13
Amnoni Na Tamari
Ikawa baada ya hayo, Amnoni mwana wa Daudi akampenda Tamari, umbu lake Absalomu mwana wa Daudi, ambaye alikuwa mzuri wa sura.
Amnoni akasumbuka sana kuhusu Tamari hata akaugua, kwa kuwa Tamari alikuwa bikira, na ilionekana kwamba haiwezekani Amnoni kumfanyia jambo lolote.
Basi Amnoni alikuwa na rafiki jina lake Yonadabu mwana wa Shimea,*Shimea pia hutamkwa Shama. nduguye Daudi. Yonadabu alikuwa mtu wa hila nyingi sana. Akamuuliza Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme; kwa nini siku baada ya siku unaonekana kukonda? Hutaniambia?”
Amnoni akamwambia, “Ninampenda Tamari, dada yake Absalomu ndugu yangu.”
Yonadabu akamwambia, “Nenda ukalale kitandani na ujifanye kuwa mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona mwambie, ‘Ningependa Tamari dada yangu aje kunipatia chochote ili nile. Tafadhali mruhusu aje na kuniandalia chakula mbele yangu ningali ninamwona, ili nipate kula kutoka mkononi mwake.’ ”
Kwa hiyo Amnoni akalala kitandani kujifanya mgonjwa. Mfalme alipokuja kumwona, Amnoni akamwambia, “Ningependa dada yangu Tamari aje na kuniandalia mikate maalum mbele yangu, ili nipate kula toka mkononi mwake.”
Daudi akampelekea Tamari ujumbe huko kwenye jumba la kifalme, kusema: “Nenda katika nyumba ya ndugu yako Amnoni ukamwandalie chakula.” Kwa hiyo Tamari akaenda nyumbani kwa nduguye Amnoni, ndugu ambaye alikuwa amelala. Tamari akachukua unga uliotiwa chachu akaukanda, akaiandaa mikate mbele yake na kuioka. Tamari akaondoa mikate kwenye kikaango ili ampatie Amnoni, lakini akakataa kula.
Amnoni akamwambia, “Mtoe nje kila mtu aliyeko hapa.” Kwa hiyo kila mmoja akaondoka. 10 Ndipo Amnoni akamwambia Tamari, “Leta mkate hapa ndani ya chumba changu ili nipate kula kutoka mkononi mwako.” Basi Tamari akachukua mikate aliyoiandaa na kumletea Amnoni ndugu yake ndani ya chumba chake. 11 Lakini alipompelekea ili ale, akamkamata kwa nguvu na kumwambia, “Njoo ulale nami, dada yangu.”
12 Akamwambia, “Usifanye hivyo, ndugu yangu! Usinitende jeuri! Jambo la namna hii halistahili kufanyika katika Israeli! Usitende jambo hili ovu. 13 Kwa upande wangu je, itakuwaje? Nitaipeleka wapi aibu yangu? Pia kwa upande wako, itakuwaje? Utakuwa kama mmoja wa wapumbavu waovu katika Israeli. Tafadhali zungumza na mfalme; hatakukatalia wewe kunioa,” 14 Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza, na kwa kuwa alikuwa na nguvu kuliko Tamari, akamtenda jeuri.
15 Kisha Amnoni akamchukia Tamari, kwa machukio makuu sana. Kwa kweli, Amnoni alimchukia kuliko alivyokuwa amempenda. Amnoni akamwambia, “Inuka na utoke nje!”
16 Tamari akamwambia, “Hapana! Kunifukuza itakuwa vibaya zaidi kuliko yale uliyonitendea.”
Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza. 17 Akamwita mtumishi wake mahsusi na kumwambia, “Mtoe huyu mwanamke hapa na ufunge mlango nyuma yake.” 18 Kwa hiyo, mtumishi wake akamtoa nje na kufunga mlango nyuma yake. Tamari alikuwa amevaa joho lililopambwa vizuri, kwa maana lilikuwa aina ya mavazi yaliyovaliwa na binti za mfalme waliokuwa mabikira. 19 Tamari akajitia majivu kichwani mwake na kurarua lile joho alilokuwa amevaa. Akaweka mkono wake kichwani, akaenda zake akilia kwa sauti.
20 Absalomu nduguye akamuuliza, “Je, huyo Amnoni ndugu yako, amekutana nawe kimwili? Sasa nyamaza umbu langu, yeye ni ndugu yako. Usilitie jambo hili moyoni.” Naye Tamari akaishi nyumbani kwa Absalomu nduguye, akiwa mwanamke mwenye huzuni.
21 Mfalme Daudi aliposikia mambo haya yote, akakasirika sana. 22 Absalomu hakusema neno lolote na Amnoni, likiwa zuri au baya, kwa kuwa alimchukia Amnoni kwa sababu alikuwa amemtia aibu Tamari, dada yake.
Absalomu Amuua Amnoni
23 Miaka miwili baadaye, wakati wakata manyoya ya kondoo wa Absalomu walipokuwa huko Baal-Hasori karibu na mpaka wa Efraimu, alialika wana wote wa mfalme kuja huko. 24 Absalomu akaenda kwa mfalme na kumwambia, “Mtumishi wako ninao wakata manyoya ya kondoo waliokuja. Tafadhali, je, mfalme na maafisa wake wanaweza kuungana nami?”
25 Mfalme akajibu, “La hasha, mwanangu si lazima sisi sote tuje, tutakuwa tu mzigo kwako.” Ingawa Absalomu alimsihi sana, mfalme alikataa kwenda, lakini alimbariki.
26 Basi Absalomu akasema, “Kama hutakuja, tafadhali mruhusu ndugu yangu Amnoni twende pamoja naye.”
Mfalme akamuuliza, “Kwa nini aende pamoja nawe?” 27 Lakini Absalomu alimsihi, kwa hiyo mfalme akamtuma Amnoni pamoja na wana wengine wa mfalme waliobaki.
28 Absalomu aliagiza watu wake, “Sikilizeni! Wakati Amnoni atakapokuwa amekunywa mvinyo na kulewa sana nami nikiwaambia, ‘Mpigeni Amnoni,’ basi muueni. Msiogope. Je, si mimi niliyewapa amri hii? Kuweni hodari na wenye ushujaa.” 29 Kwa hiyo watu wa Absalomu wakamtendea Amnoni kama vile Absalomu alivyokuwa amewaagiza. Ndipo wana wote wa mfalme wakainuka, wakapanda nyumbu zao, wakakimbia.
30 Wakati wakiwa njiani, taarifa ilimjia Daudi, kusema: “Absalomu amewaua wana wote wa mfalme; hakuna hata mmoja aliyesalia.” 31 Mfalme akasimama, akararua nguo zake, akalala chini ardhini; nao watumishi wake wote wakasimama kando yake na nguo zao zikiwa zimeraruliwa.
32 Lakini Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akasema, “Bwana wangu asifikiri kwamba wamewaua wana wote wa mfalme; ni Amnoni peke yake ndiye alikufa. Hili limekuwa kusudi la moyo wa Absalomu tangu siku ile Amnoni alipomtendea jeuri Tamari, dada yake. 33 Mfalme bwana wangu asisumbuliwe na taarifa kwamba wamewaua wana wote wa mfalme. Ni Amnoni peke yake aliyekufa.”
34 Wakati huo, Absalomu akawa amekimbia.
Basi mlinzi akaangalia, naye akaona watu wengi barabarani magharibi yake, wakishuka kutoka upande wa kilima. Mlinzi akaenda akamwambia mfalme, “Naona watu wakitokea upande wa Horonaimu, huko upande wa kilimani.”
35 Yonadabu akamwambia mfalme, “Tazama, wana wa mfalme wako hapa; imekuwa kama vile mtumishi wako alivyosema.”
36 Mara alipomaliza kusema, wana wa mfalme wakaingia ndani wakiomboleza kwa makelele. Pia mfalme na watumishi wake wote wakalia sana kwa uchungu.
37 Absalomu akakimbia na kwenda kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa Geshuri. Lakini Mfalme Daudi akaomboleza kwa ajili ya mwanawe kila siku.
38 Baada ya Absalomu kukimbia na kwenda Geshuri, akakaa huko miaka mitatu. 39 Roho ya Mfalme Daudi ikatamani kumwendea Absalomu, kwa maana mfalme alikuwa amefarijika kuhusu kifo cha Amnoni.

*13:3 Shimea pia hutamkwa Shama.