11
1 Wakati huo walipokuja Yerusalemu, walipokaribia Besthfage na Bethania, katika Mlima wa Mizeituni, Yesu aliwatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake
2 na aliwaambia, “Nendeni katika kijiji kinachokabiliana nasi. Mara mtakapoingia humo, mtamkuta mwanapunda ambaye hajapandwa. Mfungueni na mmlete kwangu.
3 Na kama yeyote akiwaambia, 'Kwa nini mnafanya hivi'?, mnapaswa kusema, 'Bwana anamhitaji na mara atamrudisha hapa'.”
4 Walikwenda na kumkuta mwanapunda amefungwa nje mlangoni kwenye mtaa ulio wazi, nao walimfungua.
5 Na baadhi ya watu walikuwa wamesimama pale na waliwaambia, “Mnafanya nini, kumfungua mwanapunda huyo?”
6 Waliwaambia kama Yesu alivyowaambia, na watu wakawaacha waende.
7 Wanafunzi wawili walimleta mwanapunda kwa Yesu na walitandika mavazi yao juu yake ili Yesu aweze kumpanda.
8 Watu wengi wakatandika mavazi yao barabarani, na wengine wakatandika matawi waliyoyakata kutoka mashambani.
9 Wale waliokwenda mbele yake na wale waliomfuata walipiga kelele, “Hosana! Amebarikiwa anayekuja kwa jina la Bwana.
10 Ubarikiwe ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi! Hosana kwa aliye juu”
11 Ndipo Yesu aliingia Yerusalemu na alikwenda hekaluni na alitazama kila kitu. Sasa, wakati ulikuwa umeenda, alikwenda Bethania pamoja nao kumi na wawili.
12 Siku iliyofuata, wakati walipokuwa wakirudi kutoka Bethania, alikuwa na njaa.
13 Na akaona mti wa mtini uliokuwa na majani kwa mbali, alikwenda kutazama kama angeweza kupata chochote juu yake. Na wakati alipokwenda kwa huo, hakupata chochote isipokuwa majani, kwa kuwa haikuwa majira ya mtini.
14 Aliuambia, “Hakuna yeyote atakayekula tunda kutoka kwako tena”. Na wanafunzi wake wakasikia.
15 Walikuja Yerusalemu, naye aliingia hekaluni na kuanza kuwatoa nje wauzaji na wanunuzi ndani ya hekalu. Alizipindua meza za wabadilishaji wa fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa.
16 Hakumruhusu yeyote kubeba chochote hekaluni kilichoweza kuuzwa.
17 Aliwafundisha na akasema, “Je haikuandikwa, 'nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote'? Lakini mmeifanya pango la wanyang'anyi”.
18 Makuhani wakuu na waandishi walisikia alivyokuwa amesema, nao walitafuta njia ya kumwua. Hata hivyo walimwogopa kwa sababu umati ulishangazwa na mafundisho yake.
19 Na kila wakati jioni ilipofika, waliondoka mjini.
20 Walipokuwa wakitembea asubuhi, waliuona mti wa mtini umekauka mpaka kwenye mizizi yake.
21 Petro alikumbuka na kusema, “Rabi! Tazama, mti wa mtini ulioulaani umekauka”.
22 Yesu aliwajibu, “Muwe na imani katika Mungu.
23 Amini nawaambia kwamba kila auambiaye mlima huu, 'Ondoka, na ukajitupe mwenyewe baharini, 'na kama hana mashaka moyoni mwake lakini anaamini kwamba alichokisema kitatokea, hivyo ndivyo Mungu atakavyofanya.
24 Kwa hiyo ninawaambia: kila kitu muombacho na kuuliza kwa ajili yake, aminini kwamba mmepokea, navyo vitakuwa vyenu.
25 Wakati mnaposimama na kuomba, mnapaswa kusamehe chochote mlichonacho dhidi ya yeyote, ili kwamba Baba yenu aliye mbinguni awasamehe pia ninyi makosa yenu.
26 (Zingatia: Mstari huu, “Lakini msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatasamehe dhambi zenu” haumo kwenye nakala za kale).
27 Walikuja Yerusalemu tena. Na Yesu alipokuwa akitembea hekaluni, makuhani wakuu, waandishi na wazee walikuja kwake.
28 Walimwambia, “Kwa mamlaka gani unafanya mambo haya?” Na ni nani aliyekupa mamlaka kuyafanya haya?”
29 Yesu aliwaambia, “Nitawauliza swali moja. Niambieni na mimi nitawaambia kwa mamlaka gani ninayafanya mambo haya.
30 Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au ulitoka kwa wanadamu? Nijibuni.”
31 Walijadiliana miongoni mwao na kushindana na kusema, “Kama tukisema, 'Kutoka mbinguni,' atasema, 'Kwa nini basi hamkumwamini?'
32 Lakini kama tukisema, 'Kutoka kwa wanadamu,'...” Waliwaogopa watu, kwa kuwa wote walishikilia kwamba Yohana alikuwa Nabii.
33 Ndipo walimjibu Yesu na kusema, “Hatujui. Ndipo Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani nayafanya mambo haya.