6
1 Zingatia kutotenda matendo ya haki mbele ya watu ili kujionyesha, vinginevyo hutapata thawabu kutoka kwa Baba aliye mbinguni.
2 Hivyo basi unapotoa usipige tarumbeta na kujisifu mwenyewe kama wanafiki wanavyofanya katika masinagogi na katika mitaa, ili kwamba watu wawasifu. Kweli nawaambia, wamekwisha kupokea thawabu yao.
3 Lakini wewe unapotoa, mkono wako wa kushoto usijue kinachofanywa na mkono wa kulia,
4 ili kwamba zawadi yako itolewe kwa siri. Ndipo Baba yako aonaye sirini atakupatia thawabu yako.
5 Na unapokuwa ukiomba, usiwe kama wanafiki, kwa kuwa wanapenda kusimama na kuomba kwenye masinagogi na kwenye kona za mitaani, ili kwamba watu wawatazame. Kweli nawaambia, wamekwishapokea thawabu yao.
6 Lakini wewe, unapo omba, ingia chumbani. Funga mlango, na uombe kwa kwa Baba yako aliye sirini. Ndipo Baba yako aonaye sirini atakupatia thawabu yako.
7 Na unapokuwa ukiomba, usirudie rudie maneno yasiyo na maana kama mataifa wanavyofanya, kwa kuwa wanafikiri kwamba watasikiwa kwa sababu ya maneno mengi wanayosema.
8 Kwa hiyo, usiwe kama wao, kwa kuwa Baba yako anatambua mahitaji yako hata kabla hujaomba kwake.
9 Hivyo basi omba hivi: Baba yetu uliye mbinguni, ulitukuze jina lako.
10 Ufalme wako uje, mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni.
11 Utupatiye leo mkate wetu wa kila siku.
12 utusamehe deni zetu, kama nasi tunavyowasamehe wadeni wetu.
13 Na usitulete katika majaribu, lakini utuepushe kutoka kwa yule mwovu.'
14 Ikiwa mtawasemehe watu makosa yao, Baba yako aliye mbinguni pia atawasamehe ninyi.
15 Lakini ikiwa hamtawasamehe makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe makosa yenu.
16 Zaidi ya yote, unapokuwa umefunga, usioneshe sura ya huzuni kama wanafiki wanavyofanya, kwa kuwa wanakunja sura zao ili kwamba watu wawatambue wamefunga. Kweli ninakuambia, wamekwisha kupokea thawabu yao.
17 Lakini wewe, unapokuwa umefunga, paka mafuta kichwa chako na uoshe uso wako.
18 Hivyo haitakuonesha mbele ya watu kuwa umefunga, lakini tu itakuwa kwa Baba yako aliye sirini. Na Baba yako aonaye sirini, atakupa thawabu yako.
19 Usijitunzie hazina yako mwenyewe hapa duniani, ambapo nondo na kutu huharibu, ambapo wezi huvunja na kuiba.
20 Badala yake, jitunzie hazina yako mwenyewe mbinguni, ambapo wala nondo wala kutu hawezi kuharibu, na ambapo wezi hawawezi kuvunja na kuiba.
21 Kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo na moyo wako utakapokuwepo pia.
22 Jicho ni taa ya mwili. Kwa hiyo, ikiwa jicho lako ni zima, mwili wote utajazwa na nuru.
23 Lakini ikiwa jicho lako ni bovu, mwili wako wote umejaa giza totoro. Kwahiyo, ikiwa nuru ambayo imo ndani yako ni giza hasa, ni giza kubwa kiasi gani!
24 Hakuna hata mmoja anayeweza kuwatumikia mabwana wawili, kwa kuwa atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au la sivyo atajitoa kwa mmoja na kumdharau mwingine. Hamuwezi kumtumikia Mungu na mali.
25 Kwa hiyo nakuambia, usiwe na mashaka kuhusu maisha yako, kuwa utakula nini au utakunywa nini, au kuhusu mwili wako, utavaa nini. Je! Maisha si zaidi ya chakula na mwili zaidi ya mavazi?
26 Tazama ndege walioko angani. Hawapandi na hawavuni na hawakusanyi na kutunza ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha wao. Je ninyi si wa thamani zaidi kuliko wao?
27 Na ni nani miongoni mwenu kwa kujihangaisha anaweza kuongeza dhiraa moja kwenye uhai wa maisha yake?
28 Na kwa nini mna kuwa na wasiwasi kuhusu mavazi? Fikiria kuhusu maua kwenye mashamba, jinsi yanavyokua. Hayafanyi kazi na hayawezi kujivisha.
29 Bado ninawaambia, hata Sulemani katika utukufu wake wote hakuvikwa kama mojawapo ya haya.
30 Ikiwa Mungu anayavalisha majani katika mashamba, ambayo yadumu siku moja na kesho yanatupwa katika moto, je ni kwa kiasi gani atawavalisha ninyi, ninyi wenye imani ndogo?
31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi nakusema, 'Je tutakula nini?' au “Je tutakunywa nini?” au “Je tutavaa nguo gani?”
32 Kwa kuwa mataifa wanatafuta mambo haya, na Baba yenu wa mbinguni anajua kuwa mnahitaji hayo.
33 Lakini kwanza tafuteni ufalme wake na haki yake na haya yote yatakabidhiwa kwako.
34 Kwa hiyo, usione shaka kwa ajili ya kesho, kwa kuwa kesho itajishughulikia yenyewe. Kila siku inatosha kuwa na tatizo lake yenyewe.