2
Maagizo Ya Daudi Kwa Solomoni
Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Solomoni agizo.
Akasema, “Mimi ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jionyeshe kuwa mwanaume, shika lile Bwana Mungu wako analokuagiza: Enenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote uendako, ili kwamba Bwana aweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na kama wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’
“Sasa wewe mwenyewe unafahamu lile Yoabu mwana wa Seruya alilonitendea, lile alilofanya kwa majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua, akimwaga damu yao wakati wa amani kama vile ni kwenye vita, tena akaipaka damu ile kwenye mkanda uliokuwa kiunoni mwake na viatu alivyovaa miguuni mwake. Shughulika naye kwa kadiri ya hekima yako, lakini usiache kichwa chake chenye mvi kishukie kaburi kwa amani.
“Lakini uwaonyeshe wema wana wa Barzilai wa Gileadi na uwaruhusu wawe miongoni mwa wale walao mezani pako. Walisimama nami nilipomkimbia ndugu yako Absalomu.
“Ukumbuke, unaye Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini kutoka Bahurimu, ambaye alinilaani kwa laana kali siku niliyokwenda Mahanaimu. Aliposhuka kunilaki huko Yordani, nilimwapia kwa Bwana: ‘Sitakuua kwa upanga!’ Lakini sasa, usidhani kwamba hana hatia. Wewe ni mtu wa hekima, utajua la kumtendea. Zishushe mvi zake kaburini kwa damu.”
10 Kisha Daudi akapumzika pamoja na baba zake naye akazikwa katika Mji wa Daudi. 11 Daudi alikuwa ametawala juu ya Israeli miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu. 12 Kwa hiyo Solomoni akaketi katika kiti cha ufalme cha baba yake Daudi, nao utawala wake ukaimarika sana.
Kiti Cha Ufalme Cha Solomoni Chaimarishwa
13 Basi Adoniya, mwana wa Hagithi, akaenda kwa Bathsheba, mama yake Solomoni. Bathsheba akamuuliza, “Je, umekuja kwa amani?”
Akajibu, “Ndiyo, kwa amani.” 14 Kisha akaongeza, “Ninalo jambo la kukuambia.”
Akajibu, “Waweza kulisema.”
15 Akasema, “Kama unavyojua, ufalme ulikuwa wangu. Israeli wote waliniangalia mimi kama mfalme wao. Lakini mambo yalibadilika, ufalme umekwenda kwa ndugu yangu, kwa maana umemjia kutoka kwa Bwana. 16 Sasa ninalo ombi moja ninalokuomba. Usinikatalie.”
Bathsheba akasema, “Waweza kuliomba.”
17 Kwa hiyo akaendelea kusema, “Tafadhali mwombe Mfalme Solomoni, anipatie Abishagi, Mshunami, awe mke wangu; hatakukatalia wewe.”
18 Bathsheba akamjibu, “Vema sana, nitazungumza na mfalme kwa ajili yako.”
19 Bathsheba alipokwenda kwa Mfalme Solomoni kuzungumza naye kwa ajili ya Adoniya, mfalme alisimama kumlaki mama yake, akamwinamia na kuketi kwenye kiti chake cha ufalme. Akaamuru kiti cha ufalme kuletwa kwa ajili ya mama yake mfalme, naye akaketi mkono wake wa kuume.
20 Bathsheba akamwambia mfalme, “Ninalo ombi moja dogo la kukuomba; usinikatalie.”
Mfalme akajibu, “Omba, mama yangu; sitakukatalia.”
21 Akasema, “Mruhusu Abishagi, Mshunami, aolewe na ndugu yako Adoniya.”
22 Mfalme Solomoni akamjibu mama yake, “Kwa nini uombe Abishagi, Mshunami, kwa ajili ya Adoniya? Ungeweza pia kuomba ufalme kwa ajili yake, kwani yeye ni ndugu yangu mkubwa: naam, kwa ajili yake, na kwa kuhani Abiathari na Yoabu mwana wa Seruya!”
23 Mfalme Solomoni akaapa kwa Bwana, akasema: “Mungu na aniulie mbali, tena bila huruma, ikiwa Adoniya hatalipa kwa uhai wake kwa ajili ya ombi hili! 24 Basi sasa, hakika kama Bwana aishivyo, yeye ambaye ameniimarisha salama kwenye kiti cha ufalme cha Daudi baba yangu, naye amenipa ufalme wa kudumu kama alivyoahidi, Adoniya atauawa leo!” 25 Hivyo Mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adoniya akafa.
26 Mfalme akamwambia kuhani Abiathari, “Nenda huko Anathothi katika mashamba yako. Wewe unastahili kufa, lakini sitakuua sasa, kwa sababu ulilichukua Sanduku la Bwana Mwenyezi mbele ya Daudi baba yangu na ulishiriki taabu zote za baba yangu.” 27 Hivyo Solomoni akamwondoa Abiathari kwenye ukuhani wa Bwana, akilitimiza neno la Bwana alilokuwa amenena huko Shilo kuhusu nyumba ya Eli.
28 Habari zilipomfikia Yoabu, ambaye alikuwa amefanya shauri baya na Adoniya, lakini sio na Absalomu, alikimbilia kwenye hema la Bwana na kushika pembe za madhabahu. 29 Mfalme Solomoni akaambiwa kuwa Yoabu amekimbilia kwenye hema la Bwana naye alikuwa kando ya madhabahu. Basi Solomoni akamwagiza Benaya mwana wa Yehoyada: “Nenda ukamuue!”
30 Ndipo Benaya akaingia kwenye hema la Bwana na kumwambia Yoabu, “Mfalme anasema, ‘Toka nje!’ ”
Lakini akajibu, “La! Nitafia hapa hapa.”
Benaya akamwarifu mfalme, “Hivi ndivyo Yoabu alivyonijibu.”
31 Kisha mfalme akamwamuru Benaya, “Fanya kama asemavyo. Muue na kumzika, ili uniondolee mimi na nyumba ya baba yangu dhambi ya damu isiyokuwa na hatia ile Yoabu aliyoimwaga. 32  Bwana atamlipiza kwa ajili ya damu aliyoimwaga, kwa sababu pasipo Daudi baba yangu kujua, aliwashambulia watu wawili na kuwaua kwa upanga. Wote wawili, Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda, walikuwa watu wazuri na wanyofu kuliko yeye. 33 Hatia ya damu yao na iwe juu ya kichwa cha Yoabu na wazao wake milele. Lakini kwa Daudi na uzao wake, nyumba yake na kiti chake cha ufalme, iwepo amani ya Bwana milele.”
34 Basi Benaya mwana wa Yehoyada akakwea, akampiga na kumuua Yoabu, naye akazikwa katika nchi yake mwenyewe katika jangwa. 35 Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada juu ya jeshi kwenye nafasi ya Yoabu na kumweka kuhani Sadoki badala ya Abiathari.
36 Kisha mfalme akatuma ujumbe kwa Shimei na kumwambia, “Ujijengee nyumba huko Yerusalemu uishi huko, lakini usiende mahali pengine popote. 37 Siku utakayoondoka kuvuka Bonde la Kidroni, uwe na hakika utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.”
38 Shimei akamjibu mfalme, “Ulilolisema ni jema. Mtumishi wako atatenda kama bwana wangu mfalme alivyosema.” Naye Shimei akakaa Yerusalemu kwa muda mrefu.
39 Lakini baada ya miaka mitatu, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi, naye Shimei akaambiwa, “Watumwa wako wako Gathi.” 40 Kwa ajili ya hili, Shimei akatandika punda wake, akaenda kwa Akishi huko Gathi kuwatafuta watumwa wake. Basi Shimei akaondoka na kuwarudisha watumwa wake kutoka Gathi.
41 Solomoni alipoambiwa kuwa Shimei ametoka Yerusalemu na kwenda Gathi na amekwisha kurudi, 42 mfalme akamwita Shimei na kumwambia, “Je, sikukuapiza kwa Bwana na kukuonya kuwa, ‘Siku utakayoondoka kwenda mahali pengine popote, uwe na hakika utakufa?’ Wakati ule uliniambia, ‘Ulilolisema ni jema. Nitatii!’ 43 Kwa nini basi hukutunza kiapo chako kwa Bwana na kutii amri niliyokupa?”
44 Pia mfalme akamwambia Shimei, “Unajua katika moyo wako makosa uliyomtendea baba yangu Daudi. Sasa Bwana atakulipiza kwa ajili ya mabaya yako uliyotenda. 45 Lakini Mfalme Solomoni atabarikiwa, na kiti cha ufalme cha Daudi kitakuwa imara mbele za Bwana milele.”
46 Kisha mfalme akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka nje, akampiga Shimei na kumuua.
Sasa ufalme ukawa umeimarika kikamilifu mikononi mwa Solomoni.