18
Baada ya hayo, nilimwona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa na uwezo mkuu, na dunia ikamulikwa na mng'ao wake. Basi, akapaaza sauti kwa nguvu akisema, “Umeanguka; Babuloni mkuu umeanguka! Sasa umekuwa makao ya mashetani na pepo wachafu; umekuwa makao ya ndege wachafu na wa kuchukiza mno. Maana mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na anasa zake zisizo na kipimo.” Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema, “Watu wangu, ondokeni kwake, ili msishirikiane naye katika dhambi zake, msije mkaipata adhabu yake. Kwa maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno, zimelundikana mpaka mbinguni, na Mungu ameyakumbuka maovu yake. Mtendeeni kama alivyowatendea ninyi; mlipeni mara mbili kwa yale aliyoyatenda. Jazeni kikombe chake kwa kinywaji kikali mara mbili zaidi ya kile alichowapeni. Mpeni mateso na uchungu kadiri ya kujigamba kwake, na kuishi kwake kwa anasa. Maana anajisemea moyoni: Ninaketi hapa; mimi ni malkia. Mimi si mjane, wala sitapatwa na uchungu! Kwa sababu hiyo mabaa yake yatampata kwa siku moja: ugonjwa, huzuni na njaa. Atachomwa moto, maana Bwana Mungu mwenye kumhukumu ni Mwenye Uwezo.” Wafalme wa Dunia waliofanya uzinzi naye na kuishi naye maisha ya anasa wataomboleza na kulia wakati watakapoona moshi wa mji huo unaoteketea. 10 Wanasimama kwa mbali kwa sababu ya kuogopa mateso yake, na kusema, “Ole! Ole kwako Babuloni, mji maarufu na wenye nguvu! Kwa muda wa saa moja tu adhabu yako imekupata.” 11 Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumfanyia matanga, maana hakuna mtu anayenunua tena bidhaa zao; 12 hakuna tena wa kununua dhahabu yao, fedha, mawe ya thamani na lulu, kitani na nguo za rangi ya zambarau, hariri na nguo nyekundu; vyombo vya kila aina ya miti ya pekee, vyombo vya pembe za ndovu, vya miti ya thamani kubwa, vya shaba, chuma na marmari; 13 mdalasini, viungo, ubani, manemane, udi, divai, mafuta, unga na ngano, ng'ombe na kondoo, farasi na magari ya kukokotwa, watumwa wao na hata maisha ya watu. 14 Wafanyabiashara wanamwambia: “Faida yote uliyotazamia imetoweka, na utajiri na fahari vimekuponyoka; hutaweza kuvipata tena!” 15 Wafanya biashara waliotajirika kutokana na mji huo, watasimama mbali kwa sababu ya hofu ya mateso yake, watalalamika na kuomboleza, 16 wakisema, “Ole! Ole kwa mji huu mkuu. Ulizoea kuvalia nguo za kitani, za rangi ya zambarau na nyekundu, na kujipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu! 17 Kwa saa moja tu utajiri wako umetoweka!” Halafu manahodha wote na wasafiri wao, wanamaji na wote wanaofanya kazi baharini, walisimama kwa mbali, 18 na walipouona moshi wa moto ule uliouteketeza, wakalia kwa sauti: “Hakujapata kuwako mji kama mji huu mkuu!” 19 Wakajimwagia vumbi juu ya vichwa vyao wakilia kwa sauti na kuomboleza: “Ole! Ole kwako mji mkuu! Ni mji ambamo wote wenye meli zisafirizo baharini walitajirika kutokana na utajiri wake. Kwa muda wa saa moja tu umepoteza kila kitu!” 20 Furahi ee mbingu, kwa sababu ya uharibifu wake. Furahini watu wa Mungu, mitume na manabii! Kwa maana Mungu ameuhukumu kwa sababu ya mambo uliyowatenda ninyi! 21 Kisha malaika mmoja mwenye nguvu sana akainua jiwe mfano wa jiwe kubwa la kusagia, akalitupa baharini akisema, “Ndivyo, Babuloni atakavyotupwa na kupotea kabisa. 22 Sauti za vinubi za muziki, sauti za wapiga filimbi na tarumbeta hazitasikika tena ndani yako. Hakuna fundi wa namna yoyote ile atakayepatikana tena ndani yako; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikika tena ndani yako. 23 Mwanga wa taa hautaonekana tena ndani yako; sauti za bwana arusi na bibi arusi hazitasikika tena ndani yako. Wafanyabiashara wako walikuwa wakuu duniani, na kwa uchawi wako mataifa yote yalipotoshwa!” 24 Mji huo uliadhibiwa kwani humo mlipatikana damu ya manabii, damu ya watu wa Mungu na damu ya watu wote waliouawa duniani.