10
Ndipo Samweli akachukua chupa ndogo ya mafuta na kuyamimina juu ya kichwa cha Sauli, akambusu, akisema, “Je, Bwana hakukutia mafuta uwe kiongozi juu ya watu wake Israeli? Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli, huko Selsa kwenye mpaka wa Benyamini. Watakuambia, ‘Punda wale uliotoka kwenda kuwatafuta, wamekwisha kupatikana. Sasa baba yako ameacha kufikiri kuhusu punda na sasa ana hofu kukuhusu wewe. Anauliza, “Nitafanyaje kuhusu mwanangu?” ’
“Kisha utakwenda mbele kutoka hapa mpaka uufikie mwaloni wa Tabori. Watu watatu wanaopanda kwa Mungu huko Betheli watakutana nawe hapo. Mmoja atakuwa amechukua wana-mbuzi watatu, mwingine mikate mitatu, na mwingine kiriba cha divai. Watakusalimu na kukupa mikate miwili, ambayo utaipokea kutoka kwao.
“Baada ya hayo utakwenda Gibea ya Mungu, ambapo hapo kuna kambi ya Wafilisti. Unapokaribia mji utakutana na kundi la manabii wakiteremka kutoka mahali pa juu wakiwa na vinubi, matari, filimbi na zeze vikipigwa mbele yao, nao watakuwa wakitoa unabii. Roho wa Bwana atakuja juu yako kwa nguvu, nawe utatoa unabii pamoja nao; nawe utageuzwa kuwa mtu wa tofauti. Mara ishara hizi zitakapotimizwa, fanya lolote mkono wako upasao kufanya, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.
“Tangulia kushuka mbele yangu mpaka Gilgali. Hakika nami nitateremka nikujie ili kutoa dhabihu za sadaka za kuteketezwa na dhabihu za amani, lakini lazima ungoje kwa siku saba hata nitakapokujia na kukuambia likupasalo kufanya.”
Sauli Afanywa Mfalme
Ikawa Sauli alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu aliubadilisha moyo wa Sauli, na ishara hizi zote zikatimizwa siku ile. 10 Walipofika Gibea, akakutana na kundi la manabii. Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akajiunga nao katika kutoa unabii kwao. 11 Ikawa wale wote waliomfahamu hapo mwanzo walipomwona akitoa unabii pamoja na manabii, wakaulizana, “Ni nini hiki kilichomtokea mwana wa Kishi? Je, Sauli naye pia yumo miongoni mwa manabii?”
12 Mtu mmoja ambaye aliishi huko akajibu, “Je, naye baba yao ni nani?” Basi ikawa mithali, kusema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?” 13 Baada ya Sauli kumaliza kutoa unabii, alikwenda mahali pa juu.
14 Basi babaye mdogo akamuuliza Sauli na mtumishi wake, “Je, mlikuwa wapi?”
Akajibu, “Tulikuwa tukiwatafuta punda. Lakini tulipoona hawapatikani, tulikwenda kwa Samweli.”
15 Babaye mdogo Sauli akasema, “Niambie Samweli amekuambia nini.”
16 Sauli akajibu, “Alituhakikishia kwamba punda wamepatikana.” Lakini hakumwambia babaye mdogo kila kitu Samweli alichomwambia kuhusu ufalme.
17 Samweli akawaita watu wa Israeli kuja kwa Bwana huko Mispa, 18 naye akawaambia, “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Niliwatoa Israeli kutoka Misri, nami niliwaokoa toka nguvu za Misri na falme zote zilizowaonea.’ 19 Lakini sasa mmemkataa Mungu wenu, ambaye anawaokoa toka katika maafa yenu yote na taabu zenu zote. Nanyi mmesema, ‘Hapana, tuteulie mfalme atutawale.’ Sasa basi, jihudhurisheni wenyewe mbele za Bwana kwa kabila zenu na kwa koo zenu.”
20 Samweli alipoyasogeza makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachaguliwa. 21 Kisha akalisogeza mbele kabila la Benyamini, ukoo kwa ukoo, nao ukoo wa Matri ukachaguliwa. Mwishoni Sauli mwana wa Kishi akachaguliwa. Lakini walipomtafuta, hakuonekana. 22 Wakazidi kuuliza kwa Bwana, “Je, huyo mtu amekwisha kufika hapa?”
Naye Bwana akasema, “Ndiyo, amejificha katikati ya mizigo.”
23 Wakakimbia na kumleta kutoka huko, naye aliposimama katikati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote. 24 Samweli akawaambia watu wote, “Je, mnamwona mtu ambaye Bwana amemchagua? Hayupo aliye kama yeye miongoni mwa watu wote.”
Ndipo watu wakapiga kelele, wakasema, “Mfalme na aishi maisha marefu.”
25 Samweli akawaeleza watu madaraka ya ufalme. Akayaandika kwenye kitabu na kuweka mbele za Bwana. Kisha Samweli akawaruhusu watu, kila mmoja aende nyumbani kwake.
26 Sauli pia akaenda nyumbani kwake huko Gibea, akisindikizwa na watu hodari ambao Mungu alikuwa amegusa mioyo yao. 27 Lakini baadhi ya watu wakorofi walisema, “Huyu mtu atawezaje kutuokoa?” Wakamdharau na wala hawakumletea zawadi. Lakini Sauli akanyamaza kimya.