6
Kisha nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa ile mihuri saba. Nikasikia kimoja cha vile viumbe hai vinne kikisema kwa sauti kama ya ngurumo, “Njoo!” Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe hapo. Na mpanda farasi wake alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka kama mshindi aendelee kushinda. Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe hai wa pili akisema, “Njoo!” Nami nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo, mwekundu. Mpanda farasi wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani duniani, watu wauane, akapewa upanga mkubwa. Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe hai wa tatu akisema, “Njoo!” Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mmoja hapo, mweusi. Mpanda farasi wake alikuwa na vipimo viwili vya kupimia uzito mkononi mwake. Nikasikia kitu kama sauti itokayo kwa vile viumbe hai vinne. Nayo ilisema, “Kibaba kimoja cha unga wa ngano wa kiasi cha fedha dinari moja, na vibaba vitatu vya shayiri kwa dinari moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!” Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa nne. Nikamsikia yule kiumbe hai wa nne akisema, “Njoo!” Nami nikatazama, na kumbe alikuwapo farasi mmoja hapo, rangi yake kijivu. Na jina la mpanda farasi wake lilikuwa kifo, na Kuzimu alimfuata nyuma. Hao walipewa mamlaka juu ya robo moja ya dunia, wawaue watu kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia. Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tano. Nikaona pale chini ya madhabahu ya kufukizia ubani roho za wale waliouawa kwa sababu ya ujumbe wa Mungu, na kwa sababu ya ushuhuda waliotoa. 10 Basi, wakalia kwa sauti kubwa: “Ee Bwana, uliye mtakatifu na mwaminifu, mpaka lini utakawia kulipiza kisasi kwa wakazi wote wa dunia kwa ajili ya kuuawa kwetu?” 11 Wakapewa kila mmoja vazi refu jeupe, wakaambiwa wazidi kusubiri kwa muda mfupi, mpaka itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu ambao watawaua kama wao wenyewe walivyouawa. 12 Kisha nikatazama, na wakati Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa sita, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi; jua likawa jeusi kama gunia; mwezi wote ukawa mwekundu kama damu; 13 nazo nyota za mbingu zikaanguka juu ya ardhi kama matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. 14 Anga likatoweka kama vile karatasi inavyokunjwakunjwa; milima yote na visima vyote vikaondolewa mahali pake. 15 Kisha wafalme wa duniani, wakuu, majemadari, matajiri, wenye nguvu, kila mtumwa na mtu huru, wakajificha mapangoni na kwenye majabali milimani. 16 Wakaiambia hiyo milima na hayo majabali, “Tuangukieni, mkatufiche mbali na yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na mbali na ghadhabu ya Mwanakondoo! 17 Maana siku maalum ya ghadhabu yao imefika. Nani awezaye kuikabili?”