6
1 Tuseme nini basi? Tuendelee katika dhambi ili neema iongezeke?
2 La hasha. Sisi tuliokufa katika dhambi, tunawezaje tena kuishi katika hiyo?
3 Je hamjui ya kuwa wale waliobatizwa katika Kristo walibatizwa katika mauti yake?
4 Tulikuwa tumezikwa pamoja naye kupitia ubatizo katika kifo. Hii ilifanyika ili kwamba kama vile Kristo alivyoinuliwa kutoka mauti kupitia utukufu wa Baba, ili kwamba nasi tuweze kutembea katika upya wa maisha.
5 Maana ikiwa tumeunganishwa pamoja naye katika mfano wa kifo chake, pia tutaunganishwa katika ufufuo wake.
6 Sisi tunajua hivi, utu wetu wa zamani ulisulubiwa pamoja naye, ili kwamba mwili wa dhambi uharibiwe. Hii ilitokea ili kwamba tusiendelee kuwa watumwa wa dhambi.
7 Yeye aliyekufa amefanywa mwenye haki kulingana na dhambi.
8 Lakini kama tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pamoja naye pia.
9 Tunajua kwamba Kristo amefufuliwa kutoka katika wafu, na kwamba si mfu tena. Kifo hakimtawali tena.
10 Maana kwa habari ya kifo alichokufa kwa dhambi, alikufa mara moja kwa ajili ya wote. Hata hivyo, maisha anayoishi, anaishi kwa ajili ya Mungu.
11 Kwa njia iyo hiyo, nanyi pia mnapaswa kujihesabu kuwa wafu katika dhambi, bali hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.
12 Kwa sababu hiyo usiruhusu dhambi itawale mwili wako ili kusudi uweze kuzitii tamaa zake.
13 Usitoe sehemu za mwili wako katika dhambi kama vyombo visivyo na haki, bali jitoeni wenyewe kwa Mungu, kama walio hai kutoka mautini. Na zitoeni sehemu za miili yenu kama vyombo vya haki kwa Mungu.
14 Msiiruhusu dhambi iwatawale. Kwa kuwa hamko chini ya sheria, bali chini ya neema.
15 Nini basi? Tutende dhambi kwa kuwa hatupo chini ya sheria, bali chini ya neema? La hasha.
16 Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa wenyewe kama watumishi ndiye ambaye ninyi mnakuwa watumishi wake, yeye mnayepaswa kumtii? Hii ni kweli hata kama ninyi ni watumwa katika dhambi ambayo inapelekea mauti, au watumwa wa utii unaopelekea haki.
17 Lakini ashukuriwe Mungu! Kwa kuwa mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mmetii kutoka moyoni ile namna ya fundisho mliopewa.
18 Mmefanywa huru kutoka kwenye dhambi, na mmefanywa watumwa wa haki.
19 Ninazungumza kama mtu kwa sababu ya madhaifu ya miili yenu. Kwa maana kama vile mlivyotoa viungo vya miili yenu kuwa watumwa kwa uchafu na uovu, kwa jinsi iyo hiyo, sasa toeni viungo vya miili yenu kuwa watumwa wa haki kwa utakaso.
20 Kwa kuwa mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na haki.
21 Kwa wakati huo, mlikuwa na tunda lipi kwa mambo ambayo kwa sasa mnaona aibu kwayo? Kwa kuwa matokeo ya mambo hayo ni kifo.
22 Lakini kwa kuwa sasa mmefanywa huru mbali na dhambi na mmefanyika watumwa kwa Mungu, mna tunda kwa ajili ya utakaso. Tokeo ni uzima wa milele.
23 Kwa kuwa mshahara wa dhambi ni mauti, bali zawadi ya bure ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.