25
1 Ndipo ufalme wa mbinguni utafananishwa na wanawali kumi waliochukua taa zao na kuondoka kwenda kumpokea bwana harusi.
2 Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano wengine walikuwa werevu.
3 Wanawali wapumbavu walipochukua taa zao, hawakuchukua mafuta yoyote.
4 Bali wanawali welevu walichukua vyombo vyenye mafuta pamoja na taa zao.
5 Sasa wakati bwana harusi amechelewa kufika, wote walishikwa usingizi na wakalala.
6 Lakini wakati wa usiku wa manane kulikuwa na yowe, 'Tazama, bwana harusi! Tokeni nje mkampokee.'
7 Ndipo hao wanawali waliamka wote na kuwasha taa zao.
8 Wale wapumbavu waliwaambia wale welevu, 'Mtupatie sehemu ya mafuta yenu kwa sababu taa zetu zinazimika.'
9 Lakini wale welevu waliwajibu na kuwaambia, 'Kwa kuwa hayatatutosha sisi na ninyi, badala yake nendeni kwa wanaouza mjinunulie kiasi kwa ajili yenu.'
10 Wakati wameenda huko kununua, Bwana harusi alifika, na wote waliokuwa tayari walienda naye kwenye sherehe ya harusi, na mlango ulifungwa.
11 Baadaye wale wanawali wengine pia walifika na kusema, 'Bwana, bwana, tufungulie.'
12 Lakini alijibu na kusema, 'Kweli nawaambia, Mimi siwajui.'
13 Kwa hiyo angalieni, kwa kuwa hamjui siku au saa.
14 Kwa kuwa ni sawa na mtu alipotaka kusafiri kwenda nchi nyingine. Aliwaita watumwa wake na kuwakabidhi utajiri wake.
15 Mmoja wao alimpatia talanta tano, mwingine alimpa mbili, na yule mwingine alimpa talanta moja. Kila mmoja alipokea kiasi kulingana na uwezo wake, na yule mtu alisafari kwenda zake.
16 Mapema yule aliyepokea talanta tano alienda kuziwekeza, na kuzalisha talanta zingine tano.
17 Vilevile yule aliyepokea talanta mbili, alizalisha zingine mbili.
18 Lakini mtumwa aliyepokea talanta moja, alienda zake, akachimba shimo ardhini, na kuificha fedha ya bwana wake.
19 Na baada ya muda mrefu, bwana wa watumwa hao alirudi na kutengeneza mahesabu nao.
20 Yule mtumwa aliyepokea talanta tano alikuja na kuleta talanta zingine tano, akasema, 'Bwana, ulinipa talanta tano. Tazama, nimepata faida ya talanta zingine tano.'
21 Bwana wake alimwambia, 'Hongera, mtumwa mzuri na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vidogo. Nitakupa madaraka juu ya vitu vingi. Ingia katika furaha ya bwana wako.'
22 Mtumwa aliyepokea talanta mbili alikuja na kusema, 'Bwana, ulinipa talanta mbili. Tazama, nimepata faida ya talanta zingine mbili,'
23 Bwana wake alimwambia, 'Hongera, mtumwa mzuri na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache. Nitakupa madaraka juu ya vitu vingi. Ingia katika furaha ya bwana wako.'
24 Baadaye mtumwa aliyepokea talanta moja alikuja na kusema, 'Bwana, najua kuwa wewe ni mtu mkali. Unachuma mahali ambapo hukupanda, na unavuna mahali ambapo hukusia.
25 Mimi niliogopa, nikaenda zangu na kuificha talanta yako katika udongo. Tazama, unayo hapa ile iliyo yako.'
26 Lakini bwana wake alijibu na kusema, 'Wewe mtumwa mwovu na mzembe, ulijua kwamba ninachuma mahali ambapo sijapanda na kuvuna mahali ambapo sikusia.
27 Kwahiyo ulipaswa kuwapa fedha yangu watu wa benki, na wakati wa kurudi kwangu ningeipokea ile yangu pamoja na faida.
28 Kwa hiyo mnyang'anyeni hiyo talanta na mpeni yule mtumwa aliye na talanta kumi.
29 Kila mtu aliye nacho, ataongezewa zaidi-hata kwa kuzidishiwa sana. Lakini kwa yeyote asiye na kitu, hata alicho nacho atanyang'anywa.
30 Mtupeni nje gizani huyo mtumwa asiyefaa, ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.'
31 Wakati Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake, na malaika wote pamoja naye, ndipo atakapokaa juu ya kiti chake cha utukufu.
32 Mataifa yote yatakusanyika mbele zake, naye atawatenganisha watu, kama vile mchungaji anavyowatenganisha kondoo na mbuzi.
33 Atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, bali mbuzi atawaweka mkono wa kushoto.
34 Kisha mfalme atawaambia wale walio mkono wake wa kulia, 'Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu.
35 Kwa kuwa nilikuwa na njaa na mlinipa chakula; Nilikuwa mgeni na mlinikaribisha;
36 Nilikuwa uchi, na mlinivika nguo; Nilikuwa mgonjwa na mkanitunza; Nilikuwa kifungoni na mkaniijia.'
37 Ndipo wenye haki watamjibu na kumwambia, 'Bwana, lini tulikuona ukiwa na njaa, na kukulisha? Au una kiu na tukakupa maji?
38 Na lini tulikuona ukiwa mgeni, na tukakukaribisha? Au ukiwa uchi na tukakuvisha nguo?
39 Na lini tulikuona ukiwa mgonjwa, au katika kifungo, na tukakujia?
40 Na mfalme atawajibu na kuwaambia, 'Kweli nawaambia, mlichotenda hapa kwa mmoja wa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.'
41 Ndipo atawaambia hao walio mkono wake wa kushoto, 'Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, nendeni katika moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya shetani na malaika zake,
42 kwa sababu nilikuwa na njaa lakini hamkunipa chakula; Nilikuwa na kiu lakini hamkunipa maji;
43 Nilikuwa mgeni lakini hamkunikaribisha; nikiwa uchi lakini hamkunipa mavazi; nikiwa mgonjwa na nikiwa kifungoni, lakini hamkunitunza.'
44 Ndipo wao pia watamjibu na kusema, 'Bwana, lini tulikuona ukiwa na njaa, au una kiu, au u mgeni, au ukiwa uchi, au ukiwa mgonjwa, au ukiwa mfungwa, na hatukukuhudumia?
45 Kisha atawajibu na kusema, 'Kweli nawaambia, kile ambacho hamkutenda kwa mmoja wa hawa wadogo, hamkunitendea mimi.'
46 Hawa watakwenda katika adhabu ya milele bali wenye haki katika uzima wa milele.”