20
1 Mapema siku ya kwanza ya juma, kungali bado giza, Mariamu Magdalena alikuja kaburini; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini.
2 Kwa hiyo akakimbia mbio kwenda kwa Simon Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, kisha akawaambia, “wamemchukua Bwana kaburini, nasi hatujui kule walikomlaza.”
3 Kisha Petro na yule mwanafunzi mwingine wakatoka, kuelekea kaburini.
4 Wote walipiga mbio kwa pamoja; yule mwanafunzi mwingine alikimbia kwa kasi zaidi ya Petro nakufika kaburini wa kwanza.
5 Akasimama na kisha kuangalia kaburini; akaiona ile sanda ya kitani imelala, lakini hakuingia ndani.
6 Kisha Simon Petro naye akafika akaingia ndani ya Kaburi. Akaiona ile sanda ya kitani imelala pale
7 na ile leso iliyokuwa kichwani pake haikuwa imelala pamoja na zile sanda za kitani bali ilikuwa imelala pembeni peke yake.
8 Ndipo yule mwanafunzi mwingine naye alipoingia ndani ya kaburi; akaona na kuamini.
9 Kwa kuwa hadi wakati huo walikuwa bado hawajayajua maandiko kwamba ilimlazimu Yesu afufuke tena katika wafu.
10 Kisha wanafunzi wakaenda tena nyumbani kwao.
11 Hata hivyo, Mariamu alikuwa amesimama kaburini akilia, alivyokuwa akiendelea kulia alisimama kisha akatazama kaburini.
12 Akaona malaika wawili wenye sura nyeupe wamekaa mmoja kichwani na mwingine miguuni mahali ambapo Yesu alikuwa amelala.
13 Nao wakamwambia, “Mwanamke, kwa nini unalia?” Naye akawaambia, “Ni kwa sababu wamemchukua Bwana wangu, nami sijui walikomweka.”
14 Alipokwisha sema hayo, aligeuka na kumwona Yesu akiwa amesimama. Lakini hakutambua kama huyo alikuwa Yesu.
15 Naye Yesu akamwambia, “Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?” Naye huku akidhani kuwa ni mtunza bustani akamwambia, “Bwana, kama ni wewe uliyemchukua, niambie ulikomweka, nami nitamchukua.”
16 Yesu akamwambia, “Mariamu.” Naye akageuka mwenyewe na kumwambia kwa Kiaramu, “Raboni,” yaani hii ni kusema, “Mwalimu.”
17 Yesu akamwambia, “Usiniguse, kwani bado sijapaa kwenda kwa baba; bali uende kwa ndugu zangu ukawaambie kuwa nitapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye pia ni Baba yenu, Mungu wangu na Mungu wenu.”
18 Mariamu Magdalena akaja kuwaambia wanafunzi, “Nimemwona Bwana,” na kwamba amemwambia mambo haya.
19 Na ilipokuwa jioni, siku hiyo, siku ya kwanza ya juma, na milango ikiwa imefungwa mahali wanafunzi walipokuwapo kwa kuwahofia Wayahudi, Yesu alikuja na kusimama katikati yao na kuwaambia, “Amani iwe kwenu.”
20 Alipokwisha sema haya akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Nao wanafunzi walipomwona Bwana walifurahi.
21 Kisha Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi. Kama vile Baba alivyonituma mimi, vivyo hivyo nami nawatuma ninyi.”
22 Yesu alipokwisha sema hayo, akawavuvia akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu.
23 Yeyote mmsameheye dhambi, wamesamehewa; na wale mtakaowafungia watafungiwa.”
24 Thomaso, mmoja wa wale kumi na wawili, aliyeitwa Didimas, hakuwa na wanafunzi wenzake Yesu alipokuja.
25 Wale wanafunzi wengine waka mwambia baadaye, “Tumemwona Bwana.” Naye akawambia, “Kama sitaona alama za misumari katika mikono yake, na kuweka vidole vyangu kwenye hizo alama, na pia kuweka mkono wangu kwenye ubavu wake sitaamini.”
26 Baada ya siku nane wanafunzi walikuwa chumbani tena, naye Thomaso alikuwa pamoja nao. Wakati milango ilipokuwa imefungwa Yesu alisimama katikati yao. na akasema, “Amani na iwe nanyi.”
27 Kisha akamwambia Thomaso, leta kidole chako na uone mikono yangu; leta hapa mikono yako na uweke kwenye ubavu wangu; wala usiwe asiyeamini bali aaminiye.”
28 Naye Thomaso akajibu na kumwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu.”
29 Yesu akamwambia, Kwa kuwa umeniona, umeamini. Wamebarikiwa wao wanaoamini, pasipokuona.”
30 Kisha Yesu alifanya ishara nyingi mbele ya wanafunzi, ambazo hazijawahi kuandikwa katika kitabu hiki;
31 bali hizi zimeandikwa ili kwamba muweze kuamini kwamba Yesu ndiye Kristo, mwana wa Mungu, na kwamba muaminipo muwe na uzima katika jina lake.