16
Changizo Kwa Ajili Ya Watakatifu
1 Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. 2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango. 3 Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu. 4 Kama ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.
Mahitaji Binafsi
5 Baada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia. 6 Huenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendapo. 7 Kwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu; natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana akipenda. 8 Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste, 9 kwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi wanaonipinga.
10 Ikiwa Timotheo atakuja kwenu, hakikisheni kwamba hana hofu yoyote akiwa nanyi, kwa sababu anafanya kazi ya Bwana, kama mimi nifanyavyo. 11 Basi asiwepo mtu atakayekataa kumpokea. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunijia tena. Namtarajia pamoja na ndugu.
12 Basi kwa habari za ndugu yetu Apolo, nimemsihi kwa bidii aje kwenu pamoja na hao ndugu. Ingawa alikuwa hapendi kabisa kuja sasa, lakini atakuja apatapo nafasi.
Maneno Ya Mwisho
13 Kesheni, simameni imara katika imani, fanyeni kiume, kuweni mashujaa kuweni hodari. 14 Fanyeni kila kitu katika upendo.
15 Ninyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio waliokuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi, 16 mjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii. 17 Nilifurahi wakati Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu. 18 Kwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa.
Salamu Za Mwisho
19 Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Prisila,*Prisila kwa Kiyunani ni Priska, hivyo tafsiri nyingine zimemuita Priska. pamoja na kanisa lililoko nyumbani kwao wanawasalimu sana katika Bwana. 20 Ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.
21 Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe.
22 Kama mtu yeyote hampendi Bwana Yesu Kristo, na alaaniwe. Bwana wetu, njoo.†Kwa Kiaramu ni Marana tha.
23 Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.
24 Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu. Amen.