47
Kwa kiongozi wa muziki. Zaburi ya wana wa Korah.
1 Pigeni makofi, enyi watu wote; mpigieni Mungu kelele za ushindi.
2 Kwa maana Yahwe Aliye Juu anatisha; ni Mfalme mkuu dunia yote.
3 Yeye anawatiisha chini yetu na mataifa chini ya miguu yetu.
4 Yeye huchagua urithi kwa ajili yetu, utukufu wa Yakobo ambaye alimpenda. Serah
5 Mungu ameinuliwa juu kwa shangwe, Kwa mbiu ya shangwe Yahwe yu juu.
6 Mwimbieni Mungu sifa, imbeni sifa; mwimbieni sifa Mfalme wetu, imbeni sifa.
7 Kwa maana Mungu ni Mfalme duniani kote; mwimbieni mkiwa na uelewa.
8 Mungu anatawala mataifa yote; Mungu hukaa kwenye kiti cha enzi.
9 Wakuu wa watu wamekusanyika pamoja kwa watu wa Mungu wa Ibrahimu; kwa kuwa ngao za duniani ni za Mungu; yeye ameinuliwa juu sana.