12
Yoashi Anakarabati Hekalu
1 Katika mwaka wa saba wa utawala wa Yehu, Yoashi alianza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka arobaini. Jina la mama yake aliitwa Sibia, kutoka Beer-Sheba. 2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana miaka yote ambayo Yehoyada kuhani alikuwa akimwelekeza. 3 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
4 Yoashi akawaambia makuhani, “Kusanyeni fedha zote ambazo zitaletwa kama sadaka takatifu kwenye Hekalu la Bwana, yaani fedha zilizokusanywa kama kodi, fedha zilizopokelewa kutokana na nadhiri za watu binafsi, na fedha zilizoletwa kwa hiari hekaluni. 5 Kila kuhani na apokee fedha kutoka kwa mmoja wa watunza hazina, nazo zitumike kukarabati uharibifu wowote unaoonekana katika Hekalu.”
6 Lakini ikawa kufikia mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake Mfalme Yoashi, makuhani walikuwa bado hawajalikarabati Hekalu. 7 Kwa hiyo Mfalme Yoashi akamwita Yehoyada kuhani na makuhani wengine, akawauliza, “Kwa nini hamtengenezi uharibifu uliofanyika hekaluni? Msichukue fedha zaidi kutoka kwa watunza hazina wenu kwa ajili ya matumizi yenu, lakini kuanzia sasa ni lazima fedha yote itumike kwa ajili ya kukarabati Hekalu.” 8 Makuhani wakakubali kuwa hawatakusanya tena fedha kutoka kwa watu na kwamba hawatakarabati Hekalu wenyewe.
9 Yehoyada kuhani akachukua kisanduku na akatoboa tundu kwenye kifuniko chake. Akakiweka kando ya madhabahu upande wa kulia unapoingia hekaluni mwa Bwana. Makuhani waliolinda ingilio wakaweka ndani ya kisanduku fedha zote ambazo zililetwa katika Hekalu la Bwana. 10 Kila mara walipoona kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha ndani ya kisanduku, mwandishi wa mfalme na kuhani mkuu walikuja, wakazihesabu fedha hizo zilizoletwa katika Hekalu la Bwana, na kuziweka katika mifuko. 11 Wakiisha kuthibitisha kiasi cha hizo fedha, waliwapa watu walioteuliwa kusimamia kazi katika Hekalu. Kwa fedha hizo, wakawalipa wale watu waliofanya kazi katika Hekalu la Bwana: yaani, maseremala na wajenzi, 12 waashi na wakata mawe. Walinunua mbao na mawe ya kuchongwa kwa ajili ya ukarabati wa Hekalu la Bwana, na kulipia gharama nyingine zote za kulitengeneza.
13 Fedha zilizoletwa kwenye Hekalu hazikutumiwa kutengenezea masinia ya fedha, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, tarumbeta wala vyombo vingine vyovyote vya dhahabu au fedha kwa ajili ya Hekalu la Bwana; 14 zililipwa kwa wafanyakazi, ambao walizitumia kwa kukarabati Hekalu. 15 Wao hawakudai kupewa hesabu ya fedha kutoka kwa wale waliowapa ili kuwalipa wafanyakazi, kwa sababu walifanya kwa uaminifu wote. 16 Fedha zilizopatikana kutokana na sadaka za hatia na sadaka za dhambi hazikuletwa katika Hekalu la Bwana; zilikuwa mali ya makuhani.
17 Wakati huu Hazaeli mfalme wa Aramu akapanda kuishambulia Gathi, akaiteka. Kisha akageuka ili kuishambulia Yerusalemu. 18 Lakini Yoashi mfalme wa Yuda akavichukua vyombo vyote vitakatifu vilivyowekwa wakfu na baba zake, yaani Yehoshafati, Yehoramu na Ahazia, wafalme wa Yuda, zawadi ambazo yeye mwenyewe alikuwa ameziweka wakfu pamoja na dhahabu yote iliyokutwa katika hazina za Hekalu la Bwana na katika jumba la kifalme, akazipeleka kwa Hazaeli mfalme wa Aramu, ambaye hatimaye aliondoka Yerusalemu.
19 Kwa matukio mengine ya utawala wa Yoashi na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 20 Maafisa wake wakafanya shauri baya dhidi yake, nao wakamuulia Yoashi huko Beth-Milo, kwenye barabara iteremkayo kuelekea Sila. 21 Maafisa waliomuua walikuwa Yozabadi mwana wa Shimeathi, na Yehozabadi mwana wa Shomeri. Akafa na akazikwa pamoja na baba zake katika Mji wa Daudi. Naye Amazia mwanawe akawa mfalme baada yake.