11
1 Basi mtu mmoja jina lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Alitokea Bethania, kijiji cha Mariamu na dada yake Martha.
2 Alikuwa ni Mariamu yule yule aliyempaka Bwana Marhamu na kumfuta miguu yake kwa nywele zake, ambaye ndugu yake Lazaro alikuwa ni mgonjwa.
3 Ndipo dada hawa walituma ujumbe kwa Yesu na kusema, “Bwana, angalia yule umpendaye anaumwa.”
4 Yesu aliposikia alisema, “Ugonjwa huu si wa mauti, lakini, badala yake ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu ili kwamba Mwana wa Mungu apate kutukuzwa katika huo Ugonjwa.”
5 Yesu alimpenda Martha na dada yake na Lazaro.
6 Aliposikia kuwa Lazaro ni mgonjwa, Yesu alikaa siku mbili zaidi mahali alipokuwa.
7 Ndipo baada ya hili aliwaambia wanafunzi wake, “Twendeni Uyahudi tena.”
8 Wanafunzi wakamwambia, “Rabi, Wayahudi walikuwa wakijaribu kukuponda mawe, na wewe unataka kurudi huko tena?”
9 Yesu akawajibu, “Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu anapotembea mchana hawezi kujikwaa, kwa sababu anaona kwa nuru ya mchana.
10 Hata hivyo, ikiwa atatembea usiku, atajikwaa kwa sababu nuru haiko ndani yake.”
11 Yesu akasema mambo haya, na baada ya mambo haya, akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini ninakwenda ili kwamba nipate kumuamsha kutoka usingizini.”
12 Ndipo wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala, ataamka.
13 Wakati huu Yesu alikuwa akizungumza habari za kifo cha Lazaro, lakini wao walidhani anazungumza juu ya kulala usingizi.
14 Ndipo Yesu akazungumza nao wazi wazi, “Lazaro amekufa.
15 Nina furaha kwa ajili yenu, kwamba sikuwepo kule ili kwamba mpate kuamini. Twendeni kwake.”
16 Basi Tomaso, aliyeitwa Pacha, aliwaambia wanafunzi wenzake, “Nasi twendeni pia tukafe pamoja na Yesu.”
17 Wakati Yesu alipokuja, alikuta kwamba Lazaro tayari amekwishakuwa kaburini siku nne.
18 Nayo Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu kama kilomita arobaini na tano hivi.
19 Wengi kati ya Wayahudi wakaja kwa Martha na Mariamu kuwafariji kwa ajili ya ndugu yao.
20 Ndipo Martha aliposikia kuwa Yesu anakuja, alienda kukutana naye, lakini Mariamu aliendelea kukaa nyumbani.
21 Ndipo Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungelikuwa hapa, kaka yangu asingelikufa.
22 Hata sasa, najua ya kuwa lolote utakaloomba kutoka kwa Mungu, atakupatia.”
23 Yesu akamwambia, kaka yako atafufuka tena.”
24 Martha akamwambia, najua kwamba atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.”
25 Yesu akamwambia, “Mimi ni ufufuo na uzima; yeye aniaminiye, ingawa atakufa, hata hivyo atakuwa anaishi;
26 na yeye aishiye na kuniamini mimi hatakufa. Unaamini hili?”
27 Akamwambia, “Ndiyo, Bwana naamini kwamba wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu, yeye ajaye katika ulimwengu.”
28 Alipokwisha kusema hili, alienda zake na kumwita dada yake Mariamu faraghani. Akasema, “Mwalimu yuko hapa na anakuita.”
29 Mariamu aliposikia haya, aliinuka kwa haraka na kwenda kwa Yesu.
30 Naye Yesu alikuwa hajaja bado ndani ya kijiji, bali alikuwa bado mahali alipokutana na Martha.
31 Ndipo Wayahudi waliokuwa na Mariamu katika nyumba na wale waliokuwa wakimfariji, walipomuona akiinuka haraka na kutoka nje, walimfuata; walidhani kuwa anaenda kaburini ili akalie huko.
32 Ndipo Mariamu, alipofika pale Yesu alipokuwa alimuona na, alianguka chini ya miguu yake na kumwambia, “Bwana, kama ungelikuwa hapa, ndugu yangu asingelikufa.”
33 Yesu alipomuona analia, na Wayahudi waliokuja pamoja naye walikuwa wakilia pia, aliomboleza katika roho na kufadhaika;
34 akasema, “Mmemlaza wapi? wakamwambia, Bwana, njoo utazame.”
35 Yesu akalia.
36 Ndipo Wayahudi wakasema, “Angalia alivyompenda Lazaro!”
37 Lakini wengine kati yao wakasema, “Siyo huyu, mtu aliyeyafumbua macho ya yule aliyekuwa kipofu, hakuweza kumfanya huyu mtu asife?”
38 Ndipo Yesu, hali akiomboleza nafsini mwake tena, alienda kwenye kaburi. Sasa lilikuwa pango, na jiwe limewekwa juu yake.
39 Yesu akasema, “Liondoweni jiwe.” Martha, dada yake na Lazaro, yeye aliyekufa, akamwambia Yesu, “Bwana, kwa muda huu, mwili utakuwa umeoza, kwa sababu amekwishakuwa maiti kwa siku nne.”
40 Yesu akamwambia, “Mimi sikukuwaambia ya kwamba, kama ukiamini, utauona utukufu wa Mungu?”
41 Kwa hiyo wakaliondoa jiwe. Yesu akainua macho yake juu na kusema, “Baba, nakushukuru kwa kuwa unanisikiliza.
42 Nilijua kwamba unanisikia mara zote, lakini ni kwa sababu ya kusanyiko ambalo limesimama kunizunguka kwamba nimesema haya, ili kwamba wapate kuamini kuwa wewe umenituma.”
43 Baada ya kusema haya, alilia kwa sauti kubwa, “Lazaro, toka nje!”
44 Mfu alitoka nje amefungwa mikono na miguu kwa sanda za kuzikia, na uso wake ulifungwa na kitambaa.” Yesu akawaambia, “Mfungueni mkamwache aende.”
45 Ndipo Wayahudi wengi waliokuja kwa Mariamu na kuona Yesu alichofanya, walimwamini;
46 lakini baadhi yao walienda kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo aliyoyafanya Yesu.
47 Ndipo wakuu wa Makuhani na Mafarisayo wakakusanyika pamoja katika baraza na kusema, “Tutafanya nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi.
48 Ikiwa tutamwacha hivi peke yake, wote watamwamini; Warumi watakuja na kuchukua vyote mahali petu na taifa letu.”
49 Hata hivyo, mtu mmoja kati yao, Kayafa, aliyekuwa kuhani Mkuu mwaka huo, akawaambia, “ Hamjui chochote kabisa.
50 Hamfikirii kwamba yafaa kwa ajili yenu kwamba mtu mmoja yapasa kufa kwa ajili ya watu kuliko taifa lote kuangamia.”
51 Haya hakuyasema kwa sababu yake mwenyewe, badala yake, kwa kuwa alikuwa kuhani mkuu mwaka ule, alitabiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa;
52 na si kwa taifa peke yake, bali Yesu apate vile vile kuwakusanya watoto wa Mungu ambao wametawanyika sehemu mbali mbali.
53 Kwa hiyo kuanzia siku hiyo na kuendelea wakapanga namna ya kumwua Yesu.
54 Yesu hakutembea tena wazi wazi kati ya Wayahudi, bali aliondoka hapo na kwenda nchi iliyo karibu na jangwa katika mji uitwao Efraimu. Hapo alikaa na wanafunzi.
55 Basi Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu, na wengi wakapanda kwenda Yerusalemu nje ya mji kabla ya Pasaka ili wapate kujitakasa wenyewe.
56 Walikuwa wakimtafuta Yesu, na kuzungumza kila mmoja walipokuwa wamesimama hekaluni, “Mnafikiri nini? Kwamba hatakuja katika sikukuu?”
57 Wakati huu wakuu wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kwamba ikiwa mmoja atajua Yesu alipo, anapaswa kutoa taarifa ili kwamba wapate kumkamata.