22
1 Basi Sikukuu ya Mkate Usiyotiwa Chachu ilikuwa imekaribia, ambayo inaitwa Pasaka.
2 Makuhani wakuu na waandishi wakajadiliana namna ya kumuua Yesu, kwa sababu waliwaogopa watu.
3 Shetani akaingia ndani ya Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi Kumi na mbili.
4 Yuda akaenda kujadiliana na wakuu wa makuhani na wakuu namna ambavyo atamkabidhi Yesu kwao.
5 Walifurahi, na kukubaliana kumpa fedha.
6 Yeye aliridhia, na alitafuta fursa ya kumkabidhi Yesu kwao mbali na kundi la watu.
7 Siku ya mikate isiyotiwa chachu ikafika, ambapo kondoo wa Pasaka lazima atolewe.
8 Yesu akawatuma Petro na Yohana, akasema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuje tukile.”
9 Wakamuuliza, “Wapi unataka tuyafanyie hayo maandalizi?”
10 Akawajibu, “Sikilizeni, mtakapokuwa mmeingia mjini, mwanamume ambaye amebeba mtungi wa maji atakutana na ninyi. Mfuateni kwenye nyumba ambayo ataingia.
11 Kisha mwambieni bwana wa nyumba, “Mwalimu anakwambia, “Kiko wapi chumba cha wageni, mahali ambapo nitakula Pasaka na wanafunzi wangu?”
12 Atawaonyesha chumba cha ghorofani ambacho kiko tayari. Fanyeni maandalizi humo.”
13 Hivyo wakaenda, na wakakuta kila kitu kama alivyowaambia. Kisha wakaandaa chakula cha Pasaka.
14 Muda ulipofika alikaa na wale mitume.
15 Kisha akawaambia, “Nina shauku kubwa ya kula sikukuu hii ya Pasaka na ninyi kabla ya kuteswa kwangu.
16 Kwa maana nawaambieni, sitakula tena mpaka itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu.”
17 Kisha Yesu akachukua kikombe, na alipokwisha kushukuru, akasema, “Chukueni hiki, na mgawane ninyi kwa ninyi.
18 Kwa maana nawaambia, sitakunywa tena mzao wa mzabibu, mpaka ufalme wa Mungu utakapokuja.”
19 Kisha akachukua mkate, na alipokwisha kushukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu ambao umetolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.”
20 Akachukua kikombe vivyo hivyo baada ya chakula cha usiku akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, ambayo imemwagika kwa ajili yenu.
21 Lakini angalieni. Yule anisalitie yuko pamoja nami mezani.
22 Kwa maana Mwana wa Adamu kwa kweli aenda zake kama ilivyokwisha amuliwa. Lakini ole kwa mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu asalitiwa!”
23 Wakaanza kuulizana wao kwa wao, nani miongoni mwao ambaye angefanya jambo hili.
24 Kisha yakatokea mabishano katikati yao kwamba ni nani anaye dhaniwa kuwa mkuu kuliko wote.
25 Akawaambia, “Wafalme wa watu wa mataifa wana ubwana juu yao, na wale mwenye mamlaka juu yao wanaitwa waheshimiwa watawala.
26 Lakini haitakiwi kabisa kuwa hivi kwenu ninyi. Badala yake, acha yule ambaye ni mkubwa kati yenu awe kama mdogo. Na yule ambaye ni wa muhimu sana awe kama atumikaye.
27 Kwa sababu yupi mkubwa, yule akaaye mezani au yule anayetumika? Je si yule aketie mezani? Na mimi bado ni kati yenu kama atumikaye.
28 Lakini ninyi ndio ambao mmeendelea kuwa nami katika majaribu yangu.
29 Nawapa ninyi ufalme, kama vile Baba alivyonipa mimi ufalme,
30 kwamba mpate kula na kunywa mezani kwangu kwenye ufalme wangu. Na mtakaa kwenye viti vya enzi mkizihukumu kabila kumi na mbili za Israel.
31 Simoni, Simoni, fahamu kwamba, Shetani ameomba awapate ili awapepete kama ngano.
32 Lakini nimekuombea, kwamba imani yako isishindwe. Baada ya kuwa umerudi tena, waimarishe ndugu zako.”
33 Petro akamwambia, “Bwana, niko tayari kwenda na wewe gerezani na hata katika mauti.”
34 Yesu akajibu, “Nakwambia, Petro, Jogoo hatawika leo, kabla hujanikana mara tatu kwamba unanijua.”
35 Kisha Yesu akawaambia, “Nilipowapeleka ninyi bila mfuko, kikapu cha vyakula, ua viatu, je mlipungukiwa na kitu?” Wakajibu “Hakuna.”
36 Kisha akawaambia, “Lakini sasa, kila mwenye mfuko, na auchukue pamoja na kikapu cha vyakula. Yule ambaye hana upanga imempasa auze joho lake anunue mmoja.
37 Kwa sababu nawaambia, yote ambayo yameandikwa kwa ajili yangu lazima yatimilike, 'Na alichukuliwa kama mtu ambaye anavunja torati.' Kwa sababu kile kilichotabiriwa kwa ajili yangu kinatimizwa.”
38 Kisha wakasema, “Bwana, tazama! Hizi hapa panga mbili.” Na akawaambia”yatosha.”
39 Baada ya chakula cha usiku, Yesu aliondoka, kama ambavyo amekuwa akifanya mara kwa mara, akaenda mlima wa Mzeituni, na wanafunzi wakamfuata.
40 Walipofika, aliwaambia, “Ombeni kwamba msiingie majaribuni.”
41 Akaenda mbali na wao kama mrusho wa jiwe, akapiga magoti akaomba,
42 akisema, “Baba, kama unataka, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nitakavyo mimi, lakini mapenzi yako yafanyike.”
43 Kisha malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu.
44 Akiwa katika kuugua, akaomba kwa dhati zaidi, na jasho lake likawa kama matone makubwa ya damu yakidondoka chini.
45 Wakati alipoamka kutoka katika maombi yake, alikuja kwa wanafunzi, na akawakuta wamelala kwa sababu ya huzuni yao,
46 na akawauliza, “Kwanini mnalala? Amkeni muombe, kwamba msiingie majaribuni.”
47 Wakati alipokuwa bado akiongea, tazama, kundi kubwa la watu likatokea, na Yuda, mmoja wa mitume kumi na wawili akiwaongoza. Akaja karibu na Yesu ili ambusu,
48 lakini Yesu akamwambia, “Yuda, je unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”
49 Wakati wale waliokuwa karibu na Yesu walipoona hayo yanayotokea, wakasema, “Bwana, je tuwapige kwa upanga?”
50 Kisha mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio lake la kulia.
51 Yesu akasema, “hii inatosha. Na akagusa sikio lake, akamponya.
52 Yesu akasema kwa kuhani mkuu, na kwa wakuu wa hekalu, na kwa wazee waliokuja kinyume chake, “Je mnakuja kana kwamba mnakuja kupambana na mnyang'anyi, na marungu na mapanga?
53 Nilipokuwa pamoja nanyi siku zote kwenye hekalu, hamkuweka mikono yenu juu yangu. Lakini hii ni saa yako, na mamlaka ya giza.”
54 Wakamkamata, wakamuongoza, wakamleta nyumbani mwa kuhani mkuu. Lakini Petro akamfuatilia kwa mbali.
55 Baada ya kuwa wamewasha moto katika ule uwanda wa ndani na walipokwisha kukaa chini pamoja, Petro akakaa katikati yao.
56 Mtumishi mmoja wa kike akamuona Petro alipokuwa amekaa katika mwanga utokanao na moto, akamtazama akamwambia, “Huyu mtu pia alikuwa pamoja naye.”
57 Lakini Petro akakana, akasema, “mwanamke, mimi simjui.”
58 Baada ya muda kidogo, mtu mwingine akamuona akasema “Wewe pia ni mmoja wao”. Lakini Petro akajibu, “Mwanaume, mimi siyo.”
59 Baada ya kama saa moja hivi, mwanaume mmoja akasisitiza akasema, “Kweli kabisa huyu mtu pia alikuwa pamoja naye, maana ni Mgalilaya.”
60 Lakini Petro akasema, “Mwanaume, sijui usemalo.” Na mara, wakati akiongea, jogoo akawika.
61 Akageuka, Bwana akamtazama Petro. Na Petro akalikumbuka neno la Bwana, pale alipomwambia, “Kabla ya jogoo kuwika leo, utanikana mimi mara tatu.”
62 Akienda nje, Petro akalia kwa uchungu mwingi.
63 Kisha wale wanaume waliokuwa wakimlinda Yesu, wakamdhihaki na kumpiga.
64 Baada ya kumfunika macho, wakamuuliza, wakisema, “Tabiri! Ni nani aliyekupiga?”
65 Wakaongea mambo mengine mengi kinyume cha Yesu na kumkufuru yeye.
66 Mara ilipokuwa asubuhi, wazee wa watu walikusanyika pamoja, wakuu wa makuhani na waandishi. Wakampeleka kwenye Baraza,
67 wakisema, “Kama wewe ni Kristo, tuambie.” Lakini yeye akawaambia, “Kama nikiwaambia, hamtaniamini,
68 na kama nikiwauliza hamtanijibu.”
69 Lakini kuanzia sasa na kuendelea, Mwana wa Adamu atakuwa amekaa mkono wa kuume wa nguvu ya Mungu.”
70 Wote wakasema, “Kwa hiyo wewe ni Mwana wa Mungu?” Na Yesu akawaambia, “Ninyi mmesema mimi ndiye.”
71 Wakasema, “Kwa nini bado tunahitaji tena ushahidi? Kwa sababu sisi wenyewe tumesikia kutoka katika kinywa chake mwenyewe.”