20
1 Ikawa baada ya jambo hili, Wamoabu na Waamoni, pamoja na baadhi ya Wameuni wakaja ili wapigane vita na Yehoshafati.
2 Watu fulani wakaja wakamwambia Yehoshafati, “Jeshi kubwa linakuja dhidi yako kutoka Edomu tokea ngʼambo ile nyingine ya Bahari.*Yaani Bahari ya Chumvi. Tayari liko Hasason-Tamari” (yaani En-Gedi). 3 Yehoshafati akaogopa, akaazimu kumtafuta Bwana, na akatangaza kwa Yuda wote kufunga. 4 Watu wa Yuda wakakusanyika pamoja ili kutafuta msaada kutoka kwa Bwana. Wakaja kutoka kila mji wa Yuda ili kumtafuta.
5 Kisha Yehoshafati akasimama katika kusanyiko la Yuda na Yerusalemu katika Hekalu la Bwana, mbele ya ua mpya, 6 akasema:
“Ee Bwana, Mungu wa baba zetu, si wewe ndiwe uliye Mungu mbinguni? Si wewe ndiwe utawalaye juu ya falme zote za mataifa? Uweza na nguvu viko mkononi mwako, wala hakuna yeyote awezaye kushindana nawe. 7 Je, si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Abrahamu, rafiki yako, hata milele? 8 Wameishi ndani yake na humo wamekujengea mahali patakatifu kwa ajili ya Jina lako, wakisema: 9 ‘Kama maafa yakitujia, ikiwa ni upanga, hukumu, tauni, au njaa, tutasimama mbele zako, mbele ya Hekalu hili ambalo limeitwa kwa Jina lako na kukulilia katika shida yetu, nawe utatusikia na kutuokoa.’
10 “Lakini sasa hawa watu wa kutoka Amoni, Moabu na Mlima Seiri, ambao hukuwaruhusu Israeli wazivamie nchi zao wakati walitoka Misri, hivyo wakageukia mbali nao na hawakuwaangamiza, 11 tazama jinsi wanavyotulipa kwa kuja kututupa nje ya milki uliyotupa sisi kuwa urithi. 12 Ee Mungu wetu, je, wewe hutawahukumu? Kwa kuwa sisi hatuna uwezo wa kukabiliana na jeshi hili kubwa linalokuja kutushambulia. Sisi hatujui la kufanya, bali macho yetu yanakutazama wewe.”
13 Watu wote wa Yuda pamoja na wake zao, watoto wao na wadogo wao wakasimama pale mbele za Bwana.
14 Ndipo Roho wa Bwana akaja juu ya mtu mmoja jina lake Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, Mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi mzao wa Asafu alipokuwa amesimama katika kusanyiko.
15 Akasema: “Sikilizeni, enyi Yuda wote nanyi nyote mkaao Yerusalemu, nawe Mfalme Yehoshafati! Hili ndilo Bwana asemalo kwenu, ‘Msiogope wala msifadhaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Kwa maana vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu. 16 Kesho shukeni kukabiliana nao. Watakwea kwa kupandia Genge la Sisi, nanyi mtawakuta mwisho wa bonde, kabla ya Jangwa la Yerueli. 17 Hamtahitaji kupigana vita hivi. Kaeni kwenye nafasi zenu, simameni imara na mkaone wokovu Bwana atakaowapatia, enyi Yuda na Yerusalemu. Msiogope, wala msifadhaike. Kesho tokeni mwende mkawakabili, naye Bwana atakuwa pamoja nanyi.’ ”
18 Yehoshafati akainamisha uso wake chini, nao watu wote wa Yuda na Yerusalemu wakaanguka chini ili kuabudu mbele za Bwana. 19 Ndipo baadhi ya Walawi kutoka kwa Wakohathi na kwa wana wa Kora wakasimama na kumsifu Bwana, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana.
20 Asubuhi na mapema wakaondoka kuelekea Jangwa la Tekoa. Walipoanza safari, Yehoshafati akasimama akasema, “Nisikilizeni, enyi Yuda, na watu wa Yerusalemu! Mwaminini Bwana Mungu wenu, hivyo mtathibitika, wasadikini manabii wake nanyi mtafanikiwa. 21 Alipomaliza kushauriana na watu, Yehoshafati akawaweka watu wa kumwimbia Bwana na kumsifu katika utukufu wa utakatifu wake walipokuwa wametangulia mbele ya jeshi, wakisema:
“Mshukuruni Bwana
kwa kuwa upendo wake wadumu milele.”
22 Walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka waviziao dhidi ya watu wa Amoni, Moabu na wale wa Mlima Seiri waliokuwa wamekuja kuishambulia Yuda, nao wakashindwa. 23 Watu wa Amoni na Moabu wakawainukia watu wa Mlima Seiri ili kuwaua na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kumaliza kuwachinja watu wa Seiri, wakaangamizana wao kwa wao.
24 Yuda walipofika katika mnara wa ulinzi wa jangwani, wakaliangalia lile jeshi kubwa, wakaona ni maiti tupu zimetapakaa ardhini, wala hakuna yeyote aliyenusurika. 25 Hivyo Yehoshafati na watu wake wakaenda kujitwalia nyara kutoka kwao, nao wakakuta humo wingi wa mifugo, mali, nguo na vitu vya thamani, ambavyo vilikuwa vingi zaidi ya vile walivyoweza kuchukua. Wakakusanya nyara kwa siku tatu kwa sababu zilikuwa nyingi mno. 26 Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Beraka†Bonde la Beraka maana yake Bonde la Kusifu. kwa maana huko ndiko walikomsifu Bwana. Ndiyo sababu linaitwa Bonde la Beraka mpaka leo.
27 Kisha watu wote wa Yuda na Yerusalemu, wakiongozwa na Yehoshafati, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kwa kuwa Bwana alikuwa amewasababisha wafurahi juu ya adui zao. 28 Wakaingia Yerusalemu na kwenda hekaluni mwa Bwana wakiwa na vinubi, zeze na tarumbeta.
29 Hofu ya Mungu ikazipata falme zote za nchi waliposikia jinsi Bwana alivyokuwa amepigana dhidi ya adui za Israeli. 30 Ufalme wa Yehoshafati ukawa na amani, kwa kuwa Mungu wake alikuwa amemstarehesha pande zote.
Mwisho Wa Utawala Wa Yehoshafati
(1 Wafalme 22:41-50)
31 Hivyo Yehoshafati akatawala Yuda. Alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala, akatawala katika Yerusalemu kwa miaka ishirini na mitano. Mama yake aliitwa Azuba binti Shilhi. 32 Alienenda katika njia za Asa baba yake wala hakwenda kinyume chake. Alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana. 33 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa, na watu wakawa bado hawajaelekeza mioyo yao kwa Mungu wa baba zao.
34 Matukio mengine ya utawala wa Yehoshafati, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha Yehu mwana wa Hanani, ambazo zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli.
35 Hatimaye Yehoshafati mfalme wa Yuda akafanya urafiki na Ahazia mfalme wa Israeli ambaye alifanya maovu sana. 36 Akaungana naye kutengeneza meli nyingi za kwenda Tarshishi,‡Au: za biashara (ona pia 1Fal 10:22; 22:48; 2Nya 9:21; Isa 2:16; 60:9). nazo zilitengenezwa huko Esion-Geberi. 37 Ndipo Eliezeri mwana wa Dodavahu wa Maresha akatoa unabii dhidi ya Yehoshafati, akasema, “Kwa kuwa umeungana na Ahazia, Bwana ataangamiza vile mlivyotengeneza.” Zile meli zikavunjika na hazikuweza kungʼoa nanga ili kwenda Tarshishi.