21
Manase Mfalme Wa Yuda
(2 Nyakati 33:1-20)
Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na mitano. Mama yake aliitwa Hefsiba. Akafanya maovu machoni pa Bwana, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo Bwana aliyafukuza mbele ya Waisraeli. Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia miungu ambapo Hezekia baba yake alikuwa amepabomoa. Pia akasimamisha madhabahu za Baali na kutengeneza nguzo ya Ashera, kama Ahabu mfalme wa Israeli alivyofanya. Akalisujudia jeshi lote la angani na kuliabudu. Akajenga madhabahu katika Hekalu la Bwana, ambamo Bwana alikuwa amesema, “Katika Yerusalemu nitaliweka Jina langu.” Katika nyua zote mbili za Hekalu la Bwana, akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani. Akamtoa kafara mwanawe mwenyewe katika moto, akafanya uchawi na uaguzi, na akataka shauri kwa wapiga ramli na kwa mizimu. Akafanya maovu mengi sana machoni mwa Bwana na kumghadhibisha.
Akachukua nguzo ya Ashera aliyoichonga na kuiweka katika Hekalu, ambalo Bwana alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Solomoni, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu niliouchagua kutoka kabila zote za Israeli, nitaliweka Jina langu milele. Sitaifanya tena miguu ya Waisraeli itangetange kutoka nchi niliyowapa baba zao, ikiwa watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru, na kuishika Sheria yote ambayo walipewa na Mose mtumishi wangu.” Lakini hawa watu hawakusikiliza. Manase akawapotosha, hivyo kwamba walifanya maovu mengi kuliko mataifa ambayo Bwana aliyaangamiza mbele ya Waisraeli.
10 Bwana akasema kupitia watumishi wake manabii: 11 “Manase mfalme wa Yuda ametenda dhambi hizi za kuchukiza. Amefanya maovu mengi kuliko Waamori waliokuwepo kabla yake, na ameiongoza Yuda katika dhambi kwa sanamu zake. 12 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nitaleta maafa makubwa juu ya Yerusalemu na Yuda, kiasi kwamba masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yatawasha. 13 Nitanyoosha juu ya Yerusalemu kamba ya kupimia iliyotumika dhidi ya Samaria, na timazi iliyotumika dhidi ya nyumba ya Ahabu. Nitaifutilia mbali Yerusalemu kama mtu afutaye sahani, nikiifuta na kuifunikiza. 14 Nitawakataa mabaki wa urithi wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao. Watapokonywa mali zao na kutekwa nyara na adui zao wote, 15 kwa sababu wametenda uovu machoni pangu na kunighadhibisha tangu siku baba zao walipotoka Misri mpaka siku ya leo.”
16 Zaidi ya hayo, Manase pia alimwaga damu nyingi isiyo na hatia, hivi kwamba aliijaza Yerusalemu kutoka mwanzo hadi mwisho, mbali na dhambi ambayo alikuwa amesababisha Yuda kufanya, na hivyo wakatenda maovu machoni pa Bwana.
17 Matukio mengine ya utawala wa Manase, na yote aliyoyafanya, pamoja na dhambi alizotenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 18 Manase akalala pamoja na baba zake na akazikwa katika bustani ya jumba lake la kifalme, katika bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
Amoni Mfalme Wa Yuda
(2 Nyakati 33:21-25)
19 Amoni alikuwa na miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili. Mamaye aliitwa Meshulemethi binti Haruzi, kutoka Yotba. 20 Akatenda maovu machoni mwa Bwana, kama baba yake Manase alivyofanya. 21 Akaenenda katika njia zote za baba yake, akaabudu sanamu ambazo baba yake aliziabudu na kuzisujudia. 22 Akamwacha Bwana, Mungu wa baba zake, wala hakuenenda katika njia za Bwana.
23 Watumishi wa Amoni wakafanya fitina juu yake, nao wakamuulia kwake nyumbani. 24 Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamefanya hila dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake.
25 Matukio mengine ya utawala wa Amoni na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 26 Akazikwa kwenye kaburi lake katika bustani ya Uza. Naye Yosia mwanawe akawa mfalme baada yake.