3
1 Ndugu zangu, siyo wengi wenu mnapaswa kuwa walimu, mkijua kwamba tutapokea hukumu kubwa zaidi.
2 Kwa kuwa wote tunakosea katika njia nyingi. Kama yeyote huwa hajikwai katika maneno yake, huyo ni mtu mkamilifu, aweza kudhibiti mwili wake wote pia.
3 Sasa kama tunaweka lijamu za farasi katika vinywa vyao wanatutii, na tunaweza kuigeuza miili yao yote.
4 Tambua pia kwamba meli, ingawa ni kubwa na husukumwa na upepo mkali, zinaongozwa kwa usukani mdogo sana kwenda popote anakotaka nahodha.
5 Vivyo hivyo, ulimi ni kiungo kidogo cha mwili, lakini hujisifia makuu sana. Angalia msitu mkubwa unavyoweza kuwashwa kwa cheche ndogo ya moto!
6 Ulimi pia ni moto, ni ulimwengu wa uovu, umewekwa miongoni mwa viungo vya mwili wetu, ambao hunajisi mwili wote na huiweka juu ya moto njia ya maisha, na wenyewe kuchomwa moto wa kuzimu.
7 Kila aina ya mnyama wa polini, ndege, kitambaacho na kiumbe cha baharini kinadhibitiwa na wanadamu.
8 lakini hakuna mwanadamu hata mmoja ambaye anaweza kudhibiti ulimi; ni uovu usiotulia, umejaa sumu ya kufisha.
9 Kwa ulimi twamtukuza Bwana na Baba yetu, na kwa huo twawalaani watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu.
10 Katika kinywa hichohicho husema maneno ya baraka na laana. Ndugu zangu mambo haya hayapaswi kuwa.
11 Je, kisima kimoja huweza kutoa maji matamu na machungu?
12 Ndugu zangu, Je, mti wa mtini unaweza kuzaa matunda ya mzeituni, au mzabibu unazaa matunda ya mtini? Wala chemchemi ya maji chumvi haitoi maji yasio na chumvi.
13 Ni nani miongoni mwenu aliye na hekima na ufahamu? Hebu mtu huyo na aoneshe maisha mema katika kazi zake kwa unyenyekevu utokanao na hekima.
14 Lakini kama mnao wivu mkali na nia ya ubinafsi mioyoni mwenu, msijivune na kusema uongo mkiupinga ukweli.
15 Hii siyo hekima ile ishukayo kutoka juu, lakini badala yake ni ya kidunia, si ya kiroho, na ni ya kipepo.
16 Kwa kuwa palipo na wivu na ubinafsi upo, kuna vurugu na kila matendo maovu
17 Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, kisha kupenda amani, upole na ukarimu, yenye kujaa rehema na matunda mema, bila kupendelea watu fulani, na kweli.
18 Na tunda la haki hupandwa katika amani kwa wale ambao wanatenda mambo ya amani.