92
Zaburi, wimbo kwa ajili ya siku ya Sabato.
1 Ni jambo jema kumshukuru Yahwe na kuliimbia sifa jina lako, Uliye Juu,
2 kutangaza uaminifu wa agano lako wakati wa asubuhi na uaminifu wako kila usiku,
3 kwa kinubi cha nyuzi kumi na kwa tuni ya kinubi.
4 Kwa kuwa wewe, Yahwe, matendo yako yamenifurahisha. Nitaimba kwa furaha kwa sababu ya matendo ya mikono yako.
5 Ni jinsi gani matendo yako ni makuu, Yahwe! mawazo yako ni ya kina.
6 Mtu mpumbavu hawezi kuyajua, wala mjinga kuyaelewa haya:
7 Wasio haki watakapochipuka kama nyasi, na hata watendao uovu watakapo stawi, bado wataangamizwa kwenye uharibifu wa milele.
8 Lakini wewe, Yahwe, utatawala milele.
9 Hakika, watazame adui zako, Yahwe! Hakika, watazame adui zako. Wataangamia! Wale wote watendao maovu watatawanywa.
10 Wewe umeyainua mapembe yangu kama mapembe ya Nyati wa porini; nimepakwa mafuta safi.
11 Macho yangu yameona kuanguka kwa adui zangu; masikio yangu yamesikia maangamizi ya maadui zangu waovu.
12 Wenye haki watastawi kama mtende; watakua kama mwerezi wa Lebanoni.
13 Wamepandwa katika nyumba ya Yahwe; wakistawi katika nyua za Mungu wetu.
14 Wao huzaa matunda hata uzeeni; hukaa safi na wenye afya,
15 kutangaza kuwa Yahwe ni wa haki. Yeye ni mwamba wangu, na hakuna udhalimu ndani yake.