24
1 Sauli aliporudi kuwafukuza Wafilisti, akaambiwa kwamba, “Daudi yuko katika jangwa la Engedi.”
2 Ndipo Sauli akachukua watu elfu tatu waliochaguliwa kutoka Iraeli yote, wakaenda kumtafuta Daudi na watu wake katika miamba ya Mbuzi Mwitu.
3 Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, mahali palipokuwa na pango. Sauli akaingia ndani yake kujisaidia. Wakati huo Daudi na watu wake walikuwa wamekaa mbali zaidi ndani ya pango lilelile.
4 Watu wake Daudi wakamwambia, “Hii ndiyo siku ambayo BWANA aliisema akikuambia, 'Nitamweka adui wako mkononi mwako, ili umtendee kama unavyotaka.”' Kisha Daudi akainuka na kumnyemelea kwa mbele kimya kimya na kulikata pindo la kanzu ya Sauli.
5 Baadaye moyo wa Daudi ukamchoma kwa sababu alilikata pindo la kanzu ya Sauli.
6 Akawaambia watu wake, “BWANA anisamehe, sikupaswa kumtendea jambo hili bwana wangu, Mtiwa mafuta wa BWANA, kwa kunyoosha mkono wangu juu yake, maana yeye ni masihi wa BWANA.”
7 Hivyo Daudi akawakemea watu wake kwa maneno haya, na kuwazuia wasimpige Sauli. Sauli akasimama, akatoka pangoni, na kwenda zake.
8 Baadaye tena, Daudi akasimama juu, akatoka pangoni, na kumwita Sauli: “Bwana wangu mfalme.” Sauli alipotazama nyuma, Daudi akasujudu hadi chini na kuonyesha heshima.
9 Daudi akamwambia Sauli, “Kwa nini unawasikiliza watu ambao wanasema, “Angalia, Daudi anatafuta kukudhuru?'
10 Leo macho yako yameona jinsi BWANA alivyokuweka mkononi mwangu tulipokuwa ndani ya pango. Wengine waliniambia nikuuwe, lakini nilikuacha hai. Nikasema, 'Sitanyoosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa kuwa ni masihi wa BWANA.'
11 Tazama, baba yangu, angalia pindo la kanzu yako mkononi mwangu. Kwa maana kama nilikata pindo la kanzu yako na sikukuua, basi ujuwe na uone kwamba sina uovu au kosa katika mkono wangu, na sijafanya dhambi juu yako, ingawa unawinda kuutoa uhai wangu.
12 BWANA aamue kati yangu na wewe, na BWANA anilipizie kisasi juu yako, lakini mkono wangu kamwe hautakuwa juu yako.
13 Kama mithali ya wazee isemavyo, 'Katika waovu hutoka uovu.' Lakini mkono wangu hautakuwa juu yako.
14 Mfalme wa Israeli ametoka kumuandama nani? Unamsaka nani? Unasaka mzoga wa mbwa! Unasaka kiroboto!
15 BWANA na awe mwamuzi na atoe hukumu kati yangu na wewe, na akaione, na akatetee sababu yangu na aniruhusu kuepuka mkono wako.”
16 Daudi alipomaliza kuongea maneno haya kwa Sauli, Sauli akasema, “Hii ni sauti yako, mwanangu Daudi?” Sauli alinyanyua sauti yake akalia.
17 Akamwambia Daudi, “Wewe ni mwenye haki kuliko mimi. Kwa sababu umenilipa mazuri, wakati mimi nimekulipa maovu.
18 Leo umetangaza jinsi ulivyonitendea mazuri, kwa sababu hukuniua wakati BWANA aliponiweka katika rehema yako.
19 Kwa kuwa mtu akimpata adui yake, atamwacha aende zake salama? Na BWANA akuzawadie mema kwa kile ulichonifanyia leo.
20 Basi, najua kwa hakika kwamba utakuwa mfalme na kwamba ufalme wa Israeli utaimarika katika mkono wako.
21 Niapie kwa BWANA kwamba baada yangu hautawakatilia mbali uzao wangu, na kwamba hautaliharibu jina langu katika nyumba ya baba yangu.”
22 Hivyo Daudi akamwapia Sauli kiapo. Kisha Sauli akaenda nyumbani, lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.