2
1 Baada ya Yesu kuzaliwa katika Bethelehem ya Uyahudi katika siku za mfalme Herode, watu wasomi kutoka mashariki ya mbali walifika Yerusalemu wakisema,
2 “Yuko wapi yeye ambaye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi? Tuliiona nyota yake mashariki nasi tumekuja kumwabudu.”
3 Pindi Mfalme herode aliposikia haya alifadhaika, na Yerusalemu yote pamoja naye.
4 Herode akawakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, naye akawauliza, “Kristo atazaliwa wapi?”
5 Wakamwabia, “Katika Bethelehemu ya Uyahudi, kwa kuwa hivi ndivyo ilivyoandikwa na nabii,
6 Nawe Bethelehemu, katika nchi ya Yuda, si mdogo miongoni mwa viongozi wa Yuda, kwa kuwa kutoka kwako atakuja mtawala atakayewachunga watu wangu Israeli.”
7 Hivyo Herode aliwaita wale wasomi kwa siri na kuwauliza ni wakati gani hasa nyota ilikuwa imeonekana.
8 Akawatuma Bethelehem, akisema, “Nendeni kwa uangalifu mkamtafute mtoto aliyezaliwa. Wakati mtakapomwona, nileteeni habari ili kwamba mimi pia niweze kuja na kumwabudu.”
9 Baada ya kuwa wamemsikia mfalme, waliendelea na safari yao, na nyota ile waliyokuwa wameiona mashariki iliwatangulia hadi iliposimama juu ya mahali mtoto aliyezaliwa alipokuwa.
10 Wakati walipoiona nyota, walifurahi kwa furaha kuu mno.
11 Waliingia nyumbani na kumuona mtoto aliyezaliwa na Mariamu mama yake. Walimsujudia na kumwabudu. Walifungua hazina zao na kumtolea zawadi za dhahabu, uvumba, na manemane.
12 Mungu aliwaonya katika ndoto wasirudi kwa Herode, hivyo, waliondoka kurudi katika nchi yao kwa njia nyingine.
13 Baada ya kuwa wameondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto na kusema, “Inuka, mchukue mtoto na mama yake na mkimbilie Misri. Bakini huko mpaka nitakapowaambia, kwa kuwa Herode atamtafuta mtoto ili amwangamize.
14 Usiku huo Yusufu aliamka na kumchukua mtoto na mama yake na kukimbilia Misri.
15 Aliishi huko hadi Herode alipo kufa. Hii ilitimiza kile Bwana alichokuwa amenena kupitia nabii, “Kutoka Misri nimemwita mwanangu.”
16 Kisha Herode, alipoona kuwa amedhihakiwa na watu wasomi, alikasirika sana. Aliagiza kuuawa kwa watoto wote wa kiume waliokuwa Bethelehemu na wote katika eneo lile ambao walikuwa na umri wa miaka miwili na chini yake kulingana na wakati aliokuwa amekwisha thibitisha kabisa kutoka kwa wale watu wasomi.
17 Ndipo lilipotimizwa lile neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yeremia,
18 “Sauti ilisikika Ramah, kilio na maombolezo makubwa, Raheli akiwalilia watoto wake, na alikataa kufarijiwa, kwa sababu hawapo tena.”
19 Herode alipo kufa, tazama malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri na kusema,
20 “Inuka mchukue mtoto na mama yake, na mwende katika nchi ya Israeli kwa maana waliokuwa wakitafuta uhai wa mtoto wamekufa.”
21 Yusufu aliinuka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, na wakaja katika nchi ya Israeli.
22 Lakini aliposikia kuwa Arikelau alikuwa anatawala Yuda mahali pa baba yake Herode, aliogopa kwenda huko. Baada ya Mungu kumuonya katika ndoto, aliondoka kwenda mkoa wa Galilaya
23 na alienda kuishi katika mji uitwao Nazareti. Hili lilitimiza kile kilichokuwa kimekwisha kunenwa kwa njia ya manabii, kwamba ataitwa Mnazareti.