5
Mwanangu, zingatia hekima yangu; sikiliza kwa makini ufahamu wangu, ili ujifunze busara na midomo yako iweze kuhifadhi maarifa. Maana midomo ya malaya hutiririsha asali na kinywa chake ni laini kuliko mafuta, lakini mwishoni anakuwa mchungu kama mnyoo, hukata kama upunga mkali. Miguu yake huelekea mauti; hatua zake huelekea njia yote ya kuzimu. Hafikirii njia ya uzima. Hatua za miguu yake hupotea, maana hajui anakwenda wapi. Sasa, wanangu, nisikilizeni; wala msiache kusikiliza maneno ya kinywa changu. Lindeni njia yenu mbali naye wala msiende karibu na mlango wa nyumba yake. Kwa njia hiyo hamtawapa wengine heshima yenu au miaka ya uzima wenu kwa mtu mkatiri; 10 wageni usije kufanya karamu kwa utajiri wenu; kazi mliyoifanya haitaenda katika nyumba ya wageni. 11 Mwishoni mwa maisha yenu mtajuta ambapo nyama na mwili wenu vitaangamia. 12 Nanyi mtasema, “ Namna gani nilichukia fundisho na moyo wangu ulidharau sahihisho! 13 Sikuweza kuwatii walimu wangu au kuwasikiliza walionielekeza. 14 Nilikuwa nimeharibika kabisa katikati ya kusanyiko, miongoni mwa makutano ya watu.” 15 Munywe maji kutoka kwenye birika lenu mwenyewe na munywe maji yanatiririka kutoka kwenye kisima chenu. 16 Je inapaswa chemichemi yenu ifurike popote na mifereji yenu ya maji itiririke katika njia kuu? 17 Yawe yenu wenyewe peke yenu wala si kwa wageni. 18 Chemichemi yako ibarikiwe na umfurahie mke wa ujana wako. 19 Maana ni ayala apendezaye na kulungu mwenye uzuri. Matiti yake na yakujaze furaha muda wote; daima na utekwe na upendo wake. 20 Mwanangu, kwa nini uwe mateka wa malaya, kwa nini uyakumbatie matiti ya mwanamke mgeni? 21 Yehova huona kila kitu afanyacho mtu na huangalia mapito yake yote. 22 Mtu mwovu atatekwa na makosa yake mwenyewe; kamba za dhambi yake zitamnasa kwa nguvu. 23 Atakufa kwa kukosa maonyo; atapotelea mbali kwa upumbavu wake wingi.