30
1 Ikawa, Daudi na watu wake walipokuwa wamefika Ziklagi siku ya tatu, Waamaleki walifanya mashambulizi katika Negevu na Ziklagi. Waliupiga Ziklagi, wakauchoma moto mji,
2 na kuwachukua mateka wanawake na kila mmoja aliyekuwa ndani yake, mkubwa kwa mdogo. Wao hawakuua hata mmoja, lakini waliwachukua watu na kuondoka nao.
3 Daudi na watu wake walipofika kwenye mji, ulikuwa umechomwa moto - na wake zao, watoto wao wakiume na wakike walichukuliwa mateka.
4 Ndipo Daudi na watu aliokuwa nao wakapaza sauti zao na kulia hadi walipokuwa hawana nguvu zaidi za kulia.
5 Wake wawili wa Daudi walichukuliwa mateka, yaani Ahinoamu Myezreeli, na Abigaili aliyekuwa mke wa Nabali Mkarmeli.
6 Daudi aliguswa sana, maana watu walikuwa wanaongea kuhusu kumpiga mawe, kwa sababu roho za watu wote walihuzunika, kila mtu kwa ajili ya mtoto wake wakiume na wakike, lakini Daudi alijiimarisha katika BWANA, Mungu wake.
7 Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, “Tafadhali, niletee hapa ile naivera.”Abiathari akaileta hiyo naivera kwa Daudi.
8 Daudi akamwomba BWANA kwa ajili ya mwongozo, akisema, “Je, kama nikiliandama jeshi hili, nitalipata?” BWANA akamjibu, “Wafuate, maana kweli utawapata, na kwa hakika utarudisha kila kitu.”
9 Kwa hiyo Daudi akaenda, yeye na wale watu mia sita waliokuwa pamoja naye; nao wakafika katika kijito cha Bethori, mahali walipokaa wale walioachwa nyuma.
10 Lakini Daudi aliendelea kuwafuata, yeye na watu mia nne; maana wale mia mbili walibaki nyuma, wakiwa wamechoka kiasi cha kutoweza kuvuka kijito cha Besori.
11 Nao walimkuta Mmisri shambani na wakamleta kwa Daudi; wakampatia mkate, na akala; wakampa maji ya kunywa;
12 kisha walimpa kipande cha keki ya tini na vishada viwili vya zabibu. Alipomaliza kula, akapata nguvu tena, kwa kuwa alikuwa hajala mkate wala kunywa maji, siku tatu mchana na usiku.
13 Ndipo Daudi akamuuliza, “Wewe ni mtu wa nani? Je, unatoka wapi?” Naye akajibu, “Mimi ni kijana wa Misri, mtumishi wa Mwamaleki mmoja; bwana wangu aliniacha, kwa sababu siku tatu zilizopita nilikuwa mgonjwa.
14 Tulifanya mashambulizi dhidi ya Negevu ya Wakerethi, na iliyochini ya Yuda, na ile Negevu ya Kalebu, na kuichoma moto Ziklagi.”
15 Daudi akamwambia, “Je, utanipeleka hadi kwa jeshi lililofanya mashabulizi?” Huyo Mmisri akasema, “Uniapie kwa Mungu kwamba hautaniua au kunisaliti na kuniweka katika mikono ya bwana wangu, nami nitakupeleka liliko hilo jeshi.”
16 Yule Mmisri alipompeleka huko Daudi, hao wateka nyara walikuwa wametawanyika kila sehemu, wakila na kunywa, na wakicheza, kwa sababu ya nyara zote walizokuwa wamezitwaa kutoka nchi ya Wafilisti na kutoka nchi ya Yuda.
17 Daudi akawashambulia tangu jua lilipozama hadi jioni ya siku ya pili. Hakuna mtu aliyeponyoka isipokuwa vijana mia nne, waliopanda ngamia na kukimbia.
18 Daudi akarudisha vyote ambavyo Waamaleki walikuwa wamevichukua; na Daudi akawaokoa wake zake wawili.
19 Hakuna kilichopotea, si kidogo wala kikubwa, si watoto wa kiume wala wa kike, si mali iliyotekwa, wala chochote ambacho wavamizi alikichukuwa kwa ajili yao. Daudi akawa amerejesha kila kitu.
20 Akachukua makundi yote ya kondoo na ng'ombe, ambayo watu waliyatanguliza mbele ya ng'ombe wengine. Wakisema, “Hizi ni nyara za Daudi.”
21 Daudi akafika kwa wale watu mia mbili waliokuwa wamechoka kufuatana naye, wale walioachwa wakae katika kijito cha Besori. Watu hawa wakajitokeza kumlaki na watu waliokuwa naye.
22 Ndipo watu wote waovu na wasiofaa miongoni mwa waliokwenda na Daudi wakasema, “Kwa sababu watu hawa hawakwenda nasi, hatutawapa chochote kutoka katika nyara tulizorudisha. Isipokuwa kila mtu aweza kuchukuwa mke na watoto wake, wawatoe na kwenda zao.”
23 Ndipo Daudi akasema, “Ndugu zangu, msifanye hivyo, kwa vitu ambavyo BWANA ametupatia. Ametuhifadhi na kuwaweka mkononi mwetu wavamizi waliotuinukia.
24 Ni nani atawasikiliza kuhusu jambo hili? Kwa maana mgawo ni kwa yeyote aendae vitani, basi pia mgawo ni kwa yeyote aliyelinda mizigo; Nao watapata tena kilicho sawa.”
25 Ilikuwa hivyo tangu siku hiyo hadi leo, maana Daudi aliamua iwe sheria na amri kwa Israeli.
26 Daudi alipofika Ziklagi, alituma sehemu ya nyara kwa wazee wa Yuda, kwa rafiki zake, akisema, “Tazama, hii ni zawadi yenu kutokana na nyara za adui wa BWANA.”
27 Zawadi zilienda kwa wazee waliokuwa Bethueli, na kwa hao waliokuwa Ramothi iliyoko kusini, na kwa hao waliokuwa Yatiri,
28 na kwa hao waliokuwa Aroeri, na kwa hao waliokuwa Sifmothi, na kwa hao waliokuwa Eshtemoa
29 Pia kwa wazee waliokuwa Rakali, na kwa hao waliokuwa katika miji ya Wayerameeli, na kwa hao waliokuwa katika miji ya Wakeni,
30 na kwa hao waliokuwa Horma, na kwa hao waliokuwa Borashani, na kwa hao waliokuwa Athaki,
31 na kwa hao waliokuwa Hebroni, na kwa sehemu zote ambazo Daudi mwenyewe na watu wake walizoea kwenda.