5
Kuweni Tayari Kwa Siku Ya Bwana
Basi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia, kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajapo usiku. Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka.
Bali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi. Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku. Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi. Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku. Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo. Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. 10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye. 11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.
Maagizo Ya Mwisho, Salamu Na Kuwatakia Heri
12 Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya. 13 Waheshimuni sana katika upendo kwa ajili ya kazi zao. Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi. 14 Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni walio wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na kuwavumilia watu wote. 15 Angalieni kuwa mtu asimlipe mwenzake maovu kwa maovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.
16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.
19 Msiuzime moto wa Roho Mtakatifu; 20 msiyadharau maneno ya unabii. 21 Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema. 22 Jiepusheni na uovu wa kila namna.
23 Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Yesu Kristo. 24 Yeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo.
25 Ndugu, tuombeeni. 26 Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu. 27 Nawaagizeni mbele za Bwana mhakikishe kuwa ndugu wote wanasomewa barua hii.
28 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amen.