102
Maombi ya aliyeteswa wakati yeye alipolemewa na kumwaga maombolezo yake mbele ya Yahwe.
1 Sikia maombi yangu, Ee Yahwe; sikia kulia kwangu kwako.
2 Usiufiche uso wako mbali nami wakati wa shida. Unisikilize. Nikuitapo, unijibu upesi.
3 Kwa maana siku zangu zinapita kama moshi, na mifupa yangu kama moto.
4 Moyo wangu umeumizwa na niko kama majani yaliyo kauka. Ninasahau kula chakula chochote.
5 Kwa muendelezo wa kuugua kwangu, nimekonda sana.
6 Niko kama mwali wa jangwani; nimekuwa kama bundi magofuni.
7 Ninalala macho kama shomoro faraghani, pekeyake juu ya paa.
8 Adui zangu wananilaumu mchana kutwa; wale wanao nidhihaki hutumia jina langu katika laana.
9 Ninakula majivu kama mkate na kuchanganya kinywaji changu kwa machozi.
10 Kwa sababu ya hasira yako kali, umeniinua juu kunitupa chini.
11 Siku zangu ni kama kivuli kanachofifia, na ninanyauka kama majani.
12 Lakini wewe, Yahwe, unaishi milele, na kumbukumbu lako ni kwa vizazi vyote.
13 Wewe utasimama na kuirehemu Sayuni. Sasa ni wakati wa mkurehemu yeye. Wakati ulio teuliwa umefika.
14 Maana watumishi wako wameyaridhia mawe yake pendwa na kuyaonea huruma mavumbi ya magofu yake.
15 Mataifa wataliheshimu jina lako, Yahwe, na wafalme wote wa nchi watauheshimu utukufu wako.
16 Yahwe ataijenga tena Sayuni na ataonekana katika utukufu wake.
17 Wakati huo, atajibu maombi ya fukara; hatayakataa maombi yao.
18 Hii itaandikwa kwa ajili ya vizazi vijavyo, na watu ambao bado hawajazaliwa watamsifu Yahwe.
19 Maana ametazama chini toka mahali pa juu patakatifu;
20 Toka mbinguni Yahwe ameiangalia nchi, ili kusikia kuugua kwa wafungwa, kuwafungua waliohukumiwa kufa.
21 Kisha watu watalitangaza jina la Yahwe katika Sayuni na sifa zake katika Yerusalemu
22 pindi mataifa na falme watakapokusanyika pamoja kumtumikia Yahwe.
23 Amechukua nguvu zangu katikati ya siku zangu za kuishi, amezifupisha siku zangu.
24 Nilisema, “Mungu wangu, usinichukue katikati ya siku zangu; wewe uko hapa hata kizazi chote.
25 Tangu zama za kale wewe uliiweka nchi mahali pake; mbingu ni kazi ya mikono yako.
26 Mbingu na nchi zitaangamia lakini wewe utabaki; zitachakaa kama mavazi; utaziondoa kama watu waondoavyo mavazi yaliyo chakaa, nazo hazitaonekana tena.
27 Lakini wewe ni yuleyule, na miaka yako haitakuwa na mwisho.
28 Watoto wa watumishi wako wataendelea kuishi, na uzao wao utaishi katika uwepo wako.