozaa mtu.
13 Lakini ikiwa umeuelekeza moyo wako kwa haki na umeunyosha mkono wako karibu na Mungu;
14 ikiwa huo uovu ulikuwa katika mikono yako, lakini hivyo tena unauweka mbali nawe, na haukuruhusu kutokuwa mwenye haki kukaa hemani mwako.
15 Ndipo kwa hakika ungeinua juu uso wako bila ishara ya aibu; Ni dhahiri, ungethibitika na usingeogopa.
16 Wewe ungesahau mateso yako; ungeyakumbuka hayo tu kama maji ambayo yametiririka mbali.
17 Maisha yako yangekuwa angavu kuliko adhuhuri; japokuwa kulikuwa na giza, litakuwa kama asubuhi.
18 Ungekuwa salama kwa sababu kuna tumaini; ni dhahiri, wewe utapata usalama juu yako na utachukua pumziko lako katika usalama.
19 Pia ungelala chini katika pumziko, na hakuna ambaye angekufanya wewe uogope; hakika wengi wangetafuta upendeleo wako.
20 Lakini macho ya watu waovu yatashindwa; hawatakuwa na njia ya kukimbia; tumaini lao la pekee litakuwa pumzi yao ya mwisho ya uhai.