2
1 Kisha kulikuwa na siku wana wa Mungu walipokwenda kujihudhurisha mbele za BWANA. Shetani pia alikwenda kati yao kujihudhulisha mbele za BWANA.
2 BWANA akamuuliza Shetani, “umetoka wapi wewe?” Kisha Shetani akamjibu BWANA na kusema, “Natoka kuzunguka zunguka duniani, kutembea huku na huko humo.”
3 BWANA akamuuliza Shetani, “Je umemwangalia mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mwenye haki na mkamilifu, mmoja aliye mcha Mungu na kuepukana na uovu. Hata sasa anashikamana na utimilifu wake, japokuwa ulinichochea juu yake, nimwangamize pasipo sababu.”
4 Shetani akamjibu BWANA na kusema, “Ngozi kwa ngozi, kweli; mtu atatoa vyote alivyo navyo kwaajili ya uhai wake.
5 Lakini nyosha mkono wako sasa na uguse mifupa yake na nyama yake, na uone kama hatakufuru mbele ya uso wako.”
6 BWANA akamwambia Shetani, “Tazama, yumo mkononi mwako; ni uhai wake tu ambao lazima uutunze.”
7 Kisha Shetani akatoka mbele ya uso wa BWANA. Akampiga Ayubu na majipu mabaya toka wayo wa mguu hadi kichwani.
8 Ayubu akachukua kipande cha kigae kujikunia, na akaketi chini majivuni.
9 Kisha mkewe akamuuliza, “Je hata sasa wewe unashikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu na ufe.
10 Lakini yeye akamwambia, “Wewe unaongea kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu waongeavyo. Je sisi tupate mema toka kwa Mungu na tusipate mabaya?” Katika mambo hayo yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa midomo yake.
11 Sasa wakati rafiki zake watatu wa Ayubu walipopata habari ya mabaya yaliyompata, kila mmoja wao akaja kutoka mahali pake: Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi. Wakatenga muda ili waende kuomboleza naye na kumfariji.
12 Walipoinua macho yao wakiwa mbali, hawakuweza kumtambua. Wakapaza sauti zao na kulia; kila mmoja wao akararua joho lake na kurusha majivu hewani na juu ya kichwa chake.
13 Kisha wakaketi chini pamoja naye kwa muda wa siku saba-mchana na usiku. Hakuna hata mmoja aliyesema naye neno, kwa kuwa waliona kuwa huzuni yake ilikuwa kuu mno.