23
Yosia Analifanya Upya Agano
(2 Nyakati 34:3-7, 29-33)
Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. Akapanda kwenda hekaluni mwa Bwana pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na manabii, watu wote wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, ambacho kilikuwa kimepatikana katika Hekalu la Bwana. Mfalme akasimama karibu na nguzo, na kufanya upya agano mbele za Bwana: yaani kumfuata Bwana na kuzishika amri zake, maagizo na sheria kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, hivyo kuyathibitisha maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kisha watu wote wakajifunga wenyewe kwa kiapo katika agano.
Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani waliomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka kwenye Hekalu la Bwana vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni, na kuyachukua hayo majivu mpaka Betheli. Akawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani. Akaiondoa nguzo ya Ashera kutoka kwenye Hekalu la Bwana, na kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu, akaiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wa kawaida. Akabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada za miungu, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Bwana na mahali wanawake walipofuma kwa ajili ya Ashera.
Yosia akawaleta makuhani wote wa Bwana kutoka miji yote ya Yuda, na kunajisi mahali pa juu pa kuabudia miungu, kuanzia Geba hadi Beer-Sheba, mahali pote ambapo hao makuhani wa miungu walifukiza uvumba. Akabomoa mahali pa kuwekea vitu vya ibada za miungu palipokuwa katika malango, kwenye ingilio la Lango la Yoshua, mtawala wa mji, lililoko upande wa kushoto wa lango la mji. Ingawa makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia miungu hawakuhudumu katika madhabahu ya Bwana katika Yerusalemu, walikula mikate isiyotiwa chachu miongoni mwa ndugu zao.
10 Kisha mfalme akanajisi Tofethi, palipokuwa katika Bonde la Ben-Hinomu, ili mtu yeyote asiweze kupatumia kumtoa kafara mwanawe au binti yake katika moto kwa mungu Moleki. 11 Akaondoa kutoka kwenye ingilio la Hekalu la Bwana wale farasi ambao wafalme wa Yuda walikuwa wamewaweka wakfu kwa ajili ya jua. Walikuwa kwenye ua karibu na chumba cha afisa aliyeitwa Nathan-Meleki. Basi Yosia akayachoma moto yale magari yaliyokuwa yamewekwa wakfu kwa jua.
12 Alizivunja madhabahu ambazo wafalme wa Yuda walikuwa wamezijenga kwenye paa la ghorofa ya Ahazi, pia madhabahu alizokuwa amezijenga Manase katika nyua mbili za Hekalu la Bwana. Akaziondoa huko, akazivunja vipande vipande, na kutupa hicho kifusi katika Bonde la Kidroni. 13 Mfalme pia akanajisi mahali pa juu pa kuabudia miungu, palipokuwa mashariki ya Yerusalemu upande wa kusini wa Kilima cha Uharibifu, pale ambapo Solomoni mfalme wa Israeli alikuwa amejenga kwa ajili ya Ashtorethi mungu mke chukizo la Wasidoni, kwa ajili ya Kemoshi mungu chukizo la Wamoabu, na kwa ajili ya Moleki mungu chukizo la watu wa Amoni. 14 Yosia akapasua yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Ashera. Kisha akafunika hayo maeneo kwa mifupa ya wanadamu.
15 Hata madhabahu yaliyokuwa huko Betheli, mahali pa juu pa kuabudia miungu palipokuwa pamejengwa na Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya Israeli watende dhambi, alibomoa hata hayo madhabahu na mahali pa juu pa kuabudia miungu. Alipateketeza kwa moto hapo mahali pa juu pa kuabudia miungu na kupasaga hadi pakawa vumbi, na kuichoma hiyo nguzo ya Ashera pia. 16 Kisha Yosia akatazama huku na huko, naye alipoona makaburi yaliyokuwa huko kwenye kilima, akaamuru mifupa itolewe humo na akaichoma juu ya madhabahu ya Betheli ili kupanajisi. Hili lilitokea kulingana na neno la Bwana lililosemwa na mtu wa Mungu ambaye alitangulia kusema mambo haya.
17 Mfalme akauliza, “Lile kaburi lenye mnara wa ukumbusho ninaloliona ni kwa ajili gani?”
Watu wa mji wakasema, “Hii ni alama ya kaburi la mtu wa Mungu aliyekuja kutoka Yuda, naye akanena dhidi ya hii madhabahu ya Betheli mambo yale yale uliyoifanyia leo.”
18 Akasema, “Liacheni, msiliguse. Msimruhusu mtu yeyote kuiondoa mifupa yake.” Basi wakaiacha mifupa yake pamoja na ile ya yule nabii ambaye alikuwa amekuja kutoka Samaria.
19 Kama alivyokuwa amefanya huko Betheli, Yosia akabomoa na kunajisi mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu ambapo wafalme wa Israeli walikuwa wamejenga ndani ya miji ya Samaria, ambayo ilikuwa imemghadhibisha Bwana. 20 Yosia akawachinja makuhani wote wa mahali pa juu pa kuabudia miungu katika madhabahu zao wenyewe, na kuchoma mifupa ya wanadamu juu yake. Kisha akarudi Yerusalemu.
Yosia Aadhimisha Pasaka
21 Mfalme akatoa agizo hili kwa watu wote: “Adhimisheni Pasaka kwa Bwana Mungu wenu, kama ilivyoandikwa katika Kitabu hiki cha Agano.” 22 Hapakuwahi kuwepo na adhimisho lingine la Pasaka kama hilo tangu nyakati za Waamuzi walioongoza Israeli, wala katika nyakati zote za wafalme wa Israeli na wafalme wa Yuda. 23 Lakini katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Yosia, Pasaka hii iliadhimishwa kwa Bwana huko Yerusalemu.
24 Zaidi ya hayo, Yosia akawaondoa waaguzi, wanaoabudu mizimu, sanamu za kuagulia, sanamu za kuabudiwa, na vitu vingine vyote vya machukizo vilivyoonekana huko Yuda na Yerusalemu. Aliyafanya haya ili kutimiza matakwa ya sheria iliyoandikwa ndani ya kile kitabu ambacho Hilkia kuhani alikipata ndani ya Hekalu la Bwana. 25 Kabla wala baada ya Mfalme Yosia hapakuwepo na mfalme mwingine yeyote ambaye alimpenda Bwana kwa moyo wake wote, kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na Sheria yote ya Mose.
26 Hata hivyo, Bwana hakuacha ghadhabu yake iliyowaka dhidi ya Yuda kwa sababu ya yale yote ambayo Manase alikuwa amefanya kumghadhibisha. 27 Hivyo Bwana akasema, “Nitamwondoa Yuda mbele zangu kama nilivyomwondoa Israeli, nami nitaukataa Yerusalemu, mji niliouchagua, na Hekalu hili, ambalo nilisema, ‘Jina langu litakaa humo.’ ”
28 Matukio mengine ya utawala wa Yosia na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
29 Yosia alipokuwa mfalme, Farao Neko mfalme wa Misri akapanda mpaka Mto Frati kumsaidia mfalme wa Ashuru. Mfalme Yosia akatoka kwenda kupigana naye, lakini Neko akamkabili na kumuua huko Megido. 30 Watumishi wa Yosia wakauleta mwili wake katika gari la vita kutoka Megido hadi Yerusalemu, wakamzika kwenye kaburi lake mwenyewe. Nao watu wa nchi wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta na kumfanya mfalme mahali pa baba yake.
Yehoahazi Mfalme Wa Yuda
(2 Nyakati 36:2-4)
31 Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miezi mitatu. Jina la mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia kutoka Libna. 32 Akafanya maovu machoni mwa Bwana, kama baba zake walivyofanya. 33 Farao Neko akamfunga kwa minyororo huko Ribla katika nchi ya Hamathi ili asiweze kutawala huko Yerusalemu, naye akatoza kodi ya talanta mia moja*Talanta 100 za fedha ni sawa na tani 3.4. za fedha, na talanta moja ya dhahabuTalanta moja ya dhahabu ni sawa na kilo 34. katika Yuda. 34 Farao Neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia kuwa mfalme mahali pa baba yake Yosia, na kulibadilisha jina la Eliakimu kuwa Yehoyakimu. Lakini akamchukua Yehoahazi na kumpeleka Misri, naye akafia huko.
Yehoyakimu Mfalme Wa Yuda
(2 Nyakati 36:5-8)
35 Yehoyakimu akamlipa Farao Neko ile fedha na dhahabu aliyodai. Ili kuweza kufanya hivyo, Yehoyakimu akatoza nchi kodi na kulipiza fedha na dhahabu kutoka kwa watu wa nchi kulingana na makadrio ya mapato yao.
36 Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake aliitwa Zebida binti Pedaya kutoka Ruma. 37 Naye akafanya maovu machoni mwa Bwana, kama baba zake walivyokuwa wamefanya.

*23:33 Talanta 100 za fedha ni sawa na tani 3.4.

23:33 Talanta moja ya dhahabu ni sawa na kilo 34.