13
1 Mtu wa Mungu alikuja tokea Yuda kwa neno la BWANA kule Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa amesimama karibu na madhabahu ili kufukiza uvumba.
2 Akalia kinyume na zile madhabahu kwa neno la BWANA: “Ee madhabahu, madhabahu” hivi ndivyo asemavyo BWANA, 'Tazama, mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika familia ya Daudi, na juu yenu atawachinja makuhani ambao sasa wanafukiza uvumba mahali hapa pa juu kwa ajili yako. Juu yako watachoma mifupa ya watu.'”
3 Kisha mtu wa Mungu akatoa ishara siku hiyohiyo, akisema, “Hii ndiyo isharaya kwamba BWANA amesema: 'Tazama, madhabahu zitavuunjika, na majivu yaliyo juu yatamwagika.”
4 Naye mfalme aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, kwamba amelia kinyume cha zile madhabahu kule Betheli, Yeroboamu akanyosha mkono wake kutoka madhabahuni, akisema, “mkamateni.” Ndipo ule mkono aliokuwa ameunyosha dhidi ya mtu wa Mungu ukakauka, kiasi kwamba hakuweza kuurudisha mwenyewe.
5 Na ile madhabahu ikavunjika vipande vipande, na yale majivu yakamwagika kutoka madhabahuni, kama ilivyokuwa imefafanuliwa kuwa ndiyo ishara ya kwamba mtu wa Mungu alikuwa amepewa kwa neno la BWANA.
6 Mfalme Yeroboamu akajibu akimwambia mtu wa Mungu, “Msihi BWANA, Mungu wako akupe neema ili uniombee, ili kwamba mkono wangu urejee kwangu tena.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwomba BWANA, na mkono wa mfalme ukarejea katika hali yake tena, na ukawa kama ulivyokuwa mwanzoni.
7 Yule mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “twende nyumbani kwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.”
8 Yule mtu wa Mungu akamwambia mfalme, “Hata kama utanipa nusu ya miliki yako. staende na wewe, wala sitakula au kunywa maji mahali hapa,
9 kwa sababu BWANA ameniamuru kwa neno lake, 'hutakula mkate wala kunywa maji, wala kurudi kwa njia ulioijia.'”
10 Kwa hiyo mtu wa Mungu akaondoka na hakurudi nyumbani kwa njia aliyokuja nayo huko Betheli.
11 Sasa kulikuwa na nabii mwingine mzee aliyekuwa akiishi Betheli, na mmoja wa wana wake akaja kumwambia mambo yote ambayo mtu wa Mungu amefanya siku hiyo kule Betheli. Wana wake wakamwambia pia maneno ambayo Yule mtu wa Mungu alimwambia mfalme.
12 Baba yao akawaambia, “Alienda kwa njia gani?” Wale wanawe walikuwa wamemwona yule mtu wa Mungu kutoka Yuda njia aliyotumia kurudi.
13 Kwa hiyo akawaambia wanawe, “Nitandikeni punda.” Kwa hiyo wakamtandikia punda naye akampanda.
14 Yule nabii mzee akamfuata yule mtu wa Mungu na akamkuta amekaa chini ya mti wa mwaloni; akamwambia, “Je, wewe ndiye mtu wa Mungu aliyetoka Yuda?” Naye akamjibu, “Mimi ndiye.”
15 Kisha yule nabii mzee akamwambia, “twende nyumbani kwangu ukale chakula.”
16 Yule mtu wa Mungu akamjibu, “Siwezi kurudi na wewe wala kuingia ndani na wewe, tena sitakula chakula wala kunywa maji pamoja na wewe mahali hapa,
17 kwa sababu niliamuriwa hivyo kwa neno la BWANA, 'Hautakula chakula wala kunywa maji kule, wala kurudi kwa njia utakayokuja nayo.'”
18 Kwa hiyo yule nabii mzee akamwambia, “Mimi pia ni nabii kama ulivyo, na malaika amesema na mimi neno la BWANA, akisema, 'Mrudishe aje na wewe katika nyumba yako, ili aweze kula chakula na kunywa maji.'” Lakini alikuwa anamdanganya mtu wa Mungu.
19 Kwa hiyo yule mtu wa Mungu akarudi pamoja na yule nabii mzee na akala chakula nyumbani kwake na akanywa maji.
20 Walipokuwa wamekaa mezani, neno la BWANA likamjia yule nabii aliyemrudisha,
21 naye akalia kwa mtu wa Mungu aliyetoka Yuda, akisema “BWANA anasema, 'Kwa kuwa umeshindwa kutii nenola BWANA na umeshindwa kuishika amri ya BWANA ambayo Mungu wako alikupa,
22 bali umerudi na umekula chakula na kunywa maji mahali ambapo BWANA alikwambia usile chakula wala kunywa maji, basi mwili wako hautazikwa kwenye makaburi ya baba zako.'”
23 Baada ya kula chakula na kunywa maji, Yule nabii akatandika punda wa mtu wa Mungu, yule mtu aliyerudi naye.
24 Baada ya mtu wa Mungu kuondoka, akakutana na simba njiani na kumwua barabarani, na mwili wake uliachwa barabarani. Na yule punda akasimama pembeni yake, na yule simba naye akasimama pembeni ya ule mwili.
25 Watu walipopita na kuuona ule mwili umeachwa barabarani, na yule simba akisimama karibu na ule mwili, walikuja wakaeleza habari hiyo mjini kule ambako yule nabii mzee aliishi.
26 Yule nabii aliyemrudisha toka njiani aliposikia, akasema, “Yeye mtu wa Muugu ndiye aliyeshindwa kutii neno la BWANA. Kwa hiyo BWANA alimtoa kwa simba, ambaye amemrarua katika vipande vipande na kumwua, kama vile neno la BWANA lilivyokuwa limemwonya.”
27 Kwa hiyo yule nabii mzee akawaamnbia wanawe, akisema, “Tandikeni punda wangu,” nao wakamtandikia.
28 Akaenda akaukuta mwili umeachwa barabarani, punda na simba wamesimama pembeni ya ule mwili. Yule simba hakuula ule mwili, wala hakumshambulia yule punda.
29 Yule nabii akauchukua ule mwili wa mtu wa Mungu, akaulaza juu ya punda, na akaurudisha. Akaja kwenye mji wake kuomboleza na kuuzika.
30 Akaulaza mwili kwenye kaburi lake, nao wakamwombolezea, wakisema, “Aa! ndugu yangu!”
31 Kisha baada ya kumzika, yule nabii mzee akawaambia wanawe, akasema, “Nitakapokufa, mtanizika kwenye kaburi ambalo tumemzika mtu wa Mungu. Mtalaza mifupa yangu pembeni mwa mifupa yake.
32 Kwa kuwa ule ujumbe uliosemwa na BWANA, dhidi ya madhabahu kule Betheli na dhidi ya nyumba zote za mahali pa juu katika mji wa Samaria, hakika yatatokea.
33 Baada ya haya Yeroboamu hakuuacha uovu wake, aliendelea kuchagua makuhani wa kawaida kwa ajili ya mahali pa juu kutoka kwa watu wa kila aina. Yeyote ambaye angeweza kutumika alimtakasa kuwa kuhani.
34 Jambo hili likawa dhambi kwenye familia ya Yeroboamu na kusababisha familia yake kuangamizwa na kuondolewa kabisa katika uso wa dunia.