26
Daudi Amwacha Sauli Hai Tena
Hao Wazifu wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kinachotazamana na Yeshimoni?”
Hivyo Sauli akashuka kwenda katika Jangwa la Zifu, akiwa na watu wake 3,000 wa Israeli waliochaguliwa, kumsaka Daudi huko. Sauli akapiga kambi yake kando ya barabara juu ya kilima cha Hakila kinachotazamana na Yeshimoni, lakini Daudi alikuwa anaishi huko jangwani. Alipoona kuwa Sauli amemfuata huko, Daudi akatuma wapelelezi na akapata habari kwa hakika kwamba Sauli alikuwa amewasili.
Ndipo Daudi akaondoka, akaenda hadi mahali Sauli alikuwa amepiga kambi. Akaona mahali Sauli na Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi, walipokuwa wamelala. Sauli alikuwa amelala ndani ya kambi, jeshi likiwa limemzunguka.
Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?”
Abishai akajibu, “Nitakwenda pamoja nawe.”
Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli.
Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome mpaka ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.”
Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa Bwana na asiwe na hatia?” 10 Daudi akasema, “Hakika kama vile Bwana aishivyo, Bwana mwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au atakwenda vitani na kuangamia. 11 Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta wa Bwana. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.”
12 Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababu Bwana alikuwa amewatia kwenye usingizi mzito.
13 Kisha Daudi akavuka upande mwingine na kusimama juu ya kilima mahali palipokuwa na nafasi pana kati yao. 14 Daudi akalipigia kelele jeshi na Abneri mwana wa Neri, akisema, “Je, Abneri, hutanijibu?”
Abneri akajibu, “Nani wewe umwitaye mfalme?”
15 Daudi akasema, “Wewe si ni mtu shujaa? Ni nani aliye kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukumlinda mfalme bwana wako? Mtu mmoja alikuja kumwangamiza mfalme, bwana wako. 16 Ulichokifanya si kizuri. Kwa hakika kama aishivyo Bwana, wewe na watu wako mnastahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, mpakwa mafuta wa Bwana. Tazameni hapo mlipo. Uko wapi mkuki wa mfalme na gudulia la maji ambavyo vilikuwa karibu na kichwa chake?”
17 Sauli akatambua sauti ya Daudi, na kusema, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?”
Daudi akajibu, “Naam, hiyo ndiyo, bwana wangu mfalme.” 18 Pia akaongeza, “Kwa nini bwana wangu anamfuatia mtumishi wake? Nimefanya nini, nalo kosa langu ni lipi nililolifanya niwe na hatia? 19 Sasa mfalme bwana wangu na asikilize maneno ya mtumishi wake. Kama Bwana amekuchochea dhidi yangu, basi yeye na aipokee sadaka yangu. Lakini hata hivyo, kama ni wanadamu waliofanya hivyo, walaaniwe mbele za Bwana! Wao sasa wamenifukuza kutoka sehemu yangu katika urithi wa Bwana wangu wakisema, ‘Nenda ukatumikie miungu mingine.’ 20 Basi usiache damu yangu imwagike kwenye ardhi mbali na uso wa Bwana. Mfalme wa Israeli ametoka kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware katika milima.”
21 Ndipo Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Rudi, Daudi mwanangu. Kwa kuwa uliyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani leo, sitajaribu kukudhuru tena. Hakika nimetenda kama mpumbavu na nimekosa sana.”
22 Daudi akajibu, “Mkuki wa mfalme uko hapa. Mmoja wa vijana wako na avuke kuuchukua. 23 Bwana humlipa kila mtu kwa ajili ya haki yake na uaminifu wake. Bwana alikutia katika mikono yangu leo, lakini sikuinua mkono wangu juu ya mpakwa mafuta wa Bwana. 24 Kwa hakika kama vile maisha yako yalivyokuwa ya thamani kwangu leo, vivyo hivyo maisha yangu na yawe na thamani kwa Bwana na kuniokoa kutoka taabu zote.”
25 Ndipo Sauli akamwambia Daudi, “Mwanangu Daudi na ubarikiwe; utafanya mambo makubwa na hakika utashinda.”
Basi Daudi akaenda zake, naye Sauli akarudi nyumbani.