11
1 Ndipo Nahashi Mwamoni akaenda na kupiga kambi kuzunguka Yabeshi Gileadi. Watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, “Fanya mkataba nasi, na tutakutumikia,”
2 Nahashi Mwamoni akawajibu, “Kwa sharti hili nitafanya mkataba na ninyi, kwamba wote niwang'oe macho ya kulia, na kwa kitendo hiki kilete fedheha katika Israeli yote.”
3 Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, “Tuache kwa siku saba, ili tuwatume wajumbe katika nchi yote ya Israeli. Ndiposa, kama hakuna mtu wa kutuokoa, tutasalimu amri kwako.”
4 Nao wajumbe wakafika Gibea, alipoishi Sauli, na wakawaeleza watu kile kilichotokea. Watu wote wakalia kwa sauti kuu.
5 Na Sauli alikuwa akiwafuata nyuma maksai kutoka shambani. Sauli akauliza, “Watu wamepatwa na nini hadi wanalia?” Ndipo wakamweleza Sauli kile ambacho watu wa Yabeshi walikisema.
6 Sauli aliposikia kile walichosema, Roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, na akakasirika.
7 Akashika nira ya maksai, akawakata hao ng'ombe vipande vipande, na akavituma hivyo vipande katika nchi yote ya Israeli kwa kuwatumia wajumbe, Akasema, “Yeyote asiyejitokeza akimfuata Sauli na Samweli, hivi ndivyo ng'ombe wake watakavyofanywa.” Na hofu ya BWANA ikawaingia watu, na wakajitokeza wote kwa pamoja.
8 Alipowahesabu hapo Beseki, watu wa Israeli walikuwa elfu mia tatu, na watu wa Yuda elfu thelathini.
9 Wakawaambia wale wajumbe waliotumwa, “Mtawaambia watu wa Yabeshi Gileadi, 'Kesho, wakati wa jua kali, Mtaokolewa.”' Basi wale wajumbe wakaenda na kuwaambia watu wa Yabeshi, na watu wakafurahi.
10 Ndipo watu wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, “Kesho tutasalimu amri kwako, na utaweza kutufanyia chochote unachoona kinakupendeza.”
11 Siku iliyofuata Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu. Wakafika katikati ya Kambi wakati wa asubuhi, wakawashambulia na kuwashinda Waamoni ilipofika mchana. Waliosalimika nao walitawanyika, kiasi kwamba hata watu wawili hawakuachwa pamoja.
12 Ndipo watu wakamwambia Samweli, “Wako wapi waliosema, 'Hivi kweli Sauli atatutawala?' Walete watu hao, ili tuwauwe.”
13 Lakini Sauli akasema, “Hakuna atakayeuwawa siku ya leo, kwa sababu leo BWANA amemuokoa Isreli.”
14 Kisha Samweli akawaambia watu, “Njoni, twendeni Gilgali na tuimarishe ufalme tena huko.”
15 Hivyo watu wote wakaenda Gilgali na wakamsimika Sauli kuwa mfalme mbele za BWANA huko Gilgali. Na huko walitoa sadaka za amani mbele za BWANA, na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.