5
Kulichunga Kundi La Mungu
Kwa wazee waliomo miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo, na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa: lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe; si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali kuweni vielelezo kwa hilo kundi. Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtapokea taji ya utukufu isiyoharibika.
Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa,
“Mungu huwapinga wenye kiburi,
lakini huwapa wanyenyekevu neema.”
Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.
Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.
10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha. 11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.
Salamu Za Mwisho
12 Kwa msaada wa Silvano,* Yaani Sila. ambaye ninamhesabu kuwa ndugu mwaminifu, nimewaandikia waraka huu mfupi ili kuwatia moyo, na kushuhudia kwamba hii ni neema halisi ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.
13 Kanisa lililoko Babeli, lililochaguliwa pamoja nanyi, wanawasalimu; vivyo hivyo mwanangu Marko anawasalimu. 14 Salimianeni kwa busu la upendo.
Amani iwe nanyi nyote mlio katika Kristo.

*5:12 Yaani Sila.