8
1 Kisha Bildadi huyo Mshuhi akajibu na kusema,
2 “hata lini wewe utasema mambo haya? Kwa muda gani maneno ya kinywa chako yatakuwa kama upepo wenye nguvu?
3 Je Mungu hupotosha hukumu? Je Mwenyezi hupotosha haki?
4 Watoto wako wametenda dhambi dhidi yake; tunalifahamu hili, kwa kuwa amewatia mkononi kwa makosa yao.
5 Lakini wewe unaonaje ukimtafuta Mungu kwa bidii na kufikisha haja yako kwa huyo Mwenyezi.
6 Ukiwa wewe ni msafi na mkamilifu, hakika angeamka mwenyewe kwa niaba yako na kukurudisha kwenye makazi ya haki yako.
7 Japokuwa huo mwanzo wako ulikuwa ni mdogo, hata hivyo hali yako ya mwisho itaongezeka sana.
8 Tafadhari uwaulize vizazi vya zamani, na utie bidii katika hayo mababu zetu waliyojifunza.
9 (Sisi ni wa jana tu na hatujui chochote kwa kuwa siku zetu duniani ni kivuli).
10 Je hawatakufunza wao na kukuambia? Je hawatatamka maneno yatokayo mioyoni mwao?
11 Je hayo mafunjo yaota pasipo matope? Je mafunjo yaota pasipo maji?
12 Wakati yakiwa bado ya kijani na hayajakatwa, hunyauka kabla ya mmea mwingine.
13 Hivyo pia njia ya wote wamsahauo Mungu, na matumaini ya asiyeamini Mungu yatatoweka.
14 Ujasiri wake utavunjika, na matumaini yake ni dhaifu kama utando wa buibui.
15 Ataitegemea nyumba yake, lakini haitamsaidia; atashikamana nayo, lakini isidumu.
16 Yeye huwa mti mbichi chini ya jua, na machipukizi yake huenea katika bustani yake yote.
17 Mizizi yake hujifunga funga kwenye rundo la mawe; huangalia mahali pazuri katikati ya mawe;
18 Lakini mtu huyu aking'olewa mahali pake, kisha mahali pale patamkana, na kusema, 'mimi sikukuona.'
19 Tazama, hii ni “furaha” ya mtu mwenye tabia hiyo; mimea mingine itachipuka toka katika udongo ule ule mahali pake.
20 Tazama, Mungu hatamtupa mtu asiye na kosa; wala hatawathibitisha watendao uovu.
21 Yeye atakijaza kinywa chako na kicheko, midomo yako na shangwe.
22 Wale ambao wanakuchukia wewe watavishwa aibu; nayo hema yake mwovu haitakuwepo tena.