Mithali
1
1 Mithali za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli.
2 Mithali hizi zinafundisha hekima na maarifa, kufundisha maneno ya busara,
3 ili mpate maarifa kwa ajili ya kuishi kwa kutenda wema, haki na adili.
4 Mithali hizi zinatoa hekima kwa wale ambao hawakufunzwa, na kuwapa vijana maarifa na hadhari.
5 Watu wenye busara wasikie na kuongeza elimu yao na watu wenye ufahamu wapate mwongozo,
6 kwa kuelewa mithali, misemo, vitendawili na maneno ya wenye busara.
7 Hofu ya Yehova ni chanzo cha maarifa- wapumbavu hudharau hekima na nidhamu.
8 Mwanangu, sikia fundisho la baba yako na wala usiziache kanuni za mama yako;
9 zitakuwa kilemba cha neema katika kichwa chako na jebu zinazoning'inia kwenye shingo yako.
10 Mwanangu wenye dhambi wakikushawishi katika dhambi zao, kataa kuwafuata.
11 Kama watasema, “ haya tufuatae, tuvizie ili kufanya mauaji, tujifiche ili tuwashambulie watu wasio na hatia, pasipo sababu.
12 Haya tuwameza wakiwa hai, kama kuzimu inavyowachukua wenye afya, na kuwa kama wale waangukao kwenye shimoni.
13 Tutapata vitu vyote vya thamani; tutazijaza nyumba zetu vile tunavyoiba kwa wengine.
14 Weka vitu vyako kwetu; tutakuwa na mfuko moja kwa pamoja.”
15 Mwanangu, usitembee katika njia moja pamoja nao; usiruhusu mguu wako kugusa katika mapito yao;
16 miguu ya hukimbilia mabaya na huharakisha kumwaga damu.
17 Kwa kuwa haina maana kumtegea ndege mtego wakati ndege anaona.
18 Watu hawa huvizia kujiua wenyewe—wanatega mtego kwa ajili yao wenyewe.
19 Ndivyo zilivyo njia za kila ambaye hupata utajiri kwa udhalimu; mapato ya udhalimu huondoa uhai wa wenye utajiri.
20 Hekima inalia kwa sauti mtaani, inapaza sauti katika viwanja;
21 katika mitaa inalia kwa sauti kuu, kwenye maingilio ya milango ya mji inasema “
22 Mpaka lini enyi wajinga mtapenda kuwa wajinga? Mpaka lini enyi wenye dhihaka mtapenda dhihaka, na hadi lini enyi wapumbavu, mtachukia maarifa?
23 Zingatia karipio langu; nitatoa mawazo yangu kwa ajili yenu; nitawafahamisha maneno yangu.
24 Nimeita, nanyi mkakataa kusikiliza; nimeunyosha mkono wangu, wala hakuna aliyezingatia.
25 Lakini mumedharau mafundisho yangu yote na wala hamkuzingatia maelekezo yangu.
26 Nitacheka katika taabu yenu, nitawadhihaki wakati wa kupatwa taabu-
27 hofu ya kutisha itawapata kama tufani na maafa yatawakumba kama upepo wa kisulisuli, taabu na uchungu vitawapata.
28 Halafu wataniita, nami sitawajibu; wataniita katika hali ya kukata tamaa lakini hawataniona.
29 Kwa sababu wamechukia maarifa na hawakuchagua kuwa na hofu ya Yehova,
30 hawakufuata mafundisho yangu na wakayadharau masahihisho yangu yote.
31 Watakula matunda ya njia zao, na watashibishwa kwa matunda ya hila zao wenyewe.
32 kwa maana wajinga hufa wanaporudi nyuma, na kutojali kwa wapumbavu kutawaangamiza.
33 Bali kila anisikilizaye ataishi kwa usalama na atapumzika salama pasipo hofu ya maafa.