8
1 Samweli alipozeeka, aliwaweka watoto wake wawe waamuzi juu ya Israeli.
2 Mtoto wake wa kwanza aliitwa Yoeli, na mtoto wake wa pili aliitwa Abiya. Hawa walikuwa waamuzi katika Bersheba.
3 Watoto wake hawakuenenda katika njia za baba yao, bali walipiga mbio kutafuta mapato ya udhalimu. Walipokea rushwa na na kupotosha hukumu.
4 Ndipo wazee wote wa Israeli walikutana pamoja na kumwendea Samweli huko Rama.
5 Wakamwambia, “Angalia, wewe umekuwa mzee, na watoto wako hawaenendi katika njia zako. Tuchagulie mfalme wakutuamua kama yalivyo mataifa yote.”
6 Lakini haikumpendeza Sameli waliposema, “Utupatie mfalme wa kutuamua.” Hivyo akamwomba BWANA.
7 Na BWANA akamwambia Samweli, “Sikiliza sauti ya watu kwa kila jambo wanalokwambia; kwa sababu hwajakukataa wewe, bali wamenikataa mimi nisiwe mfalme wao.
8 Sasa wanafanya kama vile walivyotenda tangu siku ile nilipowatoa huko Misri, kwa kuniacha, na kuwatumikia miungu mingine, na ndivyo hivyo pia wanakufanyia na wewe.
9 Basi sasa uwasikilize; lakini uwaonye sawasawa na uwafahamishe tabia ya mfalme atakaye waongoza.
10 Kwa hiyo Samweli akawaambia watu waliokuwa wakiomba mfalme maneno yote ya BWANA.
11 Akasema, “Hivi ndivyo jinsi mfalme atakavyowatawala.
12 Atawachukua watoto wenu wa kiume na kuwaweka juu ya magari ya vita na kuwa wapanda farasi wake, na kukimbia mbele ya magari yake. Atawaweka ma- kapteni wake juu ya maelfu ya askari, na ma-kapteni juu ya askari hamsini. Wengine atawafanya wakulima wamashamba yake, wengine wavunaji wa mazao yake, wengine watatengeneza silaha zake na zana za magari yake.
13 Naye atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi, na waoka mikate.
14 Atachukua mashamba yenu mazuri, mashamba ya mizabibu, na yale ya mizeituni na kuwapa watumishi wake.
15 Atachukua moja ya kumi ya nafaka zenu na mizabibu na na kuwapa maofisa na watumishi wake.
16 Atawachukua watumwa wenu na wajakazi wenu na vijana wenu waliowazuri na punda wenu; atawatumikisha wote kwa ajili yake.
17 Atawatoza moja ya kumi ya mifugo yenu, na mtakuwa watumwa wake.
18 Ndipo mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyemchagua kwa ajili yenu; lakini siku ile BWANA hatawajibu
19 Lakini watu walikataa kumsikiliza Samweli; wakasema, “Hapana!” Lazima awepo mfalme juu yetu.
20 Ili tuweze kuwa kama mataifa mengine yote, na hivyo mfalme wetu aweze kutuamua na atoke mbele yetu na atupiganie vita yetu.
21 Naye Samweli aliposikia maneno yote ya watu, akayarudia katika masiko ya BWANA.
22 BWANA akamwambia Samweli, “Sikiliza sauti yao na uwafanyie mfalme.” Hivyo Samweli akawaambia watu wa Israeli, “Kila mtu na arudi mjini kwake.”