4
1 Neno la Samweli likawafikia Israeli wote. Basi Israeli wakatoka kupigana dhidi ya Wafilisti. Nao wakaweka kambi hapo Ebenezeri, na Wafilisti waliweka kambi yao huko Afeki.
2 Nao Wafilisti walijipanga kwa ajili ya vita dhidi ya Waisraeli. Vita ilipopamba moto, Israeli ilishindwa na Wafilisti, wakauawa watu wapatao elfu nne kwenye uwanja wa vita.
3 Watu walipokuja kambini, wazee wa Israeli walisema, “Kwa nini BWANA ametushinda leo mbele ya Wafilisti? Hebu tulilete hapa sanduku la ushuhuda wa BWANA kutoka Shilo, ili kwamba liwe hapa pamoja nasi, ili litufanye tuwe salama kutokana na nguvu za maadui zetu.”
4 Hivyo waliwatuma watu huko Shilo; kutokea huko walilibeba sanduku la ushuhuda wa BWANA wa majeshi, akaaye juu ya makerubi. Hofni na Finehasi, watoto wawili wa Eli, walikuwapo pamoja na lile sanduku la ushuhuda wa Mungu.
5 Sanduku la ushuhuda wa BWANA lilipofika kambini, watu wote wa Israeli walipiga yowe, na nchi ikavuma.
6 Wafilisti waliposikia kelele za mayowe, wakasema, “sauti hii ya mayowe katika kambi ya Waebrania inamaanisha nini?” Baadaye walitambua kwamba sanduku la BWANA limefika kambini.
7 Wafilisti waliogopa sana, “Mungu ameingia kambini.” Wakasema, “Ole wetu! Jambo kama hili halijawahi kutokea huko nyuma!
8 Ole wetu! Ni nani atatulinda dhidi ya nguvu za Mungu mwenye uwezo? Huyu ndiye Mungu aliyewashambulia Wamisri kwa aina tofauti za mapigo mengi jangwani.
9 Enyi Wafilisti, iweni hodari, na fanyeni kiume, vinginevyo mtakuwa watumwa wa Waebrabia, kama walivyokuwa watumwa wenu. Fanyeni kiume, na piganeni nao.”
10 Wafilisti walipigana, na Waisraeli wakashindwa. Kila mtu alikimbilia nyumbani kwake, na mauaji yalikuwa makubwa sana; maana askari wa Israeli elfu thelathini waendao kwa miguu vitani, walianguka.
11 Lile sanduku la Mungu lilichukuliwa, na watoto wa Eli, Hofni na Finehasi waliuawa.
12 Mtu mmoja wa Benjamini alikimbia kutoka uwanja wa vita akaja Shilo siku iyo hiyo, aliwasili na mavazi yake yamechanika na matope kichwani pake.
13 Alipofika, Eli alikuwa amekaa kitini pake karibu na barabara akitazama kwa sababu moyo wake ulitetemeka kwa ajili ya sanduku la Mungu. Mtu yule alipoingia mjini na kutoa taarifa, mji wote ulilia.
14 Eli aliposikia kelele ya kilio kile, alisema, “Kilio hicho kina maana gani?” Kwa haraka mtu yule alikuja na kumweleza Eli.
15 Basi Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane; macho yake yamepofuka, na hakuweza kuona.
16 Yule mtu akamwambia Eli, “Mimi ndiye nimechomoka kutoka vitani. Nimetoroka kutoka kwenye mapigano leo.” Eli akasema, “Mambo yalienda namna gani, mwanangu?”
17 Yule mtu aliyeleta hizo habari alijibu na kusema, “Israeli wamewakimbia Wafilisti. Pia watu wengi wameuwawa. Watoto wako, Hofni na Finehasi, wamekufa, na sanduku la Mungu limechukuliwa.” .
18 Alipotamka sanduku la Mungu, Eli alianguka chali kutoka kwenye kiti chake karibu na mlango. akavunjika shingo lake, na kufariki, kwa sababu alikuwa mzee tena mzito. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka arobaini.
19 Basi mkwewe, mke wa Finihasi, alikuwa mjamzito akikaribia kujifungua. aliposikia habari kwamba sanduku la Mungu limetekwa nyara na kwamba baba mkwe na mme wake wamefariki, alichuchumaa chini akajifungua, lakini utungu wake ulimzidi na ulimtaabisha sana.
20 Alipokaribia kufariki, wanawake waliokuwa wakimhudumia walisema, “Usiogope, maana umejifungua mtoto wa kiume.” Lakini hakuwajibu lolote au kuzingatia alichoambiwa.
21 Akamwita mtoto Ikabodi, akisema, “Utukufu umetoweka Israeli!” Kwa sababu sanduku la Mungu limetekwa nyara, na kwa sababu ya kifo cha baba mkwe na mme wake.
22 Na alisema, “Utukufu umetoweka kutoka Israeli, kwa sababu sanduku la Mungu limetekwa nyala.”