140
Kwa kiongozi wa muziki. Zaburi ya Daudi.
1 Yahwe, uniokoe dhidi ya waovu; unikinge dhidi ya watu wenye vurugu.
2 Wao wanapanga uovu mioyoni mwao; wanasababisha mapigano kila siku.
3 Ndimi zao zinajeruhi kama nyoka; sumu ya fira imo midomoni mwao. Selah
4 Ee Yahwe, unilinde dhidi ya mikono ya waovu; unikinge na vurugu za watu wanaopanga kuniangusha.
5 Wenye majivuno wameweka mtego kwa ajili yangu; wameeneza nyavu; wameweka kitanzi kwa ajili yangu. Selah
6 Nilimwambia Yahwe, “Wewe ni Mungu wangu; usikie kilio changu unihurumie.”
7 Ee Yahwe, Bwana wangu, wewe ni mwenye nguvu uwezaye kuniokoa; hunifunika ngao kichwa changu siku ya vita.
8 Ee Yahwe, usiyatimize matakwa ya waovu; usiruhusu njama zao kufanikiwa. Selah
9 Wale wanao nizunguka huinua vichwa vyao; madhara ya midomo yao wenyewe na yawafunike.
10 Makaa ya moto na yawaangukie; uwatupe motoni, kwenye shimo refu, wasiweze kuinuka tena.
11 Watu wenye ndimi na wasifanywe salama juu ya nchi; na uovu umuwinde kumpiga mtu mwenye vurugu mpaka afe.
12 Ninajua kuwa Yahwe atahukumu kwa haki walioteswa, na kuwa atawapa haki wahitaji.
13 Hakika watu wenye haki watalishukuru jina lako; watu wanyoofu wataishi uweponi mwako.