Nahumu
1
1 Maono kuhusu Ninawi. Kitabu cha maono ya Nahumu, Mwelkoshi.
2 Yehova ni Mungu mwenye wivu na analipa kisasi; Yehova hulipa kisasi na amejaa ghadhabu; Yohova analipiza kisasi kwa adui zake, na huiendeleza hasira yake kwa adui zake.
3 Yehova ni mwenye nguvu nyingi na mpole wa hasira; hatakuwa na namna ya kuacha kuwahesabia hatia adui zake. Yehova hufanya njia yake kwenye upepo wa kisulisuli na dhoruba, na mawingu ni mavumbi ya miguu yake.
4 Huikemea bahari na kuifanya ikauke; hukausha mito yote. Bashani ni dhaifu, na Karmeli pia; maua ya Lebanoni ni dhaifu.
5 Milima hutetema kwenye uwepo wake, na vilima huyeyuka; dunia huanguka mbele zake, kabisa, dunia na watu wote wanaoishi ndani yake.
6 Ni nani anaweza kusimama mbele ya ghadhabu yake? Nani anaweza kuzuia ukali wa hasira yake? Ghadhabu yake imemwagwa kama moto, na miamba ameibomoa mbalimbali.
7 Yehova ni mwema, boma katika siku ya taabu; na yeye ni mwaminifu kwa wale wanaomkimbilia.
8 Lakini atafanya mwisho wa adui zake kwa mafuriko ya kutisha; atawawinda kwenye giza.
9 Watu wanapanga nini dhidi ya Yehova? Yeye atakomesha; taabu haitainuka mara ya pili.
10 Maana watakuwa wamevurugika kama michongoma; wataloweshwa katika kinywaji chao mwenyewe; wataharibiwa kabisa kwa moto kama mashina ya mabua.
11 Mtu mmoja aliinuka miongoni mwenu, Ninawi, aliyepanga ubaya dhidi ya Yehova, mtu ambaye aliimarisha uovu.
12 Hivi ndivyo anavyosema Yehova, “Hata kama wananguvu zao timilifu na idadi timilifu, hata hivyo watanyolewa, watu wao hawatakuwepo tena. Bali wewe, Yuda: Ingawa nimekutesa, sitakutesa tena.
13 Sasa nitaivunja ile nira ya watu kutoka kwako; nitaikata minyororo yako.
14 Yehova ametoa amri juu yako, Ninawi: “ Hakutakuwa na kizazi tena chenye kubeba jina lako. Nitazizuia sanamu zilizochongwa na kuziondoa sanamu za chuma kutoka kwenye nyumba za miungu yenu. Nitachimba makaburi yenu, kwa kudharauliwa kwenu.”
15 Tazama, juu ya milima kuna miguu ya mtu aletaye habari njema, anayetangaza amani! Sherehekeeni sikukuu zenu, Yuda, na tunzeni nadhiri zenu, kwa maana mwovu hatawavamia tena; ameondolewa kabisa.